Wakati Tanzania Bara ikiadhimisha miaka 63 ya Uhuru, ni wazi kuwa uwezo wa kujenga hoja wa Mwalimu Julius Nyerere ulikuwa kiini cha kufanikisha Uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza Desemba 9, 1961.
Katika kitabu “Tanganyika’s Independence Struggle” kilichoandikwa na Pius Msekwa, Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Msekwa anaelezea jinsi uwezo wa kipekee wa Nyerere wa kujenga hoja ulivyowashawishi viongozi wa chama cha Tanu kumtuma kwenda Baraza la Wadhamini la Shirikisho la Umoja wa Mataifa (UNO), ambalo sasa linafahamika kama Umoja wa Mataifa (UN).
Msekwa anasema mwaka 1954, wajumbe wa Baraza la Wadhamini la UNO walipokuja Tanganyika walitoa mapendekezo ya ratiba ya kuipa nchi uhuru ndani ya kipindi cha miaka 20 hadi 25. Wakati huo, Nyerere alikuwa mwalimu katika Shule ya Mtakatifu Francis, Pugu, ambayo sasa inajulikana kama Shule ya Sekondari Pugu.
Hata hivyo, viongozi wa Tanu walipinga ratiba hiyo wakiona ni kuchelewesha maendeleo ya nchi. Walimkabidhi Nyerere jukumu la kuwasilisha hoja ya Tanganyika kupata Uhuru haraka zaidi kwenye Baraza la Wadhamini la UNO huko New York, Marekani.
Nguvu ya hoja na matokeo ya haraka
Kwa ushawishi wa hoja za Nyerere, Tanganyika ilipata Uhuru ndani ya miaka saba tu, kutoka mwaka 1954 hadi 1961, tofauti na mapendekezo ya miaka 20-25. Mafanikio haya yalimfanya Nyerere kuwa kiongozi mwenye mvuto mkubwa kitaifa na kimataifa.
Changamoto ya uamuzi mgumu
Aliporejea kutoka UNO, Nyerere alikumbana na barua kutoka kwa Padri Walsh, mkuu wa Shule ya Mtakatifu Francis, akimtaka achague kati ya siasa na kazi ya ualimu.
Kwa maoni ya Walsh na wamisionari wenzake, Nyerere alionekana kuwa mwanaharakati wa kisiasa zaidi kuliko mwalimu wa kawaida.
Tatizo hilo liliwasilishwa kwa Clement Mtamila, Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Tanu. Kamati hiyo iliku-tana nyumbani kwa Mtamila kmtaa wa Kipata, na baada ya mjadala, ilimshauri Nyerere kujiuzulu. Machi 23, 1955, Nyerere aliacha rasmi kazi ya ualimu na kujitosa kikamilifu kwenye siasa.
Uamuzi huo wa Nyerere uliashiria mwanzo wa safari yake kama kiongozi wa kitaifa. Siku hiyo, alisafiri kutoka Pugu hadi Dar es Salaam akiwa si mwalimu tena, bali kiongozi aliyejitoa kikamilifu kuikomboa Tanganyika.
Miaka 63 baadaye, mchango wa Mwalimu Nyerere unabaki kuwa mfano wa uzalendo na uongozi wa maono, akiwahamasisha Watanzania kuendeleza azma ya kujitegemea na maendeleo.
Mwanahistoria Mohammed Said, mwandishi wa kitabu kuhusu Abdulwayde Sykes, anasimulia tukio hili kupitia simulizi aliyosikia kutoka kwa mtoto wa Iddi Faiz Mafungo, aliyekuwa mweka hazina wa Tanu kabla ya uhuru. Said anaeleza jinsi mipango ya safari ya Nyerere ilivyopangwa sebuleni nyumbani kwa Mafungo.
Mafungo, akiwa mweka hazina wa Tanu, alihusika kukusanya fedha. Mwanahistoria huyo anasema jioni moja ya Februari, kikao muhimu kilifanyika nyumbani kwa Mafungo, kikihusisha viongozi wengine mashuhuri wa Tanu, akiwemo Oscar Kambona na John Lupia, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanu.
Katika kikao hicho, Kambona na Lupia walimweleza Mafungo changamoto za kifedha zilizokuwepo.
“Sheikh, kama unavyoelewa bado hatujapata pesa za kutosha kumpeleka Mwalimu UNO.”
Kwa mujibu wa simulizi hiyo, Mafungo alipewa jukumu la kwenda Tanga kuchukua fedha zilikusanywa na wanachama wa Tanu chini ya uongozi wa Mwalimu Kihere.
Fedha hizo zilikusanywa kufanikisha safari ya Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa, safari ambayo ingekuwa ya kwanza kwake kuzungumza mbele ya Baraza la Wadhamini la UNO.
Safari hiyo ilifanikiwa kutokana na mshikamano wa viongozi wa Tanu na wanachama wake, licha ya changamoto za kiusalama kutoka kwa watawala wa kikoloni wa Uingereza.
Kwa Said, simulizi hii inaakisi mchango wa watu kama Mafungo na viongozi wa Tanu waliojitolea kwa hali na mali kuhakikisha ndoto ya uhuru inakaribia kutimia.
Katika kikao cha Tanu kilichofanyika nyumbani kwa Iddi Faiz Mafungo, John Lupia alimweleza Mafungo kuhusu taarifa walizopokea kutoka Tanga kwamba mwanachama wa Tanu, Mwalimu Kihere, aliripotiwa kuwa amekusanya fedha kutoka kwa wanachama wa chama hicho, fedha ambazo zilikuwa muhimu kufanikisha safari ya Mwalimu Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa.
Mafungo, akiwa mweka hazina wa Tanu, alipewa jukumu la kwenda Tanga kuchukua fedha hizo.
Mafungo alisafiri kwenda Tanga salama na kukabidhiwa fedha hizo, lakini hakujua kuwa alikuwa akifu-atiliwa kwa karibu na maofisa wa ‘Special Branch’, idara ya ujasusi ya polisi wa kikoloni wa Uingereza.
Wakati huo, Waingereza walijua kuhusu mipango ya Nyerere kwenda UNO na walikuwa wakifanya kila jitihada kufuatilia harakati za Tanu.
Akiwa na wasiwasi kuhusu usalama wa fedha hizo, Mafungo alibuni mpango wa kuzilinda. Akiwa ndani ya basi lililokuwa likielekea Dar es Salaam, alimkabidhi begi lenye fedha binti mdogo aliyekuwa akisafiri kwenye basi hilo. Kwa busara, hakukaa karibu na binti huyo na alihakikisha hawakujulikana kuwa wali-husiana.
Safari yao ilipofika katikati ya njia, basi lilisimamishwa na Land Rover ya polisi wa kikoloni. Mafungo alishushwa pamoja na mizigo yake kwa ukaguzi wa kina, huku abiria wengine wakiruhusiwa kuendelea na safari. Polisi walimpekua Mafungo na mizigo yake kwa makini, lakini hawakupata chochote.
Hawakujua kuwa binti mdogo aliyekuwa kwenye basi hilo ndiye aliyekuwa na begi lenye fedha. Baada ya kuwasili Dar es Salaam, binti huyo alizifikisha fedha hizo salama makao makuu ya Tanu, eneo ambalo sasa linafahamika kama ofisi ndogo za makao makuu ya CCM Lumumba.
Mafungo alikamatwa na kuhojiwa Kituo Kikuu cha Polisi kilichokuwa karibu na ofisi za reli (sasa eneo la stesheni ya SGR). Baada ya uchunguzi, hakufunguliwa mashtaka kwa sababu hapakuwa na ushahidi wowote wa kumtia hatiani.
Wanaharakati waliojitoa muhanga
Mwanahistoria Mohammed Said anasema mafanikio ya harakati za uhuru yalitokana na juhudi za watu waliotoa muda, mali na hata kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya Tanganyika.
Anamtaja Sheikh Mohamed Rania wa Bagamoyo, ambaye ushawishi wake ulihamasisha wanachama wa Tanu katika eneo hilo. Mafungo alimpeleka Mwalimu Nyerere kwa sheikh huyo ambaye alikuja ku-wa sehemu muhimu ya harakati hizo.
Mwanaharakati mwingine aliyetoa mchango alikuwa Mwamtoro binti Chuma, ambaye nyumba yake jijini Dar es Salaam iliunganishwa na ofisi za Tanu ili kurahisisha mikutano ya usiku na kupanga mikakati ya ukombozi.
Wanaharakati wa kike wengine kama Nyange binti Chande wa Tabora, Halima Selengia wa Kaskazini, na Lucy Lameck walitoa mchango katika nyanja mbalimbali za harakati hizo.
Vijana watukutu walinzi Siku ya Uhuru
Katika shamrashamra za kutangaza uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, hofu ilikuwepo kwamba huenda siku hiyo ingetibuliwa na vitendo vya uhalifu. Hata hivyo, kupitia ujasiri na mbinu za ubunifu za viongozi wa Tanu, hali hiyo ilidhibitiwa kwa njia ya kipekee.
Said anaeleza jinsi Kamanda Rajabu Diwani, aliyekuwa Kamanda wa Vijana wa Tanu, alivyochukua hatua ya kuwajumuisha vijana watukutu wa Dar es Salaam katika mpango wa kulinda mji.
Vijana hao, ambao awali walijulikana kwa tabia zao za kuleta vurugu, walipewa sare rasmi na kibarua cha kusimamia amani. “Diwani aliwakusanya vijana waliokuwa maarufu kwa utukutu na kuwapa juku-mu la kuhakikisha mji unakuwa salama siku ya sherehe za Uhuru,” anasema Said.
Katika siku hiyo muhimu, vijana hao walifanya kazi ya kuigwa.
Miaka 63 baadaye: Undugu umepungua
Huku akiangalia historia ya Tanganyika, Said anasema moja ya mambo ya kipekee yaliyokuwepo wakati huo ni mshikamano wa undugu uliowajumuisha Watanganyika wote.
Anahuzunika kuona mshikamano huo umepungua kwa kiasi kikubwa sasa. Licha ya maendeleo katika miundombinu na sekta nyingine, undugu uliochochea harakati za uhuru hauonekani kwa nguvu ile ile.