Vyanzo vya ndani vimeeleza kuwa mapigano hayo ya jana Jumapili yamezuka baada ya utulivu ulioonekana Jumamosi jioni katika vijiji vya Luofu, Miriki na Matembe ambako jeshi la Kongo lilishambuliwa kwa mizinga na waasi wa M23 wanaodaiwa kusaidiwa na jeshi la Rwanda.
Milio ya mabomu na silaha nzito yamesababisha hofu kubwa kwa wakaazi walioanza kuhangaika kwa wiki moja sasa.
Wakimbizi ni wengi na misaada hakuna
Baadhi wamekimbilia mji mdogo wa Kitsumbiro ulio umbali wa kilometa 20 kutoka eneo la vita wakibeba mizigo na mifugo yao, kama anavyoshuhudia hapa raia huyu.
“Vita vinapamba moto kwenye mji mdogo wa Kaseghe. Jeshi linaendelea kukabiliana na waasi wa M23. Tatizo ni kwamba wakazi wanaokimbia kutoka Kaseghe na Miobwe wamekuwa wengi sana na hadi sasa hakuna msaada, hakuna dawa na hata maji safi. Imekuwa ni shida kubwa kabisa. Ni mambo magumu tunayoyapitia kwa sasa,” alisema raia mmoja.
Hata hivyo, jeshi la Kongo, kupitia msemaji wake kwenye operesheni hizo, limedai kufanikiwa kuwazuia waasi wa M23 kusonga mbele kwenye vijiji vingine jirani na mji wa Kaseghe ambamo raia wote wamekimbia. Muhindo Simisi ni mbunge mchaguliwa wilayani Lubero anasema.
“Nchi ya Rwanda inaitesa Kongo sababu inalisaidia kundi la M23 na kulipa nguvu zaidi na hivi Rais Kagame anastahili kuchukuliwa mipango na kufikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa, ICC. ili aulizwe kwa nini anaitesa Kongo. Anayefahamu magumu ya wanawake na watoto hata wazee afadhali awape uhuru Wakongo sababu ardhi hii ni yetu,” alisema Muhindo Simisi.
Hadi Jumatatu, mji wa Kaseghe umekuwa chini ya udhibiti wa kundi la M23 huku jeshi la Kongo likirudi nyuma takribani kilomita 10, vimeeleza vyanzo vya kiraia.
Pamoja na kukemea kutoshirikishwa kwao katika mazungumzo ya Angola, viongozi wa makabila mbalimbali mkoani Kivu Kaskazini wameleeza juu ya kile walichotaja kuwa njama ya kuivamia Kongo.
Tshisekedi na Kagame kukutana Angola
Mbele ya vyombo vya habari mwanzoni mwa juma lililopita, Joseph Nkinzo, afisa kutoka kundi linalowajumuisha viongozi hao wa makabila ameeleza hofu yake.
“Kumekuwa na mikataba mingi inayosainiwa kushoto na kuume na tumegundua kwamba inaweza kuliweka taifa la Kongo katika hatari kubwa sana. Ni lazima jambo hili lichukuliwe kwa umakini viongozi wa makabila yakishirikishwa,” alisema Joseph Nkinzo.
Hali hii inajiri wakati ambapo Rais Felix Tshisekedi wa Kongo na Rais Paul Kagame wa Rwanda wanatarajiwa kukutana Desemba 15 nchini Angola kwa ajili ya mazungumzo yanayolenga kumaliza mzozo kati ya mataifa hayo mawili.
Mwandishi: Benjamin Kasembe