Tanga. Mkoa wa Tanga, upo Pwani ya kaskazini ya Tanzania, umepata sifa maalum katika masuala ya mapenzi na jinsi wakazi wake hasa wanawake wanavyodumisha na kuonyesha upendo wa dhati kwenye uhusiano.
Inasemekana kwamba, kama kuna mahali ambako mapenzi yanaheshimiwa na kuenziwa hapa, basi ni Tanga.
Hapa inaelezwa kuwa mapenzi hayachukuliwi kama hisia tu bali ni urithi wa kipekee unaopaswa kutunzwa na kuenziwa.
Mji wa Tanga, pamoja na wilaya zake umejipambanua kwa ustadi wa kuonesha hisia za mapenzi kupitia vitendo, maneno na mila za kale ambazo zimekuwa zikisifiwa sana.
Wakati huohuo wakazi wa Tanga wanaamini kwamba mapenzi ni sanaa ambayo inahitaji moyo wa kujali, subira na lugha ya sauti nyororo iliyojaa hisia.
Ukweli huo ndio uliomteka mkazi wa mkoani Tabora, Ezekiel Michael, anayesema yeye ni mmoja wa wanaume wanaokiri mahaba yapo Tanga, kwani katika mikoa ambao amepita kwa sasa amebaini hapo ndio mwisho.
Amesema wanawake wa Tanga sio tu wanasifika kwa mapenzi, lakini hata kwa upishi.
‘’Ukikutana na mwanamke aliyefundishwa na kuelewa somo la kuwekwa ndani , mwanaume hupindui kwake.
“Kweli mapenzi yamezaliwa Tanga tena ukija hapa huondoki kwa sababu ukikutana na mwanamke wa Tanga, huwezi kutafuta mwingine wanajua kujali ukikutana na hao wenyewe umekwisha maana wapo waliofundishwa na somo wamelielewa”, amesimulia Ezekiel.
Mwananchi imezunguka na kuongea na wananchi wa mkoa wa huo kutoka wilaya ya Handeni na Tanga mjini kwa nyakati tofauti, kutaka kujua ni kwa nini eneo hilo linasifika kwamba ndio mji ambao mapenzi yamezaliwa.
Mkazi wa Tanga Nicolas Kusaka, ambaye ni mzee wa kabila la Kizigua, amesimulia kwamba maandalizi ya tangu utoto kwenye malezi hadi utu uzima, ndio siri ya watu wa hapo kusifika kuwa na mahaba ya dhati kwenye uhusiano wakiwa watu wazima.
Amesema wakazi wa Tanga wanajulikana kwa lugha yao ya upole na ukarimu na huwa wanatumia maneno yanayobeba hisia nzito, yakiwemo “mpenzi wangu,” “moyo wangu,” na “nakupenda.”
Amesema maneno haya si ya kawaida bali yanatamkwa kwa sauti tamu na yenye upole, hali inayomfanya kila anayesikia ahisi kujaliwa na kuthaminiwa.
Kusaka amesema Tanga inajivunia mila na desturi zinazokuza mapenzi katika jamii. Kwa mfano, katika tamasha au sherehe za harusi, utaona jinsi watu wanavyoimba nyimbo za mapenzi, wakicheza na kufurahia maisha ya ndoa.
‘’Hivyo mtoto wa kiume na yule wa kike wanaandaliwa mapema kwa ajili ya maisha yao ya baadae, kuanzia kushiriki kwenye shughuli za kiichumi kwa kwenda shamba, kutafuta maji, kuni na mahitaji mengine ya msingi ambayo atakwenda kukutana nayo baadaye,’’ anasema.
Ameeleza kuwa kwa makabila ya Tanga kijana wa kiume anapokaribia umri wa balehe hufanyiwa tohara,ndani ya kitendo hicho ndio anafundishwa mambo yote kuhusu maisha anayokwenda kuishi baadaye akiwa na familia yake.
“Ule wakati ambao yule mtoto anawekwa ndani awe wa kiume au wa kike pale ndipo anapopewa mafundisho jinsi ya kuhudumia ndoa yake, na anapewa kabisa miongozo kwamba ukiwa kwenye ndoa jambo hili na hili huruhusiwi kufanya,hivyo ukifanya madhara yake ni haya”, anasimulia mzee Kusaka.
Mkazi wa Tanga, Rehema Rajabu amesimulia kwamba mabinti zao hutulia kwenye uhusiano yao kwa sababu binti anapotoka kwao, akirudi kwa kushindwa ndoa, lawama anataupiwa mama kwa kushindwa kutoa mafunzo bora kwa binti yake.
“Mtoto wako atoke kwake aende na kurudi sababu ya kwanza ni wewe mwenyewe mzazi, kwa sababu unatakiwa kumueleza anatakiwa akawe mvumilivu, amheshimu mume na jamii yake inayomzunguka na mafunzo mengine na kwa kufanya hivyo ataweza kuimudu ndoa yake”, anasema Rehema.
Amesema yapo mafunzo ambayo wanapewa wasichana wanapowekwa ndani ambayo yanampa kabisa msisitizo, kwamba ukifanya hili baba au mama yako anaweza kufa, hivyo kwa sababu ya hilo, binti anapata hofu ya kuingia kwenye vishawishi vya kuvunja ndoa yake.
Mkazi wa Barabara ya Tatu, Halima Hassani, anaeleza kwamba kwanza ni mwiko wao kueleza hadharani vitu ambavyo wanafundishwa wanapowekwa ndani, na msichana yoyote ambae amewekwa ndani na kuelewa somo hawezi kutoa mafunzo hayo hadharani.
Anasema anachoweza kueleza ni kweli wasichana au wanawake wengi wa Kitanga wapo vizuri kwenye kuhudumia uhusiano yao yawe kwenye ndoa au nje ya ndoa kutokana na mafunzo hayo.
“Yapo mambo mengi hasa sisi wanawake tunatakiwa kufanya kwenye ndoa zetu mapenzi sio tu kupenda lakini na vitendo viwepo ikiwa mume anataka kwenda au anarudi kazini. Ni kweli anaogeshwa, analishwa na huduma nyingine muhimu sasa ukishindwa kufanya hivyo wenzako watakusaidia”, anasema Halima.