Mzigo wa mawaziri watano huu hapa

Dar es Salaam. Mzigo mzito wa majukumu ya kiserikali na ya kuwahudumia Watanzania unawasubiri mawaziri watano na wateule wengine wa Rais Samia Suluhu Hassan wanaoapishwa leo kuanza kazi rasmi, baada ya kuteuliwa juzi.

Waziri mpya wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ni miongoni mwa mawaziri wanaotajwa kukabiliwa na mizigo hiyo, hasa kutokana na wizara yake kubeba taasisi zinazolalamikiwa zaidi na Watanzania.

Ingawa si mgeni katika kusimamia wizara zenye vyombo vya ulinzi na usalama, aliwahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, lakini nafasi aliyopelekwa sasa kunatajwa si lelemama na ni moja ya wizara zinazonyooshewa kidole na raia.

Mzigo huo wa majukumu kwa mawaziri hao, unakuja siku moja baada ya mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia katika baraza la mawaziri akiwahamisha kadhaa kutoka eneo moja kwenda lingine akiwemo Bashungwa.

Katika mabadiliko hayo, Bashungwa aliyekuwa Wizara ya Ujenzi, amehamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi huku Abdallah Ulega aliyekuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, akiteuliwa kumrithi Bashungwa.

Profesa Palamagamba Kabudi aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, huku mikoba yake katika Wizara ya Katiba na Sheria, ikirithiwa na Dk Damas Ndumbaro.

Lakini wengine walioteuliwa ni Gerson Msigwa anayeendelea kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo pia akiongezewa na jukumu la kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali.

Aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba ameteuliwa kuwa Balozi, pamoja na Mobhare Matinyi na Kamishna wa Rasilimali Watu na Utawala wa Jeshi la Polisi nchini, Suzan Kaganda.

Matukio ya utekaji, ukamataji raia usiofuata sheria, matumizi ya nguvu kupitiliza dhidi ya wananchi na vitisho ni miongoni mwa malalamiko yanayoiangukia Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, ambayo Bashungwa ataihudumu.

Vitendo hivyo, vinadaiwa kufanywa na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi, huku likihusishwa na madai ya kutumiwa kukandamiza haki za kiraia za wananchi.

Agosti mwaka huu, Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), kiliripoti matukio zaidi ya 80 ya watu kutekwa na kutoweka, huku Jeshi la Polisi likitupiwa lawama, ama ya kuhusika au kushindwa kutimiza wajibu wake kudhibiti matukio hayo.

Kama hiyo haitoshi, wizara hiyo pia inaingia midomoni mwa watu kwa kile kinachoelezwa, imeshindwa kuratibu vema mchakato wa upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa kupitia Mamlaka ya Taifa ya Vitambulisho (Nida).

Hayo ni machache kati ya mengi yanayomsubiri Bashungwa, kuanzia leo, anapoapishwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, akimrithi Masauni.

Wingi wa malalamiko na hofu za wananchi dhidi ya taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo, ni moja ya jukumu linalomkabili Bashungwa katika wadhifa wake mpya, kama inavyofafanuliwa na Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi mstaafu, Jamal Rwambow.

Katika awamu mbalimbali za Serikali, kumekuwa na malalamiko dhidi ya matumizi ya nguvu kupitiliza, matukio ya utekaji, kupotea kwa watu, mauaji ya raia na ukamataji usiofuata sheria, yote yakihusishwa na Jeshi la Polisi.

Kwa mujibu wa Rwambow, waziri mpya anapaswa kusikiliza malalamiko hayo ya wananchi na kutafuta mbinu ya kukabili vitendo vyote visivyostahili ndani ya jeshi hilo.

Kusikiliza na kuchukua hatua juu ya malalamiko ya watu, alisema ndilo jambo muhimu linalopaswa kuzingatiwa na Bashungwa katika utendaji wake.

“Wawe wanasiasa au wananchi wa kawaida wasikilizwe kwa sababu hao ndiyo wanaokumbana na madhila ya uongozi,”amesema Rwambow aliyewahi kuhudumu kama Kamanda wa Polisi katika mikoa ya Manyara na Mwanza.

“Watu wakisema wasionekane ni wachochezi au wana majungu, wasikilizwe na panapohitajika hatua waziri au amshauri mwenye mamlaka afanye hivyo,” amesema.

Katika hatua hizo za kusikiliza amesema ni muhimu waziri atenge muda kwa ajili ya kuwasikiliza wastaafu wa nafasi aliyonayo sasa au polisi akisema ni muhimu kwa sababu hawana cha kupoteza, hivyo hawataogopa kumweleza ukweli.

“Awe na utaratibu wa kukutana na wastaafu ili kupata mrejesho wa utendaji kila baada ya muda fulani,”ameeleza.

Amesema kibarua kingine kinachomkabili ni kutafuta namna ya kuwadhibiti wanasiasa wasiotimiza wajibu wao, badala yake wanataka kutumia polisi kuonyesha nguvu walizonazo.

Ulega anaukwaa uwaziri wa ujenzi katikati kitendawili cha huduma za vivuko Magogoni-Kivukoni.

Katika eneo hilo linalovusha watu zaidi ya 60,000 kwa siku, kimebaki kivuko kimoja pekee cha MV Kazi, huku vingine viwili vikiwa kwenye matengenezo makubwa.

Suala hilo linageuka kuwa changamoto hasa ukizingatia, kivuko kama MV Magogoni kilishapita muda uliopangwa kikamilike kufanyiwa matengenezo hayo, lakini hadi sasa hakijakamilika.

Mei mwaka huu, Mwananchi iliandika ripoti maalumu iliyoonyesha kinachokwamisha matengenezo hayo na sababu ni kukosekana fedha ya kumlipa mkandarasi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kivuko cha MV Magogoni kilipaswa kulipiwa tangu mwaka 2023, lakini malipo ya awali ambayo ni asilimia 10 ya malipo ya jumla yamefanywa Machi mwaka huu.

Kibarua kingine kinachomkabili Ulega ni ukamilishaji wa miradi ya miundombinu zikiwemo barabara katika mikoa mbalimbali, ambazo kwa sasa zimekuwa zikilalamikiwa.

Malipo ya makandarasi wanayoidai Serikali baada ya kukamilisha miradi mbalimbali ni mzigo mwingine unaomkabili Ulega anapopokea kijiti kutoka kwa Bashungwa katika wizara hiyo.

Mtaalamu wa masuala ya Ujenzi, Joseph Rwihula alisema ili kuleta ufanisi tarajiwa, Waziri mpya anapaswa kuzungumza na wakuu wa taasisi chini yake.

Sambamba na hilo, alimshauri asiwe mtu wa kupenda ofisi kwa kuwa wizara hiyo inahitaji mtendaji anayekwenda kwenye maeneo ya miradi.

“Akiwa mtu wa ofisini, atakuwa amekubali kudanganywa, kwa sababu hii wizara ina mambo mengi ya kitaalamu ni vema ushuhudie usisubiri kusimuliwa,” amesema.

Kadhalika, alimtaka kuhakikisha anaheshimu na kutoa nafasi kwa taaluma badala ya kuingilia kisiasa.

Profesa Kabudi ni waziri mwingine anayekabiliwa na kibarua kigumu mbele yake, hasa kutokana na imani duni ya wanataaluma wengi wa habari juu ya mabadiliko yaliyofanyika.

Mabadiliko hayo yanaiondoa sekta ya habari kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na imerudishwa katika Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo.

Awali, wadau walilalamika hatua ya sekta ya habari kufungamanishwa na sanaa na utamaduni na kusababisha  isitiliwe maanani.

Kibarua kinachomsubiri Profesa Kabudi ni kuhakikisha anafufua matumaini ya wadau wa habari kwa kuhakikisha anatenda sawa kwa sekta zote, ndani ya wizara anayoapa leo kuiongoza.

Akizungumzia hilo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari (Jowuta), Suleiman Msuya amesema pamoja na kumpongeza kwa kuteuliwa katika wadhifa wake huo, lakini kuna mambo ana mashaka hasa umri wa Profesa Kabudi unapingana na sekta atakazoziongoza ambazo aghalabu zinahitaji damu changa.

“Kwa ukongwe wake na taaluma zake za habari na sheria anastahili, lakini umri unamkataa. Simuoni kama ataendana na mchakamchaka wa sekta husika,” amesema.

Hata hivyo, amesema kinachomsubiri kiongozi huyo ni usimamizi wa sheria ya masilahi ya wanahabari mahala pa kazi.

“Wanahabari hadi sasa hawana uhakika kuhusu masilahi yao na mikataba, tunatarajia Profesa Kabudi kwa kuwa ni mwanahabari na Mwanasheria atayasimamia haya,” amesema.

Kwa upande wa Dk Ndumbaro, kwanza ameteuliwa kuiongoza sekta aliyobobea kwayo, kwani naye ni mwanasheria lakini pili ameteuliwa katika eneo alilowahi kuhudumu, hivyo si mgeni katika wizara hiyo.

Licha ya ubobevu na uzoefu, ufanisi katika utendaji ndani ya wizara hiyo si lelemama, kwani kuna mengi yanayotarajiwa na wananchi kutoka kwake.

Miongoni mwa matarajio hayo ni kuratibiwa kwa mabadiliko ya sheria mbalimbali zinazolalamikiwa, zikiwemo za uchaguzi, lakini kubwa zaidi ni Katiba ambayo imekuwa kilio cha baadhi ya wananchi na wadau wa siasa.

Lingine ni usimamizi wa taasisi zilizo chini yake, kuhakikisha zinatenda haki hasa zile za mifumo ya haki jinai.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe amesema mabadiliko ya sheria hasa zinazolalamikiwa ndilo jambo linalopaswa kusimamiwa na mteule huyo mpya.

Amesema katika utekelezaji wa jukumu hilo, anapaswa kushirikisha watendaji wenzake na sekta nyingine stahiki kuhakikisha kila kinachotarajiwa kinakamilishwa.

Kwa mujibu wa Dk Kabobe, kwa kuwa tayari kuna mwongozo wa mapendekezo ya tume na kamati mbalimbali ikiwemo Tume ya Haki Jinai, jukumu la Dk Ndumbaro ni kurejea na kusimamia utekelezaji.

“Inahitaji umakini na kufuata njia stahiki kufanikisha kila kinachopangwa kwa masilahi ya Taifa, ili kushinikiza mabadiliko ya sheria atalazimika kwenda na mwenendo huo,” amesema.

Lakini, kwa kuwa Dk Ndumbaro kitaaluma ni Mwanasheria, mwanazuoni huyo alisema haitakuwa vigumu kwake kujua njia za kupita kufanikisha mabadiliko ya sheria kama ilivyopendekezwa na tume mbalimbali.

Related Posts