Mfahamu aliyeongoza mapinduzi ya Rais Assad wa Syria

Dar es Salaam. Baada ya utawala wa familia ya aliyekuwa Rais wa Syria, Bashar al-Assad uliodumu kwa zaidi ya miaka 53 kuangushwa, yupo mtu aliyekuwa nyuma ya pazia kufanikisha operesheni hiyo.

Mtu huyo ambaye ni kiongozi wa kijeshi anajulikana kama Abu Mohammed Al-Jolani, ndiye aliyeongoza operesheni ya kumng’oa Rais Assad ambaye kwa upande wake ametawala nchi hiyo kwa miaka 24.

Jina halisi anaitwa Ahmad al-Sharaa, katika operesheni aliyofanyika hivi karibuni alifanikisha kuuteka mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Aleppo ndani ya siku tatu, kisha safari kuelekea Damascus.

Al Jolani ni kiongozi wa kundi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS), kundi ambalo limekuwa na nguvu kubwa zaidi ya upinzani hasa wa silaha nchini Syria.

Kwa miaka mingi, Jolani amekuwa akifanya kazi ya kuunganisha na kuimarisha nguvu ya kundi, alipokuwa katika jimbo la Idlib lililopo kona ya kaskazini magharibi mwa Syria wakati utawala wa Assad uliokuwa ukiungwa mkono na Iran na Russia ukiwa imara hadi pale operesheni ilipoanza.

Kwa mujibu wa Al Jazeera, Al Jolani alizaliwa mwaka 1982 (kwa sasa ana miaka 42) huku katika maisha yake aliwahi kukaa huko Riyadh, Saudi Arabia wakati baba yake akifanya kazi kama mhandisi sekta ya mafuta.

Baada ya maisha ya Riyadh, familia yao ilirejea Syria mwaka 1989 na walienda kukaa karibu na Damascus.

Mwaka 2003 alihamia nchini Iraq ambapo alijiunga na kundi la al-Qaeda, ikiwa kama sehemu ya upinzani dhidi ya uvamizi wa Marekani mwaka huohuo.

Alikamatwa na vikosi vya Marekani nchini Iraq mwaka 2006 na kuzuiliwa kwa miaka mitano,  Jolani alipewa jukumu la kuanzisha tawi la al-Qaeda nchini Syria la Nusra Front, ambalo lilikua na ushawishi wake katika maeneo yanayoshikiliwa na upinzani, hasa Idlib.

Katika miaka iliyofuata, Jolani alionekana kujitenga na harakati za al-Qaeda za kuanzisha ukhalifa katika nchi zote zenye Waislamu wengi, akiweka mkazo juu ya kujenga kundi lake ndani ya mipaka ya Syria.

Amesema madhumuni yake ni kukomboa Syria kutoka kwa serikali ya kimabavu ya Assad, kuondoa wanamgambo wa Iran na kuanzisha Serikali kulingana na tafsiri ya sheria ya Kiislamu.

Saa chache baada ya kufanikisha operesheni ya kukamata Damascus, al-Jolani amejitokeza kwa mara ya kwanza katika msikiti maarufu wa Umayyad, akitangaza kuanguka kwa Assad kuwa “ushindi kwa taifa la Kiislamu.”

“Pia alisema Syria inastahili mfumo wa utawala ambao ni wa kitaasisi, si wa mtawala mmoja kufanya maamuzi ya kiholela,” alisema katika mahojiano na CNN.

Kwa sasa Jolani anatajwa kuwa ndiye kiongozi mpya wa Syria, baada ya aliyekuwa Rais Assad kukimbia, huku akiacha maagizo ya kukabidhiana madaraka kwa amani kwa waliobakia nchini humo.

Related Posts