Ujenzi wa nyumba Hanang wakamilika

Arusha. Tabasamu lakaribia kurejea. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mwaka mmoja tangu kutokea kwa maafa yaliyosababishwa na maporomoko ya mawe, tope na miti kutoka Mlima Hanang yaliyotokea Desemba 3, 2023 wilayani Hanang mkoani Manyara.

Kaya 108 zilizokosa makazi kutokana na maafa hayo zinatarajia kurejesha tabasamu tena baada ya ujenzi wa nyumba 108 zilizojengwa kwa ajili yao kukamilika.

Wilaya ya Hanang ilikumbwa na maafa yaliyosababishwa na maporomoko hayo na watu 89 walipoteza maisha, huku 139 wakijeruhiwa na mamia wakiachwa bila makazi.

Lakini pia kulitokea uharibifu mkubwa wa miundombinu ikiwamo barabara, madaraja, nguzo za umeme na masoko.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Desemba 8, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema ujenzi umekamilika kwa asilimia 100 na kwa sasa wanasubiri maelekezo ya Serikali.

“Tunashukuru ujenzi wa zile nyumba umemalizika, kila kitu kiko tayari ila kwa sasa tunasubiri maelekezo ya Serikali kuhusu utaratibu unaofuata ikiwemo makabidhiano ya nyumba hizo,”amesema mkuu huyo wa mkoa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Almishi Hazali amesema mbali na ujenzi wa nyumba hizo, miundombinu mingine ikiwemo ya maji, barabara, umeme na hati za nyumba hizo vimeshakamilika.

Nyumba hizo 108 zimejengwa katika eneo la Gdagamowd, lililopo wilayani Hanang mkoani Manyara.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dk Jim Yonazi, Serikali imetenga eneo la ekari 100 ambako jumla ya viwanja 269 vimepimwa na kati ya hivyo, 226 ni makazi pekee, 26 ni makazi na biashara na 17 ni maeneo ya huduma za kijamii.

Oktoba 7, mwaka huu Serikali iliweka wazi ripoti kuhusu chanzo cha maporomoko hayo na kuwasihi wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kutorejea kwenye maeneo hatarishi waliyoondolewa.

Ripoti hiyo iliyotolewa na kamati maalumu ya wataalamu waliopewa kazi ya kuchunguza tukio hilo, imebaini kuwa maporomoko hayo yalisababishwa na mipasuko kwenye miamba ambayo ilikuwa ikihifadhi maji ya mvua nyingi zilizonyesha mfululizo.

Hali hiyo ilisababisha miamba kushindwa kuhimili uzito na hivyo kusababisha udongo kuserereka na kuleta maafa hayo.

Mkurugenzi wa huduma ya jiolojia kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa madini Tanzania (GST), Dk Ronald Massawe, alisema tathmini hiyo ilifanyika Aprili mwaka huu na ilihusisha wataalamu kutoka vyuo vikuu mbalimbali kikiwamo Chuo cha Kilimo cha Morogoro (Sokoine), Chuo Kikuu cha Ardhi na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA).

 “Kwa ushauri wa kitaalamu, tunawashauri wananchi wasikae katika maeneo hatarishi ili kuepuka madhara iwapo tukio kama hili litajitokeza tena.”

“Kabla ya Desemba 3, 2023 ambayo ndiyo siku maafa hayo  yalitokea, mlima ulikuwa umenyeshewa na umenyonya maji kwa muda mrefu,  kwa sababu kuna nyufa nyingi, maji yaliyokuwa yamehifadhiwa yakaanza kutoka hivyo  mlima ukashindwa kuhimili uka ukaserereka na kusababisha maporomoko,”alieleza.

Related Posts