Othman: Vijana tambueni mambo mnayopigania

Unguja. Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud amewataka vijana wa chama hicho kutambua mambo wanayopambania na kuyasimamia bila kusahau kurejesha mamlaka kamili mikononi mwa Wazanzibari.

Othman ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Desemba 9, 2024 wakati akifungua kongamano la vijana Mkoa wa Kati Unguja.

“Mnarithi kijiti cha kuipambania nchi na kuendeleza hilo, ni wajibu na haki yetu kwani wenzetu wamepambana tangu huko nyuma na kufika hapa tulipo, kwa hiyo ni wajibu wenu kuhakikisha kijiti hiki mnakirithi,” amesema Othuman.

Amesema licha ya kuwa kwenye Muungano, Zanzibar imekosa fursa mbalimbali kwa sababu ya kutokuwa na mamlaka kamili, huku akitolea mfano wa nchi ya Uswis ambayo ina muungano wa muda mrefu wa nchi 26, lakini kila nchi inanufaika na fursa zake inazozipata.

“Uswis ndio nchi yenye muungano wa muda mrefu duniani na ina muungano wa nchi 26, lakini huwezi kusikia kuna malalamiko miongoni mwa nchi hizo ni kwa sababu kila nchi ilipewa mamlaka yake kamili,” amesema mwenyekiti huyo.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, amesema elimu, afya, miundombinu ndio vinatumia fedha nyingi, lakini havipo kwenye muungano.

Hivyo, amesema Zanzibar inaelemewa na mzigo mkubwa, licha ya mambo ya forodha kuwa kwenye muungano.

Amesema falsafa ya chama hicho kinaamini katika kuendesha nchi kwa kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji badala ya kuahidi kutoa ajira kwa vijana.

“Vijana wakumbuke kila wakati wajiulize wanasimamia kitu gani na kitu gani wanachopambania, kama kuna mtu anapambania ajira bado hajatoa ushirikiano na kujua mwelekeo wa chama hiki, vijana kaeni mtafakari, tunaposema haya wenzetu hawayaoni,” amesema Othman.

Ameongeza kuwa: “Ukiwa na mamlaka katika mfumo ndio unaweza kukuza uchumi, mwekezaji akija anaangalia uwezo wa nchi.”

Kuhusu ajira, amesema kazi ya Serikali ni kutengeneza mazingira bora na kuweka mifumo ya uwekezaji na sio kutangaza kutoa ajira kwa vijana.

Kutokana na hilo, amesema chama hicho kinaamini katika kuweka utulivu na kukuza amani ambapo vitawavutia wawekezaji wengi na kuzalisha ajira za kutosha.

“Mwekezaji anakwenda kuwekeza eneo lenye amani, ambapo kuna utulivu wa kodi kwa sababu hakuna mtu anaweza kuwekeza eneo ambalo anaona mtaji wake utakumbana na kashikashi, na sisi hilo ndio tunalotengeneza ACT,” amesema Othman.

Awali, Mwenyekiti wa vijana Mkoa wa Kati, Suleiman Muhammed amesema watahakikisha wanapambana kurejesha mamlaka kamili na kuchukua kiti cha Zanzibar katika Umoja wa Mataifa.

“Niliwahi kumuuliza mheshimiwa Ismail Jussa (Makamu mwenyekiti ACT Wazalendo Zanzibar) kuwa hivi tukirejesha mamlaka yetu na kiti chetu UN kile namba 112 UN kitaendelea kuwa kilekile au tunapaswa kupewa kingine, akanijibu kuwa ni kilekile. Kwa hiyo wajibu wetu sisi tuna jambo moja tu kuvuta mamlaka kamili ya Zanzibar,” amesema.

Related Posts