Dar es Salaam. Rais mstaafu, Jakaya Kikwete amesema kukamilika kwa ujenzi wa kampasi ya Taasisi ya Taaluma za Bahari (IMS), iliyopo Buyu, Zanzibar kutaiweka Tanzania kwenye nafasi nzuri hasa eneo la tafiti za sayansi ya bahari ukanda wa Afrika Mashariki.
Kampasi hiyo itakayokuwa na kituo cha utafiti, itaifanya Tanzania kung’ara kwenye tafiti za sayansi ya bahari na mazao yake hasa katika kipindi hiki ambacho nguvu kubwa imewekwa kwenye uchumi wa buluu.
Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kampasi hiyo iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), jana, Desemba 8, 2024 Kikwete ambaye ni mkuu wa chuo hicho amesema kituo hicho cha utafiti kitaiongezea hadhi kimataifa taasisi hiyo ya elimu ya juu.
“Tunapozungumzia uchumi wa buluu ni dhahiri tunaweka nguvu pia katika maeneo muhimu kama haya ya utafiti wa sayansi za bahari na mazao ya bahari. Kwa hiki kinachoendelea hapa ni wazi tunakwenda kuwa na kituo kikubwa cha utafiti kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki,” amesema.
Kikwete pia ameeleza furaha yake baada ya kuona hatua ya ujenzi wa kampasi hiyo ambayo ilisimama kwa takribani miaka 20, kabla ya kupata fedha chini ya mradi huo na kuanza upya kwa ujenzi.
“Nilipoteuliwa kuwa mkuu wa chuo nilitembelea kampasi zote zilizo chini ya UDSM, nilikuja hapa Buyu nikakuta jengo moja na huku kwingine kuna msingi ambao ujenzi wake ulisimama kwa miaka 20.
“Wacha tu niseme maana najua siku hizi tukisema unaambiwa umekuwa chawa, Rais Samia ametusaidia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha ujenzi wa kampasi hii unaendelea na ulipokuja huu mradi tukaelekeza nguvu na hatimaye tunaona mwakani kazi inaenda kukamilika,” amesema Kikwete na kuongeza:
“Haikuwa rahisi, kulikuwa na ugumu na ikabidi tutumie maarifa zaidi, ikiwemo kuzungumza na wakubwa kwa maana wakuu wa nchi wa pande zote mbili hadi kufikia kuanza upya kwa ujenzi huu ambao ulisimama kwa miaka 20, yaani hadi msingi ulishakuwa mweusi kabisa.”
Mtaalamu aliyehusika kwenye uandaaji michoro wa majengo hayo yanayojengwa sasa, Dk Fatma Mohamed amesema kabla ya kuanza kwa awamu mpya ya ujenzi walifanya sampuli kuhakiki kama msingi huo uliodumu kwa miaka 20 ungefaa.
“Tulifanya vipimo vya kisayansi kujiridhisha kama huo msingi unafaa kuendelea na ujenzi au ujengwe mwingine, matokeo yakatuonyesha bado ni imara, hivyo tunaweza kuendelea na uandaaji wa michoro kwa kuongeza maeneo ambayo hayakuwepo kwenye ramani ya awali, ikiwemo vyumba vya kompyuta,” amesema Dk Fatma.
Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa kampasi hiyo, Naibu Mratibu wa mradi wa HEET, Dk Liberato Haule amesema umefikia asilimia 50 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamlika Agosti 2025.
Mradi huo unaogharimu Sh11.1 bilioni ukihusisha ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 40, jengo la utawala na taaluma.
Kuhusu jengo la utawala na taaluma, Dk Haule amesema litahusisha madarasa manne yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 216, ukumbi wa mikutano wa watu 150 na maabara tano.
Amesema taasisi hiyo kwa sasa inadahili wanafunzi 88, ila ujenzi utakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 200.