Dar es Salaam. “Ni siku ya furaha kwangu,” ni kauli ya Hadija Shaban mama wa pacha wawili walioungana baada ya kurejea nchini kutoka Saudi Arabia akiwa na watoto wake waliopata tiba ya kutenganishwa.
Watoto hao Hussein na Hassan walipelekwa Saudi Arabia, Agosti mwaka jana na kufanyiwa upasuaji Oktoba, 2023 wa kutenganisha maeneo ya tumbo, kibofu, nyonga, utumbo mkubwa, mishipa ya damu na fahamu maeneo ambayo viliungana.
Pacha kama hao walioungana Anishia na Melanese, waliwahi kusafirishwa Julai 8, 2018 kwenda Saudi Arabia na kufanikiwa kutenganishwa na jopo la wataalamu 32 waliofanya tiba hiyo kwa saa 13.
Matibabu ya kuwatenganisha Hussein na Hassan yalifadhiliwa na Serikali ya Saudi Arabia, ambayo iliahidi kufanya hivyo mwaka jana kwa watoto hao wenyeji wa Mkoa wa Tabora.
Kwa mara ya kwanza watoto hao walifikishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) wakiwa na siku 12 wakiugua maambukizi na tatizo la lishe, hivyo kusababisha kuwekwa chini ya uangalizi kwa matibabu ya kibobezi ya kuwatenganisha.
Baada ya kuwasili leo Jumatatu Desemba 9, 2024 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Hadija amesema ni furaha kwake kuwaona wapendwa wake wakiwa hai, akiishukuru Serikali kwa msaada wa kurejesha tumaini la kuwapakata watoto wake.
“Nina furaha watoto wangu wamerudi nchini wakiwa wametenganishwa na wana afya nzuri,” ni kauli ya Hadija mama wa pacha hao.
Akizungumzia matibabu ya watoto hao, Daktari Bingwa wa upasuaji wa watoto Muhimbili, Zaitun Bokhary amesema upasuaji wa kuwatenganisha watoto hao ulifanyika kwa saa 16 mapema Oktoba mwaka jana.
“Upasuaji huo uliwahusisha wataalamu wa mifupa, moyo, kibofu cha mkojo na mishipa ya damu, kibofu cha watoto hawa kiliungana, walikuwa na miguu mitatu ila mmoja haukuwa unafanya kazi, hivyo umetumika kutengeneza maeneo mengine,” amesema.
Dk Zaitun amesema watoto hao wamekaa nchini humo kwa mwaka mmoja na miezi minane na matibabu waliyapata katika Hospitali ya King Abdullah bin Abdulaziz ya nchini Saudi Arabia.
Mtaalamu huyo amesema sababu ya watoto kuzaliwa wameungana bado haifahamiki, lakini hutokea kwa wanawake wenye asili ya kuzaa pacha pekee kulingana na tafiti.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi wa Hospitali ya Muhimbili, Dk Rachel Mhavile amesema upasuaji wa kutenganisha pacha hao, ni wa awamu ya kwanza ya matibabu na baada ya muda watarejeshwa nchini humo kuendelea na matibabu.
“Tutawapa sehemu ya kuishi hapa hospitali na baadaye watakwenda kuendelea na matibabu, tunafanya hivi ili wawe chini ya uangalizi wa wataalamu, baada ya mwaka watakwenda kutengenezwa miguu kila mmoja kwa sababu sasa wana mguu mmojammoja,” amesema.
Mtaalamu huyo amewaomba Watanzania kumsaidia mama huyo makazi ya kuishi ili kuwasaidia watoto hao kuishi salama bila kupata maradhi mengine.
“Kwa yeyote mwenye kuhitaji kutoa msaada kwa watoto hao awasiliane na Hospitali ya Muhimbili.”
Itakumbukwa, hospitali hiyo pia iliwahi kufanya upasuaji wa pacha walioungana, Anishia na Melanese na ilifanikiwa kuwatenganisha Desemba 23, 2018. Walirejea nchini Ijumaa ya Agosti 30, 2019.
Kwa mujibu wa gazeti la nchini Saudi Arabia, saudigazette.com pacha hao walitenganishwa na jopo la wataalamu 32 kwa muda wa saa 13.
Pacha hao wa kike walizaliwa katika Kituo cha Afya cha Missenyi mkoani Kagera, Januari 2018.