Na Mwamvua Mwinyi, Mafia
Desemba 8, 2024
Kiwanja cha ndege wilayani Mafia, mkoani Pwani, kinatarajia kufanyiwa maboresho kwa kujengwa jengo jipya la abiria na kusimikwa taa kwenye njia za kutua na kuruka ndege.
Maboresho haya yanalenga kurahisisha usafiri wa anga, hususan nyakati za usiku, na hivyo kuchochea ongezeko la watalii na wawekezaji katika sekta ya utalii na uwekezaji wilayani humo.
Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Mafia, Roland Mwalyambi, alifafanua mpango huo wakati wa maonyesho ya Tamasha la Utalii la Mafia (Mafia Festival)ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph Kolombo.
“Mafia sasa inaendelea kufunguka, hivyo watalii wanaoingia ni wengi, jukumu letu la msingi lililopo ni kuhakikisha panafikika kwa urahisi” alisema Kanal Kolombo
Kolombo alitoa wito kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kuboresha kiwanja cha ndege kwakuwa hivi sasa safari za ndege haziwezi kufanyika usiku, kwakuwa hakuna taa zinazowezesha ndege kutua usiku.
Alieleza, wananchi wa Mafia wamekuwa wakihitaji maboresho ya usafiri wa anga na majini ya muda mrefu na kuongeza usimikaji wa taa kwenye kiwanja hicho cha ndege utaimarisha usafiri wa uhakika kwa wageni wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, Kanali Kolombo alihimiza maboresho ya bandari na gati ili kuepuka utegemezi wa maji kupwa na kujaa.
“Nimesafiri kwa usafiri wa majini kuja Mafia, na tumekuwa tukifuata ratiba za maji. Hali hii inadidimiza uwekezaji na utalii wetu,” alisema Kolombo.
Kanali Kolombo aliomba wataalamu kutafuta suluhisho la muda mrefu kwa changamoto hizo ili kuimarisha usafiri wa majini.
Kwa mujibu wa Meneja Mwalyambi, bajeti ya mwaka wa fedha inayoendelea inatarajia kutumika kusimika taa na kujenga jengo jipya la abiria kuanzia Januari hadi Juni 2025.
Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, aliwataka wataalamu wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kutembelea Mafia ili kubaini na kutangaza malikale zilizopo.
Hata hivyo alisema Mafia ina fursa za Uwekezaji na vivutio mbalimbali, hivyo anawaomba wawekezaji kuwekeza katika wilaya hiyo yenye fukwe nzuri na fursa ikiwemo kilimo cha nazi, mwani, na uvuvi wa majongoo bahari.
Kwa upande wake, Veronica Kombe, Mhifadhi wa Mambo Kale wa TFS Bagamoyo, alieleza tamasha hilo ni fursa muhimu ya kutangaza vivutio na malikale mbalimbali za Mafia.
Dkt. Asha Mshana, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, alisema kuwa matamasha kama hayo ni nyenzo muhimu ya kukuza utamaduni nchini.
Alihimiza jamii kudumisha utamaduni kwa maslahi ya vizazi vijavyo.
Tamasha la Mafia Festival limeanza disemba 6 na linatarajia kumalizika disemba 8 mwaka huu.