Dar es Salaam. Safari ya mwisho ya aliyekuwa Mfamasia wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke (TRRH) Magdalena Kaduma imehitimishwa jijini hapa, huku uongozi wa hospitali hiyo ukisema umepoteza mtu aliyekuwa chanzo cha watumishi wengine kubadilika katika kuwahudumia wagonjwa.
Magdalena (36) ameagwa nyumbani kwa wazazi wake, Tabata-Sanene, Dar es Salaam leo Jumatatu, Desemba 9, 2024 na mwili wake kusafirishwa kwenda Makambako, Mkoa wa Njombe kwa ajili ya mazishi.
Kifo cha mfamasia huyo kimeacha maswali juu ya nani aliyehusika. Hii ni baada ya Desemba 4, 2024, familia yake kupokea taarifa za kupotea kwa binti yao kupitia simu ya mumewe, Kenan Mwandalima aliyempigia mama yake Sofia Kaduma.
Jitihada za kumtafuta zilifanyika na siku mbili baadaye Desemba 6, 2024 mwili wake ulipatikana nyuma ya nyumba yao Kibamba, jijini Dar es Salaam walipokuwa wakiishia na mumewe ukiwa umefukiwa kwenye shimo.
Polisi bado haijatoa taarifa juu ya tukio hilo, huku ndugu wa marehemu wakieleza waliripoti tukio hilo kituo cha Polisi Gogoni na mumewe, Mwandalima anashikiliwa na jeshi hilo kwa uchunguzi zaidi.
Mara baada ya ibada nyumbani hapo, Mganga Mfawidhi wa TRRH, Dk Joseph Kimaro akitoa salamu za rambirambi amesema wamepotelewa na mtumishi ambaye alijitoa kwa ajili ya wengine, kwani alikuwa akisimamia maadili.
“Kama tulivyosikia hapa wamesema alikuwa mtumishi kanisani, lakini kwetu sisi alikuwa na cheo chake pia, licha ya kuwa mfamasia lakini alikuwa katibu wa kamati ya maadili katika hospitali yetu,” amesema Dk Kimaro.
Amesema watumishi wa Hospitali ya Temeke wamekuwa na maadili kwa sababu ya utendaji kazi wa marehemu Magdalena, kwa sababu alikuwa anaifanya kazi yake ipasavyo na kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.
Naye Ignas Kaduma, baba mzazi marehemu amesema walishukuru kupatikana kwa mwili wa binti yao.
“Hayo mengine Mungu ndiye anayejua lakini sisi kwetu tunamshukuru sana Mungu kwa kuupata mwili wa binti yetu, tumekuwa na amani tofauti na tusingemuona kabisa,” amesema Kaduma.
Awali, Mchungaji wa Kanisa la Efatha, Emmanuel Chao ametoa wito kwa watu kuacha kuhukumu kwa kutoa uhai wa binadamu wengine, kabla ya kutenda jambo hilo inatakiwa kutafakari.
Amesema inabidi kila mtu aangalie mienendo yake anayokwenda nayo maana hakuna anayejua anayekaa naye karibu anawaza nini juu ya mwenziye, hivyo kuna haja ya kumkabidhi Mungu kila anachokifanya.
“Unapomdhuru mtu si kwamba unafanya kwa ajili ya uliyemfanyia bali kwa mtu aliyemleta duniani hata kumuondoa mtu katika nafasi yake unamuumiza aliyemuweka katika nafasi hiyo, kila tunachofanya tukitafakari kwanza,” amesema Chao.
Pia, amesema wapo wanaosema wameokoka lakini wanachokifanya hakihusiani na wokovu anaoutangaza kwa watu, hivyo si kumuamini mtu kwa sababu ya kitu anachokihubiri, anayeweza kufanya hivyo ni Mungu pekee aliyemuumba.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari na Wafamasia Wilaya ya Temeke, Francis Benedict amesema wamepoteza mwanachama aliyekuwa anajitoa katika shughuli mbalimbali ikiwamo matukio ya misiba.
“Kwetu ni pigo kwa sababu ni kifo cha ghafla na cha kusikitisha,” amesema Benedict.
Awali, waombolezaji wamehoji muhusika wa mauaji hayo ni nani. “Wazazi siku zote wanaona ni heri mtoto augue na kufa kuliko kuuliwa na mtu halafu hawajui aliyefanya hivyo ni nani, inaumiza zaidi kwani muda wote watawaza alimkosea nini muuaji hadi akaamua kukatisha uhai wa mtoto wao,” amesema Judith Kalenga.
Mfanyakazi mwenzaye ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini amesema tangu amfahamu Magdalema mwaka 2017 hajawahi kumuona kwenye ugomvi, alikuwa akifanya kazi zake na kuondoka.
“Tangu nimfahamu Mage sijamuona akiwa na makundi, sema amekuwa msiri mno kwenye mambo yake, maana baada ya kuolewa tuliona mabadiliko ambayo hatukumuelewa, alianza kupauka na alikuwa na gari lakini akawa anakuja kazini na daladala,” amesema.
Amesema kwa kuwa hakuwa anasema kwa watu changamoto zake, hivyo ilikuwa ngumu kumuuliza kwani alikuwa anacheka na kufurahi na wafanyakazi wake akiwa msimamizi wa kitengo cha dawa hospitalini.
Magdalena alizaliwa Januari 30, 1988 na alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chang’ombe, Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1995 hadi 2002.
Mwaka 2003 hadi 2007, alisoma sekondari ya wasichana St. Francis, Mbeya. Baadaye alijiunga na Shule ya Wasichana Marian, mkoani Pwani.
Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, alijiunga na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) mwaka 2007, na alihitimu mwaka 2011. Alianza kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili mwaka 2011 hadi 2012, kabla ya kujiunga na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke mwaka 2013 kama mfamasia hadi alipofariki.
Marehemu Magdalena alifunga ndoa na Kenan Mwandalima katika Kanisa la Efatha Novemba 17, 2018.