TPA YAENDELEA KWA KASI YA MABORESHO YA TSHARI ILIYOZAMA MAFIA

Mwamvua Mwinyi, Mafia Desemba 9, 2024

KAMPUNI ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inaendelea na maboresho ya miundombinu katika kisiwa cha Mafia, ikiwemo kurekebisha tshari iliyozama Septemba mwaka huu, ili kurejesha huduma muhimu za usafiri wa majini.

Sambamba na hilo, TPA kwa kushirikiana na wataalamu, inaendelea kutafuta eneo sahihi kwa ajili ya ujenzi wa bandari mpya kama suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazokumba usafiri wa majini katika kisiwa hicho.

Msimamizi wa Bandari ya Nyamisati, Mohammed Mkango, alieleza juhudi hizo wakati wa kufungwa kwa Maonyesho ya Utalii Mafia.

Mkango alisema ,mamlaka hiyo inasimamia bandari ndogo, zikiwemo za Nyamisati, Mafia, na Kisiju, huku ikiboresha gati zinazotumika na meli katika safari kati ya Nyamisati na Mafia.

Mkango alisisitiza kuwa jitihada kubwa zimeelekezwa Mafia, hususan katika sleepway ya Kilindoni eneo la upakiaji na upakuaji wa mizigo, magari, na abiria.

“Tshari hiyo imeibuliwa na ipo katika hatua za mwisho za matengenezo,kipande kidogo tu kimebaki kabla ya kurejesha huduma kwa wananchi,” alisema.

“Changamoto hizi zinasababisha ratiba za meli zinakumbwa na athari za maji kupwa na kujaa, hali inayosababisha ucheleweshaji wa safari na usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa huduma hizo.

Kwa mujibu wa TPA makao makuu, wakandarasi wanaendelea na kazi ya matengenezo ya tshari, huku mipango ya maboresho ya miundombinu ikitegemea bajeti ya mwaka husika.

“Changamoto zilizojitokeza zinafanyiwa kazi haraka ili kupunguza kero kwa wananchi.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph Kolombo, alihimiza TPA kuharakisha maboresho ya bandari na gati ili kupunguza utegemezi wa ratiba za maji na kupata suluhisho la kudumu.

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, aliishukuru Serikali kwa hatua za kushughulikia changamoto za usafiri wa majini.

Alisema juhudi hizo ni muhimu kwa kuhakikisha huduma za usafiri zinaimarika, na hivyo kuboresha maisha ya wananchi na kuvutia watalii n sanjali na uwekezaji.

Related Posts