Wadau wataka hatua zichukuliwe kukabili mimba za utotoni Songwe

Songwe. Wakati Nyanda za Juu Kusini ikitajwa kuwa miongoni mwa Kanda zenye mimba za utotoni nyingi, Songwe imekuwa Mkoa kinara kwa ukanda huo ikiwa na asilimia 45.

Takwimu hizo zimetolewa jana Desemba 7, 2024 na Mkurugenzi wa Jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi maalum, Badru Abdunun, kwenye mdahalo wa wazi uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe.

Mdahalo huo ulioandaliwa na Shirika la HJFMRI ulilenga kujadili masuala mbalimbali ikiwamo ukatili wa kijinsia na mimba za utotoni ikiwa ni kuelekea siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia duniani.

Abdunun amesema Songwe, Ruvuma, Katavi na Rukwa ni miongoni mwa mikoa mitano nchini inayoongoza kwa ndoa za utotoni ukiachia Mkoa wa Mara.

“Takwimu za mwaka 2023 zinaonyesha mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ina idadi kubwa ya mimba za utotoni, ambapo Songwe ndio kinara kwa kuwa na asilimia 45 ukifuatiwa na Ruvuma asilimia 37 na Mkoa wa  Katavi unashika nafasi ya tatu kwa kuwa na asilimia 34, Mara asilimia 30 na Rukwa ukiwa na asilimia  30 na kushika nafasi ya tano,” amesema Abdunun.

Hata hivyo, amesema sababu kubwa inayotajwa ni kukosekana kwa matunzo na  malezi bora katika ngazi ya familia.

“Bado tatizo linaendelea kuwa kubwa licha ya Serikali na wadau kuwekeza nguvu kupiga vita mimba za utotoni, hivyo ni jukumu letu sote kushirikiana katika vita hii,” amesema ofisa huyo.

Awali akifungua mdalalo huo, Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, John Mwaijulu alilishukuru Shirika la HJFMRI kwa kuratibu mdahalo huo ambao utaleta chachu katika vita dhidi ya mimba za utotoni.

“Tunakwenda kuhakikisha Mkoa wa Songwe unatoka katika asilimia hizo kwa kuelekeza  elimu ya athari za ukatili unaotokana na mimba za utotoni ili kusaidia watoto wa kike kutimiza ndoto zao,” amesema Mwaijulu.

Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee  Mkoa wa Songwe, Davis Songolo amesema tatizo kubwa la  mimba za utotoni linatokana na usimamizi mbovu kuanzia ngazi ya familia.

Amesema changamoto nyingine ni imani potofu za mila na desturi kwa mwanaume mmoja kuishi na mke zaidi ya mmoja, sambamba na wazazi kuona hakuna umuhimu wa mtoto wa kike kupata elimu.

“Niombe Serikali kufanya marekebisho ya sheria kwa  wazee na viongozi wa mila kutambuliwa ili waweze kushiriki katika kudhibiti malezi, makuzi na kurejesha maadili ya Mtanzania,” amesema Songolo.

Sophia Mwashambwa, ameishauri Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kuwawajibisha wazazi watakaobainika kukwepa majukumu ya malezi na kusababisha  kupatikana mimba za utotoni.

Related Posts