Mashishanga awataka viongozi wajifunze aliyotenda Nyerere

Morogoro. Mkuu wa mkoa mstaafu wa Morogoro, Stephen Mashishanga amewataka viongozi wa sasa kujifunza kutoka kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere hasa katika kuhakikisha nchi inakuwa na uhuru kamili na amani itakayofanya uchumi kukua.

Akizungumza katika kongamano la maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika lillilofanyika leo Jumatatu, Desemba 9, 2024 mjini Morogoro, Mashishanga amesimulia jinsi Mwalimu Nyerere alivyohakikisha nchi inapata uhuru kamili bila purukushani za kumwaga damu, bali kwa amani na utulivu.

Mashishanga ambaye pia ni mwanasiasa mkongwe nchini, amesema Nyerere alikuwa mfano bora, alikuwa na uwezo wa kujieleza na kuwashawishi wananchi na kwamba huo ndio ulikuwa msingi ulioiwezesha nchi kupata uhuru kutoka kwa wakoloni.

Katika kudumisha misingi ya amani na mshikamano, Mashishanga amewaasa viongozi wa dini kuendelea kuiombea nchi, ili iendelee kudumisha misingi hiyo kama alivyokuwa akisisitiza Nyerere.

Kwa upande wake, Diwani wa Kiwanja cha Ndege, Majuto Mbuguyu amesema Serikali inapaswa kuimarisha huduma vijijini na kutoa elimu ya kilimo cha kisasa, ili kupunguza wimbi la vijana wanaohamia mijini kutafuta maisha bora.

“Sasa hivi wamachinga wamejaa mijini wakitafuta maisha bora, vijana wanakimbia vijijini kwa sababu ya changamoto za kilimo cha mazoea, Serikali iendelee kutoa elimu ya kilimo cha kisasa,” amesema Mbuguyu.

Akizungumza katika kongamano hilo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala amesema mkoa umeendelea kuimarika kwa kiwango kikubwa katika sekta ya viwanda, kilimo, afya na miundombinu.

“Miaka ya 61 Wilaya ya Morogoro haikuwa na vituo vya afya kama ilivyo leo, kila wilaya sasa ina vituo vya afya vya kisasa, hivi karibuni Manispaa ya Morogoro itapata jengo la mama na mtoto na tayari Sh5 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi huo,” amesema Kilakala.

Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro wameeleza tathimini yao ya miaka 63 ya uhuru, huku baadhi wakisema uhuru wa kweli utapatikana pale Tanzania itakapojitegemea kikamilifu katika sekta muhimu kama chakula, elimu, afya na miundombinu.

Mmoja wa wananchi hao, Malaki Msaki amesema Tanzania ina ardhi kubwa yenye rutuba inayoweza kuzalisha chakula na mazao ya biashara ya kila aina.

Hivyo, amesema Serikali inapaswa kuwekeza zaidi katika kilimo cha kisasa, ili Taifa lijitegemee kwa chakula.

“Natamani sekta ya kilimo isihusishwe na siasa, Tanzania tuna ardhi yenye rutuba, hivyo viongozi waweke mkazo katika kuimarisha sekta hii kwa sababu tukiwa na njaa ni rahisi kutawaliwa, lakini tukijipanga vizuri uhuru wetu utakuwa wa kweli,” amesema Msaki.

Pia amesema kuna haja ya kuboresha bei za pembejeo na masoko kwa wakulima, jambo litakalosaidia kuimarisha maendeleo yaliyopatikana tangu uhuru.

Naye Mariam Khalid ambaye ni mfanyabiashara amesema Serikali inapaswa kuongeza nguvu katika kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.

“Serikali ijipange kuhakikisha fursa za kiuchumi zinawafikia watu wote, tunapoadhimisha uhuru wetu, tunapaswa kufikiria jinsi ya kushirikiana zaidi kama Watanzania, ili kuboresha maisha ya kila mmoja wetu,” amesema Khalid.

Related Posts