Geita. “Mume wangu alipoteza maisha 1998, mtoto wangu wa tatu akafa mwaka 1999 hali yangu ilikua mbaya sana mwili ulidhoofika, nikawa na upele kila mahali, nywele zote kichwani zilinyonyoka, kikawa kimejaa vidonda na nilikua natokewa na mkanda wa jeshi mara kwa mara hata sikuweza kumzika mwanangu.”
Ndivyo anavyoanza kusimulia Mchungaji, Ester Mhangwa wa Kanisa la TAG, lililopo Kijiji cha Chabulongo Kata ya Kasamwa Mjini Geita, anayeishi na VVU kwa miaka 39 huku akiendelea kuamini katika nguvu ya dawa za kufubaza maambukizi ya ugonjwa huo ARV.
“Maisha yangu yalikuwa ya kawaida, nilikua binti mzuri wakati napata maambukizi mwaka 1985 nilikua nimetoka jeshini na kupangiwa kazi ya ualimu Shule ya Msingi Mkuyuni, Manispaa ya Mwanza (sasa jiji),” anasimulia.
Anasema kutokana na ujana na msongo wa mawazo alioupata baada ya kutoka jeshini na kukuta aliyekua mpenzi wake ameoa, aliingia kwenye uhusiano na mwanaume ambaye hakuwa amemfahamu kiundani.
Wakiwa kwenye uhusiano, mwaka 1987 alipata ujauzito na kuanza mipango ya ndoa, hivyo alilazimika kwenda kupima maambukizi katika Hospitali ya Bugando na daktari aliyewachukua vipimo, alionyesha wasiwasi wa wao kutokuwa sawa, lakini akawaeleza wataelezwa vizuri na wauguzi.
“Daktari alituambia wazi kuwa damu zetu haziendani, lakini akasema wauguzi watatueleza siku tukija kuchukua majibu, wakati huo ulikua ukipima majibu ni baada ya wiki mbili kwa kuwa tulikua na afya nzuri, wanene, tuliamini hatuna maambukizi na mume wangu akawa anasema daktari anamuonea wivu kwa kuwa mimi ni mzuri,” anasema Ester.
Anasema baada ya wiki mbili walirudi hospitali kuchukua vipimo ambavyo kabla ya kupewa, walipita kwa watu watatu tofauti waliowapatia ushauri nasaha ili kuwaandaa kupokea majibu.
“Zamani Ukimwi ulijulikana kwa jina la Juliana na watu walikua wanakonda sana kwa kuwa sisi tulikua na afya nzuri, hata kwenye ushauri sisi tuliona kawaida, kifupi hatukukubali kuwa tumeathirika, tulipewa majibu lakini hatukuyaamini,” anasema mchungaji huyo.
Mwaka 1988 walifanikiwa kupata mtoto wao wa kwanza ambaye hakwa ameathirika na wakati huo mume wake alikua mfanyakazi wa basi la Tanganyika na yeye akiendelea na kazi ya ualimu.
Baadaye wakapata mtoto wa pili aliyezaliwa na maambukizi na kutokana na kuugua, aliishi muda mfupi na akapoteza maisha.
Anasema mwaka 1989 mume wake alianza kushambuliwa na magonjwa ya mara kwa mara na yeye mwenyewe kupata msongo wa mawazo na kukutana na daktari, aliyewaeleza ugonjwa huo hauuwi kama watakubali kutumia dawa.
“Mwaka 1989 Mwanza uwanja wa Furahisha kulikuwa na mkutano wa injili yule mchungaji aliniuliza unataka nini mimi nilimwambia nataka Mungu anipe maisha marefu walau wanangu wakue, maana hali zetu zilikuwa mbaya na alituombea,” anasimulia mchungaji Ester.
Anasema kwa mara ya kwanza alijitangaza kuwa muathirika mwaka 1989 baada ya kupata washauri na kupewa dawa ya ‘fightdefence’, ambayo iliwasaidia waathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na mashambulizi ya mkanda wa jeshi.
Anasema mwaka 1998, mume wake alifariki dunia na mwaka uliofuatia mwanawe wa tatu naye akafariki dunia, hata hivyo anasema hakuweza kumzika kutokana na hali yake kiafya kuwa mbaya.
“Mimi nimeugua mkanda wa jeshi zaidi ya mara tano na nilidhoofika sana, mwaka 1999 Rais Mkapa akatangaza mfanyakazi anaweza kuacha kazi kwa hiari na mimi kutokana na hali yangu niliomba kuacha kwa hiari, mwili wangu ulikua umedhoofika, una madonda na nywele zilikua zimenyonyoka,” anasimulia historia yake.
Anasema aliendelea kutumia dawa za Wachina alizopatiwa hospitali na katika kutafuta matibabu, alienda kuombewa ili apone na baada ya maombi alitakiwa kuacha dawa kwa miaka mitatu lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya zaidi.
Anasema miaka ya nyuma yeye mwenyewe alijitenga na kujikataa huku akiona kifo mbele yake, lakini kwa msaada wa familia na ndugu kumshika mkono na kumtia moyo, imemsaidia kwenye safari yake ya miaka 39 anayoishi na VVU.
Anasema changamoto kubwa wanazokutana nazo watu wenye VVU ni unyanyapaa kutoka kwa ndugu wa karibu na jamii yenyewe, hivyo kuwafanya wakate tamaa na wasione kama maisha yana faida kwao.
Anasema pamoja na mtoto wake wa kwanza na wanne kutokuwa na maambukizi, lakini walikumbana na unyanyapaa kwenye jamii uliompa msongo wa mawazo mtoto wake wa mwisho na hadi sasa hajakaa sawa.
“Mwanangu ile hali ya kusemwa na watoto wenzake na kunyooshewa vidole na watu kuwa ni mtoto wa muathirika ilimpa msongo wa mawazo akawa mtu wa kujitenga anakaa mwenyewe, hana marafiki licha ya kusoma hadi chuo kikuu lakini hajakubaliana na hali na hata sasa inaathiri akili yake, hawezi kufanya kitu hii yote imechangiwa na unyanyapaa kwenye jamii,” anasema.
Namna alivyoishinda hali ya maumivu
“Kwanza nimezingatia suala la kujilinda na kula vizuri, najipenda na kujipa amani mwenyewe. Vitu vyote hivi vinaanzia kwa wewe mwenyewe kwa kuwa ukijipenda utapendeka, ukijiamini utaaminika hivyo ukijipenda utajali uhai wako na kumtanguliza Mungu mbele,” anasema.
“Mimi huwa namshukuru Mungu kila wakati nasimama na neno. Nakushukuru Mungu maana ukimsamehe mtu unamponya na magonjwa yake yote na kuuepusha uhai wake na mauti unamvika taji la fadhili na rehema na Mungu ameushibisha vema uzee wangu sasa nimezeeka lakini bado afya yangu inaonekana ya kijana”anasema mchungaji huyo.
Anasema anapoishi na VVU ni imani yake kuwa nako ni kumtumikia Mungu, magonjwa yake yatapona na amekuwa mtu wa kupima afya mara kwa mara.
Anasema kwa sasa haugui tena shinikizo la damu wala tatizo jingine lolote, “Mungu ameshinda kila ugumu kwenye maisha yangu na mimi ni mfano wa jinsi ya kuishi na VVU kwa matumaini na imani kubwa.”
Imani kwenye maombi na dawa za kisasa
Kwa maoni yake, mchungaji huyo anasema dawa za kisasa ni zawadi kutoka kwa Mungu. “Yesu alisema, ‘Imani yako imekuponya.’ Hii ina maana hatupaswi kudharau vipawa vya wengine ambavyo Mungu ameweka kwa lengo la kutimiza kusudi lake hapa duniani.”
Anasema anaamini yeye ni mzima bila kujali ana VVU na yaliyoujaza moyo wake ndio yanayoonekana kwa nje.
Anasema wote wanaowazuia waviu kutotumia dawa za ARV wakati wakiuugua magonjwa mengine wanatumia dawa ni sawa na kumdhihaki Mungu.
Amewataka watu kufungua akili na kuamini Mungu yupo lakini hakatazi kutumia dawa zinazotengenezwa na binadamu kwa lengo la kuponya magonjwa.
Athari alizopata baada ya kuacha kutumia dawa
Baada ya kuacha kutumia dawa kwa miaka mitatu, anasema hali yake kiafya ilizorota sana. Mkanda wa jeshi, ambao alidhani amepona, ulimrudia tena kwa kasi.
Anasema alianza kupata majipu makubwa mwilini, hali iliyosababisha ngozi ya kichwa kuoza.
“Magonjwa yote niliyowahi kuyapata awali yalianza kunirudia moja baada ya jingine, na mwili wangu ulidhoofika kupita kiasi,” anasema.
Elimu kwa wanawe kuhusu VVU
Mchungaji huyo anasema akiwa mama wa watoto wawili, anajitahidi kuwapa mafunzo bora kuhusu VVU na namna ya kuishi kwa usalama.
“Nimekuwa ushuhuda hai kwao na wanajifunza kutokuwa na hofu au aibu kuhusiana na ugonjwa huu,” anasema Ester.
Anasema wanawe wamejifunza umuhimu wa kujilinda dhidi ya maambukizi na kuwa wa wazi kuhusu mama yao.
Anasema ndani ya familia yao pia wana mtoto aliyezaliwa na maambukizi ya VVU lakini anajitambua na anaishi kwa uwazi, anajipenda, na sasa anasoma chuo kikuu.
Akizungumzia unyanyapaa, anasema ni changamoto kubwa kwa watu wanaoishi na VVU.
Lakini anasema jamii inapaswa kuelewa kwamba si kila mtu mwenye VVU ameupata kwa njia ya ngono bali wapo walioupata kwa njia nyingine.
Hivyo, ameiasa jamii kuacha kuwanyanyapaa au kuwatenga watu wenye VVU na badala yake wawapende, wawaheshimu na kuwapa ushirikiano ili kuwasaidia kuishi maisha yenye matumaini na heshima.
Mchungaji Ester anasema watu wengi wanapoombewa huacha dawa kwa kuambiwa kwa mdomo bila kupima. Hivyo, anatoa rai watu wapime mara kwa mara na wenye maambukizi wasikubali kuacha dawa.
Mchungaji Ester anasema wapo vijana wengi waliozaliwa na VVU na wanatumia dawa lakini wanapopata wenza, wanashindwa kujiweka wazi kwao hali inayochochea maambukizi mapya.
Anaitaka jamii iunge mkono juhudi za Serikali za kutokomeza maambukizi ya VVU nchini.
Anasema Serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kuwafikia waathirika na kuwapa dawa, lakini kama haitakubali kuwa wazi na kueleza hali zao ni rahisi kwa nchi kuendelea kupata maambukizi mapya ya VVU kila mara.