Dar es Salaam. Katika kusherehekea miaka 63 ya uhuru a Tanganyika, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 1,548 ambapo 22 kati yao wanaachiliwa huru leo Jumatatu, Desemba 9, 2024.
Wafungwa wengine 1,526 wanabaki gerezani kumalizia sehemu ya kifungo kilichobaki baada ya kupewa msamaha huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kusainiwa na Naibu Waziri, Daniel Sillo, matarajio ya Serikali wafungwa hao watarejea tena katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa, letu na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.
Taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari inaeleza Rais ametoa msamaha huo kwa mamlaka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1) (a) – (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa msamaha kwa wafungwa.
Ibara hiyo inatoa msamaha huku ikiainisha masharti mbalimbali ikiwemo wafungwa wenye sifa mbalimbali wamepunguziwa robo ya adhabu zao wanazozitumikia hivi sasa baada ya kutoa punguzo la kawaida la moja ya tatu linalotolewa chini ya Kifungu cha 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58.
Wafungwa hao ni wale waliohukumiwa adhabu ya kifungo cha kuanzia miaka miwili na kuendelea, ambao wametumikia robo ya adhabu zao gerezani na walioingia gerezani kabla ya Oktoba 19, 2024.
“Pia wafungwa wenye magonjwa ya kudumu au sugu ambao wapo kwenye hatua ya mwisho. Ugonjwa na hatua hiyo viwe vimethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au wilaya.
Wafungwa hao kipengele cha kutumikia robo ya adhabu zao hakiwahusu na makosa yao ni yenye sifa ya kunufaika,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Sharti lingine ni wafungwa wote waliotumikia kifungo cha maisha gerezani bila kujali kosa ambao wametumikia adhabu zao kwa 15 na kuendelea wamebadilishiwa adhabu zao kuwa kifungo cha miaka 30 kuanzia tarehe ya hukumu.
Pia wafungwa waliobadilishiwa adhabu kwa msamaha wa Rais kutoka adhabu ya kifo na kuwa kifungo cha maisha ambao wametimiza miaka kumi na kuendelea tangu kupata msamaha huo, wamebadilishiwa kifungo cha maisha kuwa kifungo cha miaka thelathini gerezani.
Wengine ni wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini au zaidi, umri huo uwe umethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa mganga mkuu wa wilaya. Wafungwa hao kipengele cha kutumikia robo ya adhabu zao hakitawahusu na makosa yao yawe ni yenye sifa ya kunufaika.
“Pia wafungwa wa kike walioingia na ujauzito gerezani au wenye watoto wanaonyonya, wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili wasio na uwezo wa kufanya kazi, ulemavu huo umethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa wilaya au mkoa, wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kuwekwa kizuizini ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka kumi au zaidi,” imeeleza taarifa hiyo.
Hata hivyo, msamaha huo hautawahusisha wafungwa wanaotumikia vifungo vya nje na wale waliowahi kukiuka masharti chini ya Sheria ya Bodi za Parole Sura ya 400 (R.E 2002), na kurudishwa gerezani kutumikia adhabu zao.
Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji wa fedha, rushwa na usafirishaji au kujihusisha kwa namna yoyote ile na dawa za kulevya ikiwemo bangi.
Wengine ambao hawajaguswa ni wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya kujamiiana, utekaji au wizi wa watoto, kupoka, kuwapa mimba wanafunzi au makosa yoyote yale yanayohusiana na ukatili dhidi ya watoto na kujihusisha kwa namna yoyote ile na biashara haramu ya binadamu.
“Pia wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya kukutwa na viungo vya binadamu, unyang’anyi, unyang’anyi wa kutumia nguvu, unyang’anyi wa kutumia silaha, kumiliki silaha, risasi, milipuko au kujaribu kutenda makosa hayo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Wafungwa wanaotumikia kifungo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali au ujangili, wafungwa wanaotumikia kifungo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya wizi au ubadhilifu wa fedha za Serikali.
Wengine wasiohusika na msamaha huo ni wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kifo, wafungwa wanaotumikia vifungo gerezani kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali au kusaidia kutendeka kwa makosa hayo, wenye makosa ya kujaribu kuua, kujaribu kujiua au kuua watoto wachanga, ugaidi, uharamia na makosa ya kimtanda.