Fountain Gate yawinda straika Zenji

KLABU ya Fountain Gate iko katika hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa nyota wawili, beki wa kati Shabani Pandu Hassan na mshambuliaji Mudrik Abdi Shehe ‘Gonda’ kutokea JKU ya visiwani Zanzibar, ili kuongeza makali ya timu hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo, zililiambia Mwanaspoti nyota hao wako hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho huo na dirisha la usajili litakapofunguliwa Desemba 15, kila kitu kitakuwa kimekamilika ili wakaongeze nguvu kikosini humo.

“Ni kweli wachezaji wote tuko katika mazungumzo nao na yanaenda vizuri hadi sasa tulipofikia, ni pendekezo la benchi la ufundi ambalo limehitaji kuboreshewa maeneo hayo kutokana na mapungufu yaliyoonekana kikosini,” kilisema chanzo chetu.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate, Kidawawa Tabitha alisema huu ni muda wa kila mmoja wao kuzungumza jambo lolote linalohusu usajili kwa sababu wakati wake umekaribia, ingawa wataweka wazi watakapokamilisha.

Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua kocha wa timu hiyo, Mohamed Muya amewasilisha ripoti yake kwa viongozi na mojawapo ya maeneo ambayo amekuwa akihitaji kuongezewa nguvu ni eneo la mabeki wa kati, kutokana na kutokuwa na safu bora ya ulinzi.

Fountain iliyopo nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 17, licha ya kuonekana tishio katika kufunga ikiwa ya pili baada ya kutupia kambani mabao mengi (20), nyuma ya Simba yenye 22, ila imekuwa na eneo bovu la ulinzi.

Katika michezo 12 iliyocheza kikosi hicho kinachoongozwa na kinara wa ufungaji, Seleman Mwalimu mwenye mabao sita, ni timu ya pili msimu huu kwa kuruhusu mabao mengi ikifanya hivyo mara 21, nyuma ya KenGold inayoongoza kwa kufungwa 22.

Ujio wa Mudrik ambaye amefunga mabao manane katika Ligi Kuu ya Zanzibar msimu huu, unaenda kuongeza ushindani wa eneo la ushambuliaji akishirikiana na nyota, Seleman Mwalimu na Edgar William aliyefunga mabao manne ya Ligi Kuu Bara hadi sasa.

Related Posts