TFS yasherehekea miaka 63 ya uhuru kwa upandaji miti

Rukwa/Sengerema. Katika kuadhimisha miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), imetoa miche ya miti kwa taasisi za serikali kwa lengo la kupandwa ili kuboresha mazingira.

Maadhimisho hayo yamefanyika leo Jumatatu, Desemba 9, 2024 katika maeneo tofauti nchini, huku mkoani Rukwa TFS ikitoa miche 1,000 kwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Rukwa iliyopo katika Mji wa Laela ili kuboresha na kutunza mazingira ya shule hiyo.

Akizungumza na wananchi wa Laela kabla ya kuanza upandaji miti, Katibu Tawala wa Wilaya ya Sumbawanga, Gabriel Masinga amewataka wananchi kuendelea kupanda miti na kuitunza sambamba na kutunza afya zao kwa kufanya mazoezi.

Pia, amewataka kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kuilinda amani na mshikamano, ili Tanzania iendelee kuwa na umoja na utulivu kama nguzo ya mafanikio.

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Lumeya iliyoko Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza wakipanda miche kwenye shule hiyo Kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika. Picha na Daniel Makaka

“Hakuna uhuru wa Taifa kama hakuna uhuru binafsi, hatuwezi kuulinda uhuru wa Taifa kama hatuwezi kuulinda uhuru binafsi, tujikomboe kifikra kiuchumi tunaweza kuikomboa nchi,” amesema Masinga.

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi katika tukio hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga vijijini, Kwangwalu Misana amesema wameadhimisha siku hiyo kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya mji wa Laela na kushiriki kupanda miti katika sekondari ya wasichana ya Laela.

“Miche hii tuliyoipanda ni kielelezo tosha cha kuwa tunataka mazingira yaendelee kutunzwa kwa kuhakikisha kila mwanafunzi wa shule hii analinda mche wake, jambo hili litasaidia kuitunza mazingira,” amesema.

Baadhi ya wanafunzi na wananchi wamesema watailinda miti hiyo kwa lengo la kutunza kumbukumbu sambamba na kutunza mazingira ya shule hiyo.

Mhifadhi Mwandamizi wa TFS mkoani Rukwa, Adolf Mara amewataka wanafunzi na wananchi kujijengea utamaduni wa kupanda miti na kuacha kasumba ya kupanda miti na kuitelekeza.

“Itunzeni miche hii ya miti nayo itawatunza kwa kupata hewa safi, kivuli na matunda ambayo yataboresha afya zenu,” amesema.

Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani hapa nayo imeadhimisha miaka 63 ya uhuru kwa kufanya usafi katika soko la Laela na kuwatembelea wagonjwa.

Wakati huohuo, wilayani Sengerema mkoani Mwanza, TFS imegawa bure miche zaidi ya 37,500 ya matunda na mbao kwa taasisi binafsi, za Serikali na watu binafsi kwa ajili ya kupandwa ili kuhifadhi mazingira.

Miche hiyo yenye gharama ya Sh26.7 milioni imetolewa ikiwa ni utekelezaji wa mikakati na mipango ya TFS Wilaya ya Sengerema kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025, huku Serikali ikiweka lengo la kupanda miche milioni 1.5 kila mwaka.

Akigawa miche hiyo leo inayokwenda kupandwa katika mitaa na maeneo ya taasisi za umma, Mhifadhi Misitu wilayani Sengerema, Stephen Oyugi amesema mpaka sasa TFS imeshatoa zaidi ya miche 70,000 kwa ajii ya kupandwa kwenye maeneo mbalimbali wilayani Sengerema.

Baadhi ya wananchi wamepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kulinda na kuhifadhi mazingira, hususan kwenye maeneo ya vyanzo vya maji.

Shule ya Msingi Lumeya ni miongoni mwa taasisi za Serikali zilizonufaika na msaada wa miche ya miti ya matunda na mbao kutoka TFS.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Msaghaa Kitiku ameushukuru wakala huo huku akiahidi kuhakikisha miti hiyo inatunzwa ipasavyo.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Sengerema, Cuthbert Midala amesema uongozi wa Serikali wilayani humo utaendelea kutekeleza mipango ya uhifadhi wa mazingira kwa kuhamasisha wananchi kupanda miti na kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yao.

Related Posts