Mbeya yaingilia kati Prisons na Ken Gold

WAKATI Tanzania Prisons na Ken Gold zikiendelea kuchechemea kwenye Ligi Kuu, chama cha soka mkoani Mbeya (Mrefa) kimezitaka timu hizo kutekeleza ushauri wa kamati ya mashindano ili kukwepa aibu ya kushuka daraja.

Timu hizo pekee mkoani Mbeya kwenye Ligi Kuu, hazijawa na matokeo mazuri na kuweka presha kwa mashabiki na wadau wa soka katika vita ya kushuka daraja msimu huu.

Mbeya iliyowahi kutesa kwa kuwa na timu nyingi Ligi Kuu, kwa sasa imebakiwa na Prisons na Ken Gold baada ya Mbeya Kwanza na Mbeya City kushuka daraja, huku Ihefu ikipigwa bei.

Hata hivyo hadi sasa timu hizo hazijawa na matokeo mazuri, ambapo Ken Gold inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza ndio inaburuza mkia kwa pointi sita, huku Prisons ikiwa nafasi ya 12 kwa alama 11.

Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya chama hicho, Mohamed Mashango alisema wamekuwa na vikao vya mara kwa mara na timu hizo kujadiliana mustakabali wa kuwa salama.

Alisema moja ya mapendekezo na ushauri ni kujipanga dirisha dogo kuhakikisha wanafanya maboresho ya katika timu zao ili mzunguko wa pili wafanye vizuri na kubaki salama Ligi Kuu msimu ujao.

“Bila hizi timu, hatutaziona Simba wala Yanga, Mrefa tumekuwa na vikao vya mara kwa mara kujadiliana na kupeana ushauri na mapendekezo nini cha kufanya ili kubaki salama Ligi Kuu”

“Matarajio yetu ni kwamba dirisha dogo litaleta mabadiliko chanya na timu zetu zitafanya vizuri mzunguko wa pili na hatimaye kumaliza ligi katika nafasi nzuri”  alisema Mashango.

Katibu Mkuu wa Ken Gold, Benson Mkocha alisema hawafurahishwi na matokeo waliyonayo, akiahidi kuwa dirisha dogo itakuwa na mafanikio kwao katika kubaki salama Ligi Kuu.

“Tumekubali mzunguko wa kwanza matokeo yaliyotokea, tumejifunza kitu, naamini tutafanya usajili imara dirisha dogo na kurejea kwa ubora raundi ya pili ili kutoshuka daraja.” alisema Mkocha.

Related Posts