KIKOSI cha Serengeti Boys, kinaendelea na maandalizi yake kwa ajili ya michuano ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) U17 kwa kanda ya CECAFA, itakayofanyika kuanzia Desemba 14 hadi 28, 2024, Uganda.
Katika maandalizi hayo, kocha wa kikosi hicho, Agrey Morris, alisema kuwa timu yake iko katika hali nzuri na inajiandaa kikamilifu kwa mashindano hayo. Alieleza kuwa wachezaji wanazidi kuimarika kila siku na wanajua kabisa umuhimu wa michuano hiyo kwa ajili ya maendeleo ya soka la vijana Tanzania.
“Maandalizi yetu yanaendelea vizuri, tunafanya kila kitu kwa bidii ili kuhakikisha kwamba tunakuwa na timu imara kwa michuano ya kufuzu AFCON. Wachezaji wanajitahidi na wana ari kubwa ya kushinda. Lengo letu ni kufuzu kwa michuano ya AFCON U17 na tutahakikisha tunafanya kila lililo bora ili kulifikia hilo,” alisema Morris.
Katika kuwapa hamasa wachezaji wa kikosi hicho, siku chache zilizopita Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, liwatembelea wachezaji hao na kuwatia moyo katika maandalizi yao wakiwa chini ya Morris na Boniface Pawasa.
Wakati akizungumza nao, Karia alisisitiza umuhimu wa michuano hiyo kwa ustawi wa soka la vijana Tanzania na kuwahimiza wachezaji kuwa na nidhamu ya hali ya juu na kujituma kwa ajili ya taifa lao.
“Serengeti Boys ni matumaini yetu katika kuendeleza soka la vijana na kuleta mafanikio kwa taifa letu. Nawaahidi wachezaji wote kuwa TFF itaendelea kuwaunga mkono katika kila hatua ya maandalizi haya, na tunatarajia mafanikio makubwa kutoka kwao,” alisema Karia.
Kwa mujibu wa Yusuf Mossi, Mkurugenzi wa Mashindano wa CECAFA, nchi tisa kutoka kanda ya CECAFA zitashiriki kwenye michuano hii ya kufuzu, ambazo ni Uganda, Burundi, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudan Kusin, na Tanzania.
Nchi hizo zitakuwa na nafasi ya kupigania moja ya nafasi mbili za juu (fainali) zitakazowapa tiketi ya kushiriki AFCON U17 2025.
Mashindano ya kufuzu yatachezwa kwenye miji ya Bukedea, Mbale, na Kampala, Uganda, na timu zote zitakuwa na jukumu la kufanya vipimo vya Magnetic Resonance Imaging (MRI) kwa wachezaji wao kabla ya kuingia uwanjani.