REA YAANZA KUTEKELEZA AGIZO LA SERIKALI LA KUSAMBAZA MAJIKO YA GESI WILAYANI CHATO

 

*Majiko ya gesi 3,255 yaanza kununuliwa kwa bei ya ruzuku*

Wananchi wilayani Chato mkoa wa Geita wanaendelea na zoezi la kununua majiko ya gesi ya kilo 6 yapatayo 3,255; kutoka kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupitia msambazaji, kampuni ya MANJIS Logistic Ltd ambapo tarehe 7 Disemba, 2024 katika kijiji cha Msilale Katibu Tawala wa wilaya hiyo Bwana Thomas Dimme alishiriki kwenye zoezi la ugawaji wa majiko hayo na kusisitiza kuwa ipo haya Serikali kuongeza mgao wa majiko hayo kwa kuwa mwamko ni mkubwa.

Bwana Thomas Dimme amesema Viongozi wa wilaya wanaendelea na zoezi la kuwahamasisha Wananchi ili wajitokeze kwa wingi katika kata za wilaya hiyo ili wanufaike na fursa hiyo ya kununua majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku ya shilingi 17,500 ambayo Serikali imewalipia kupitia REA badala ya shilingi 35,000, bei ya awali.

“Kwa upande wetu, tunaendelea kuwahamasisha Wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ili wajitokeze kwa wingi kununua majiko haya, yanayotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia REA kwa bei ya punguzo ya asilimia 50.” Ameeleza, Katibu Tawala wa wilaya, Bwana, Dimme.

Aidha, Dimme ameiomba Serikali kuongeza mgao zaidi katika wilaya ya Chato kwa kuwa uhitaji ni mkubwa pamoja na kuomba ruzuku kwenye gharama ya kujaza mitungi hiyo mara gesi itakapoisha.

“Sisi Wilaya yetu tupo wengi, tunazaa kwa wingi, niombe Mamlaka (Serikali) watuongezee mgao zaidi, jambo la pili tunaomba waweke utaratibu wa ruzuku ya kuweza kujaza hii mitungi.” Amesema Bwana Dimme.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Mhandisi, Francis Manyama amesema ili Mwananchi apate jiko hilo la gesi, anatakiwa kuja kwenye vituo vilivyotangazwa kwa ajili ya kugawa majiko hayo akiwa na Kitambulisho cha NIDA au namba ya NIDA pamoja na shilingi 17,500.

“Serikali kupitia REA inatekeza mikakati hii, Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania, wawe wanatumia nishati safi ya kupikia”. Amesema, Mhandisi, Manyama.

Itakumbukwa, tarehe 2 Disemba, mwaka huu, Mkuu wa mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigela, aliupokea rasmi Mradi kusambaza majiko hayo ya gesi yapatayo 16,275 kwa mkoa mzima; majiko yenye thamani ya shilingi milioni 285 katika hafla iliyofanyika ofisi kwake na alitoa wito kwa Wananchi kuchangamkia fursa hiyo.

Related Posts