Dodoma/ Mbeya. Hofu ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, imeibuka katika mikoa ya Dodoma na Mbeya, huku mamlaka za afya zikiwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kufuata taratibu za usafi wa mazingira na chakula.
Waganga wakuu wa mikoa hiyo wamewatoa hofu wananchi juu ya viashiria vya ugonjwa huo, baada ya baadhi ya watu kuripotiwa kuharisha, hali inayotajwa kuwa ya tahadhari kwa uwezekano wa kusambaa kwa kipindupindu.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, mvua zinazoendelea kunyesha, zimeongeza uwezekano wa uchafu kuingia kwenye vyanzo vya maji.
Aidha, msimu wa matunda kama maembe umebainishwa kuwa mojawapo ya sababu zinazoweza kuchangia kuongezeka kwa wagonjwa wa kuharisha, hususan pale ambapo matunda hayo hayasafishwi vizuri kabla ya kuliwa.
Mamlaka za afya zimewasihi wananchi kuhakikisha wanatumia maji safi na salama, kunawa mikono kwa sabuni kabla ya kula na baada ya kutoka chooni, na kuhakikisha vyakula vyao vimepikwa ipasavyo.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dk Pima Sebastian amewatoa hofu wakazi wa Jiji la Dodoma kufuatia hofu iliyozuka kuhusu uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
Akizungumza leo Jumatatu, Desemba 9, 2024, Dk Sebastian ameeleza hakuna mgonjwa yeyote aliyepimwa na kuthibitishwa kuwa na kipindupindu, bali wagonjwa waliopo hospitalini wanasumbuliwa na matatizo ya kuhara.
“Kumekuwa na taarifa za kusambaa kuhusu mlipuko wa kipindupindu hapa Dodoma, hususan katika Kata ya Chang’ombe, lakini napenda kuwahakikishia wananchi kuwa hakuna mgonjwa hata mmoja aliyepatikana na ugonjwa huo,” amesema Dk Sebastian alipokuwa akizungumza na Mwananchi.
Dk Sebastian amebainisha mvua zinazoendelea kunyesha zimechangia mafuriko na maji kutuama, hali inayosababisha mazingira machafu kutokana na takataka kusombwa na maji na kufika kwenye makazi ya watu.
“Kwa sasa, uchafu unaosababishwa na maji ya mvua unaziba mitaro na kuleta changamoto kubwa ya usafi. Ni muhimu wakazi wa Dodoma wachukue hatua za kusafisha mazingira yao kwa kuzibua mitaro, kuchemsha maji ya kunywa, na kuhakikisha wanatunza miundombinu ya maji kwa usalama wa afya yao,” amesisitiza.
Dk Sebastian ametoa wito kwa wakazi wa Dodoma kuzingatia kanuni za usafi wa mazingira na afya kwa kusafisha mazingira, kuzibua mitaro na kuondoa taka zinazozagaa.
Amewataka wananchi kuhakikisha matumizi salama ya maji kwa kuchemsha maji ya kunywa na kuhakikisha kuwa maji yanayotumika ni salama.
Pia, amewataka wananchi kula vyakula vya moto kwa lengo la kupunguza hatari ya maambukizi ya magonjwa ya kuhara na kunawa mikono kabla ya kula na baada ya kutoka chooni.
Dk. Sebastian alitoa wito wa matumizi sahihi ya vyoo, akisisitiza ujenzi wa vyoo bora, visafi, na kuhakikisha vyoo vya shimo vinakuwa vimefunikwa wakati wote.
Pia, ameonya kuwa kujisaidia ovyo kunasababisha wadudu kama nzi kubeba vimelea vya magonjwa na kusambaza kwa haraka.
“Wakati wa Uviko-19 tulizingatia sana usafi wa mikono, na hilo lilisaidia sana kupunguza magonjwa ya mlipuko. Hivyo, ni lazima turejee utamaduni huo ili kujikinga na magonjwa ya kuhara na mengine yanayoweza kusababishwa na mazingira machafu,” amesema Dk Sebastian.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Elizabeth Nyema, amethibitisha hakuna tukio la ugonjwa wa kipindupindu lililoripotiwa mkoani humo hadi sasa.
Hata hivyo, amewataka wananchi kuwa waangalifu na kuchukua hatua za tahadhari kutokana na mvua zinazonyesha na msimu wa ulaji wa maembe, hali inayoweza kuchangia magonjwa ya milipuko.
“Kwa sasa hatuna mgonjwa yeyote mwenye viashiria vya kipindupindu, lakini ni muhimu wananchi wawe makini. Mvua zinazonyesha na tabia ya kutozoa taka kwa wakati, vinaweza kusababisha magonjwa ya kuhara. Pia, ni muhimu kuhakikisha maembe na matunda mengine yanaoshwa vizuri kabla ya kuliwa,” amesema Dk. Nyema.
Dk Nyema amehimiza wananchi kuzingatia usafi wa mazingira na kuepuka kushikana mara kwa mara mikononi.
“Kwa sababu tuko karibu na nchi za Malawi na Zambia ambako kipindupindu kimesharipotiwa, ni lazima tuwe waangalifu, hasa na wageni wanaoingia nchini kupitia maeneo ya mpakani,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Dk Nyema, Serikali imeweka wataalamu katika maeneo ya mpakani, kama vile Kasumulu na Uwanja wa Ndege wa Songwe, ili kuchunguza afya za watu wote wanaoingia na kutoka.
“Wataalamu wetu wana vifaa vya kutosha na wanaendelea kuchunguza wageni. Tunashukuru hadi sasa hatuna mgonjwa yeyote wa kipindupindu,” amesema.
Mmoja wa wananchi wa mtaa wa sokoine jijini humo, Angela Mwalimu amesema kutokana na mvua zinazonyesha Serikali ipambane kuhimiza takataka zinazokusanywa zinazotolewa haraka.
“Miundombinu ya Mbeya si rafiki kwa wote, kuna watu wanaoishi milimani na mabondeni ambao wanakumbana na changamoto kubwa wakati wa mvua. Ni muhimu wale wanaosimamia usafi wa mji kujitahidi kwenda na kasi ya hali ya sasa,” amesema Angela.