Waajiri na viongozi ofisi za umma wapewa neno,matumizi ya Kiswahili Sanifu na Fasaha katika nyaraka mbalimbali

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa amewataka Waajiri na Viongozi katika ofisi za umma kuwapa fursa Waandishi Waendesha Ofisi (Masekretari) kuwasidia katika uandishi kwa kutumia Kiswahili sanifu na fasaha katika nyaraka mbalimbali badala ya Maboss hao kung’ang’ania kuandika wenyewe na mwisho kupelekea makosa mengi kwenye nyaraka.

Msigwa amesema hayo Mkoani Morogoro wakati akifunga Mafunzo ya Matumizi ya Kiswahili Sanifu na Fasaha kwa Waandishi Waendesha Ofisi yaliyosimamiwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ambapo amesema kwakuwa Viongozi na Waajiri wengi wana kazi nyingi za kufanya zinazowafanya wakose muda wa kuandika Kiswahili sanifu na fasaha, inabidi wawape fursa Waandishi Waendesha Ofisi wao kwasababu wamepata mafunzo ya namna ya kuandika kiswahili Sanifu na Fasaha.

“Fanyeni utafiti, nyaraka nyingi za ofisi ambazo zina makosa mengi ni zile ambazo Maboss wamejifungia wanaandika wao, anaandika akiwa na stress, huku kavurugwa, anakimbizana na muda na mambo mengine mengi analeta nyaraka zina makosa, niwaombe tunapofanya kampeni hii onesheni tofauti, Boss akiandika mwenyewe na utakayoandika wewe ziwe na tofauti, wale ni Binadamu na wameumbiwa na aibu, akiona anapiga boko nyingi kwenye nyaraka ataacha”

Msigwa amewataka pia Viongozi kuwapeleka Waandishi Waendesha Ofisi wao katika mafunzo ya matumizi ya Kiswahili sanifu na fasaha na mafunzo mengine ya ndani na nje ya nchi ili waweze kuwasaidia vizuri kwakuwa ndio Wasaidiz wao wa karibu katika uandaaji wa taarifa na nyaraka mbalimbali za kiofisi.

Related Posts