Ujumbe wa Rais Samia maadhimisho miaka 63 Uhuru wa Tanganyika

Dar es Salaam. Ulinzi wa tunu za amani, umoja na mshikamano ndiyo ujumbe wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania wanapoadhimisha miaka 63 ya uhuru.

Ujumbe wa Rais Samia unakuja, ikiwa siku kama ya leo Desemba 9, miaka 63 iliyopita yaani mwaka 1961, Tanganyika ilipata uhuru wake kutoka utawala wa Uingereza.

Baadaye mwaka 1964, Tanganyika iliungana na Zanzibar na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jina linalotumika hadi sasa.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, mkuu huyo wa nchi alitangaza kufuta sherehe, badala yake fedha zilizopangwa kufanya shughuli hiyo zielekezwe kwa jamii.

Uamuzi huo si wa kwanza nchini, kwani umewahi kufanywa mara kadhaa na mtangulizi wake, hayati John Magufuli ambaye alifuta sherehe hizo na kuelekeza fedha kutumika katika miradi ya maendeleo.

Akitoa ujumbe wa maadhimisho ya siku wa uhuru wa Tanganyika leo Jumatatu, Desemba 9, 2024, Rais Samia kupitia kurasa za mitandao yake ya kijamii amewatakia Watanzania heri ya miaka 63 ya uhuru, kuwasihi kuitumia siku hiyo kumshukuru Mungu kwa hatua zinazoendelea kupigwa katika maendeleo ya Taifa.

Pia amewataka wajivunie na kufanya kazi kuzilinda tunu za amani, umoja na mshikamano, akizitaja ndizo nguzo za mafanikio.

“Tujivunie na kwa pamoja tuendelee kufanya kazi ya kuzilinda na kuzitunza tunu za amani, umoja na mshikamano ambazo ndizo nguzo za mafanikio yetu,” ameandika Rais Samia katika kurasa zake hizo.

Related Posts