Miaka 63 ya uhuru katikati ya utekaji, raia kupotea, kuuawa

Tanganyika imepata uhuru kamili. Mtoto mwema wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere na wenzake wamewezesha nchi kuwa huru. Ni Desemba 9, 1961. Leo, Desemba 9, 2024, imetimia miaka 63 tangu tukio hilo.

“Heri kushinda njaa kwenye uhuru, kuliko chakula cha kusaza utumwani.” Nyimbo ziliimbwa. Maneno ya tambo za kila aina, yaliwatoka Watanganyika. Yote ilikuwa furaha na fahari ya uhuru.

Miaka 63 baadaye, Tangangyika inaadhimisha uhuru wake kukiwa na matukio makubwa ya utekaji, wananchi kuuawa na wengine wanapotea. Haijulikani wanapotelea wapi. Wanajipoteza au wanapotezwa? Watapatikana hai au wafu? Au hawatapatikana moja kwa moja?

Uhuru wa Tanganyika unaadhimishwa siku nne baada ya tukio la maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kushambuliwa na wananchi, Tegeta, Dar es Salaam. Kisha, mmoja, Aman Simbayao kufariki dunia akiwa anatibiwa, Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam.

Sababu ya maofisa wa TRA kushambuliwa, bila shaka ni hofu ambayo ipo ndani ya wananchi. Vilevile, imani yao kuwa ndogo juu ya vyombo vya usalama pamoja na magari ya Serikali au ya taasisi za umma. Kikubwa, matukio ya utekaji yamekosa ufumbuzi. Jeshi la Polisi Tanzania haliwapi wananchi matumaini.

Desemba mosi, 2024, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana, chama cha ACT-Wazalendo, Abdul Nondo, alitekwa na watu wasiojulikana, wakatumia gari aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop nyeupe, kuondoka naye kutoka eneo la tukio Mbezi, Dar es Salaam.

Nondo, alipanda basi Novemba 30, 2024, mkoani Kigoma, alifika Dar es Salaam katika kituo cha mabasi cha Magufuli, Mbezi, Desemba mosi, 2024, saa 10 alfajiri. Kwa kilichoonekana alikuwa akifuatiliwa hatua kwa hatua, alipokuwa anatoka kwenye geti la kituo hicho, alijikuta anavamiwa na watu sita. Akaingizwa kwenye gari, wakaondoka naye.

Viongozi wa ACT-Wazalendo walitoa taarifa kwa umma iliyodai kuwa gari aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop nyeupe, lenye namba za usajili T249 CMV, lililoonwa na mashuhuda likiondoka na Nondo, lilikutwa kituo cha polisi Gogoni, likiwa linabadilishwa namba za usajili.

Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, ilijibu madai hayo kuwa gari Toyota Land Cruiser Hardtop, lililokutwa kituo cha polisi Gogoni, silo lililotumika kumchukua Nondo kituo cha mabasi cha Magufuli.

Ni jambo la kumshukuru Mungu Nondo alipatikana akiwa hai, japo aliumizwa vibaya na mwili wake ulikutwa na sumu nyingi. Waliomteka ni simulizi ya “watu wasiojulikana”. Hofu ni kubwa. Katikati ya mazingira hayo, maofisa wa TRA wakawa wanalifuatilia gari lililoingizwa nchini kinyemela na kusajiliwa kimagumashi.

Aliyekuwa akifuatiliwa alipiga mayowe kuwa wenye Land Cruiser Hardtop nyeupe walitaka kumteka. Wananchi waliposikia kuwa eneo lao, Tegeta, Dar es Salaam, kulikuwa na watekaj, halafu gari walilotumia linafanana kama lile lililotumika kumteka Nondo, haraka walijichukulia sheria mkononi kuwashambulia maofisa wa TRA, wakasababisha kifo cha Simbayao, gari wakalivunja vioo na kuliacha nyang’anyang’a.

Miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika, inaadhimishwa kipindi ambacho polisi, jeshi la kulinda usalama wa umma, linatuhumiwa kuhusika na vitendo vya utekaji. Watu ambao huvaa nguo za kawaida, inadaiwa hujitambulisha ni maofisa wa polisi, wanapokuwa kwenye harakati zao za utekaji.

Karne ya 19, mhalifu Eugene Francois Vidocq, raia wa Ufaransa, alibadilika na kutumia mbinu zake za ujahili kuisaidia Serikali ya Ufaransa, dunia ilipokea, kuendeleza na kuupanua mfumo wa vyombo vya usalama kuwa na mashushushu, ili kurahisisha kunasa wahalifu na mitandao yao.

Mwaka 1811, Vidocq alianzisha mtandao wake wa mashushushu, ukiitwa Surete Nationale, yaani Usalama wa Taifa. Mtandao huo ulifanya kazi za kuzisaidia mamlaka za nchi kuwanasa wahalifu na makundi yao. Surete Nationale kwa sasa ni jeshi rasmi la polisi, likiitwa National Police.

Muongo wa tatu wa karne ya 19, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Robert Peel, kipindi akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, alianzisha mtindo wa kutumia mashushushu kwenye jeshi la polisi la nchi hiyo, The Metropolitan ‘The Met’, kisha Marekani ilifuata mwanzoni mwa Karne ya 20, polisi New York walipoanzisha idara waliyoiita Kikosi cha Kiitaliano (Italian Squad).

Kila nchi kuna mashushushu, wapo wenye kufanya kazi ndani au nje ya nchi. Wapo mashushushu wa idara za itelijensia, vilevile polisi wanaotumika kwa kazi maalumu. Umuhimu wake ni mkubwa katika kulinda na kuzuia uhalifu wa aina mbalimbali kwa nchi na wananchi.

Shushushu wa polisi kwa Kiingereza anaitwa undercover police. Katika Kiswahili tuna msamiati mwingine; askari kanzu, kwa maana ya askari asiyevaa sare rasmi za jeshi lake. Askari kanzu lina upana mkubwa, linamtafsiri kila askari asiyevaa sare. Ndani ya jeshi la polisi, askari wa aina hiyo wanatumika zaidi kitengo cha itelijensia.

Bahati mbaya, Tanzania, askari wasio na sare, ndiyo hasa wamekuwa wakituhumiwa kuhusika na vitendo vya utekaji. Madhara yake ndiyo hayo ambayo yamejionyesha. Maofisa wa TRA kushambuliwa, na mmoja kupoteza maisha.

Aprili 2017, mwanamuziki wa Hip Hop nchini, Ibrahim Mshana ‘Roma Mkatoliki’, akiwa na wenzake watatu, walitekwa na watu wasiojulikana na kuwashikilia kwa takriban siku tatu. Akina Roma walikuwa studio ya muziki ya Tongwe Records, Masaki, walipovamiwa na watekaji.

Kwa mujibu wa maelezo ya Roma na wenzake, watekaji walikuwa na bunduki pamoja na pingu. Walivyochukuliwa walidhani ni polisi, lakini ikawa kinyume chake. Waliwapiga, kuwavunja meno na kuwaachia majeraha na alama mbalimbali zenye kuonyesha kwamba walipewa msoto mkali.

Jinsi mwandishi wa habari wa kujitegemea, aliyekuwa akiripoti gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda, alivyopotea Novemba 2017, hisia za karibu zaidi ni kwamba alitekwa. Kuna watu waliokuwa wamevalia kiraia walikuwa naye, wakaongozana mpaka kwa mkewe shambani kufuata ufunguo wa nyumba yao, baada ya hapo hakuonekana tena.

Dhana ya awali ingekwambia watu walioongozana na Azory ni polisi waliokuwa katika mavazi ya kawaida. Hata hivyo, baada ya Azory kupotea jumla, jawabu ambalo lina nguvu zaidi ni kuwa wale watu hawakuwa polisi, isipokuwa ni watekaji. Mtanzania aliyefuatilia tukio la Azory anawaza jinsi ya kujilinda dhidi ya watu wenye kuvaa kiraia wenye kujiita polisi.

Ben Saanane, kada wa Chadema aliyekuwa msaidizi binafsi wa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alitoweka tangu Novemba 2016. Taarifa za simu yake zinaonyesha mara ya mwisho alikuwa Mburahati, Dar es Salaam, kisha alikwenda au alipelekwa Mikocheni ambako simu yake ilizimwa.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Kigoma, Simon Kanguye, inaelezwa alifuatwa nyumbani kwake. Hisia za mwanzoni kwa wanafamilia au pengine Kanguye mwenyewe, ni kwamba waliomfuata ni maofisa wa polisi ambao hawakuvaa sare au mashushushu wa vyombo vingine vya Serikali.

Baada ya kitambo kirefu kupita na Kanguye kutafutwa vituo vyote vya polisi bila mafanikio, jawabu la karibu ni kuwa wale waliomchukua ni watekaji. Hapohapo ongeza kwamba mitaani kuna watu hujifanya maofisa wa polisi na wengine Usalama wa Taifa. Hujivika wasifu bandia ili kufanya utapeli.

Jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola, havishughulikii utekaji kwa ukweli, uwazi na kwa kushirikisha wananchi. Hiyo ndiyo sababu imani ya wananchi imekuwa ndogo. Ni sababu ya maofisa TRA kushambuliwa.

Utekaji unaoendelea nchini ni nafuu kwa wahalifu. Wakifuatwa kukamatwa, watapiga mayowe kuwa wanatekwa. Wananchi wakichukua sheria mkononi lawama kwa nani? Deusdedith Soka, Jacob Mlay, Frank Mbise, kutaja wachache, walitoweka tangu Agosti 2024. Jitihada za kuwafikia watekaji hazitoi matumaini.

Septemba 2024, mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema, Ali Kibao, alitekwa na watu waliojitambulisha ni polisi ndani ya basi lenye abiria. Halafu akakutwa ameuawa Ununio, Dar es Salaam. Hata mmoja hajakamatwa kuhusiana na kifo cha Kibao.

Kisha, polisi wakatumia nguvu kubwa kudhibiti maandamano yaliyolenga kushinikiza wauaji wa Kibao watafutwe, tunategemea nini siku mhalifu akiwa anakaribia kukamatwa na maofisa wasio na sare, akipaza sauti kuwa anatekwa?

Wito tukiadhimisha miaka 63 ya uhuru ni kuwa lazima kutazama wapi kama nchi tumejikwaa. Siyo kunung’unikia tulipoangukia. Namna ya ushughulikiaji matukio ya utekaji, imefikisha nchi mahali hapa. Wasiwasi ni mkubwa kwa wananchi. Imani kwa vyombo vya dola ni haba.

Related Posts