Dar/Moshi. Sauti ya Ofisa wa Jeshi la Magereza ikiashiria iko siku maofisa wa Jeshi hilo wataonyeshana umwamba na wale wa Jeshi la Polisi nchini, imeibua mjadala katika mitandao ya kijamii juu ya uhalali wa kauli ya ofisa huyo.
Baadhi ya wanasheria wamesema kilichotokea ndio picha halisi iliyopo barabarani ambapo madereva wengi wa Serikali wanajiona wapo juu ya sheria wawapo barabarani, jambo ambalo halistahili katika nchi inayoheshimu utawala wa sheria.
Hata hivyo, alipotafutwa kwa simu jana, msemaji wa Magereza, Naibu Kamishina wa Magereza (DCP), Elizabeth Mbezi alijibu kwa kifupi; “Sasa suala hilo tayari limeshazungumzwa kati ya viongozi wa juu na limemalizwa. Siwezi kulisemea tena.”
Pamoja na kauli hiyo, lakini taarifa zinazosambaa mitandaoni huku zikimtaja kwa jina na cheo ofisa anayesikika katika video hiyo, zilidai Kamishina Jenerali wa Magereza (CGP), Jeremiah Katungu ameelekeza avuliwe nafasi ya uongozi wa timu.
Andiko hilo ambalo linasambaa linadai ofisa huyo alikuwa ameshindwa kukemea mwendo wa dereva ambao kwa mujibu wa Mfumo wa Kisatelaiti wa Ufuatiliaji Mwenendo wa Magari Barabarani (VTS), alikuwa katika spidi ya 125.
“Alishindwa kumuelekeza dereva kusimama aliposimamishwa na askari wa barabarani kuanzia huko Kagera. Huyu hatambui kuwa awapo barabarani yeye ni abiria tu na marehemu mtarajiwa wa ajali za barabarani,”linaeleza andiko hilo.
“Huyu Mkaguzi haelewi kuwa jukumu la trafiki ni kudhibiti mwendo wa ovyo na kuzuia ajali ambacho ndicho kilikuwa kinatekelezwa hapo,” linadai andiko hilo.
Tukio hilo limekuja wakati nchini kukiwa na mjadala kuhusu madereva wengi wa magari ya Serikali, mashirika ya umma na taasisi zake kuwa na kiburi na kutoheshimu sheria za usalama barabarani ikiwamo kuyapita magari mengine bila tahadhari.
Yanayosikika yakisemwa kwenye sauti iliyopo mitandaoni
Sauti hiyo kupitia mkanda wa video ambayo ilianza kusambaa kwa kasi mwishoni mwa wiki, inalionyesha basi la Timu ya Tanzania Prisons likiwa katika kituo kikuu cha Polisi mkoani Iringa kwa makosa ya barabarani.
“Hii ni Polisi Iringa tuko hapa tangu saa 5 safari yetu ilikuwa inatokea Kagera, RTO (mkuu wa trafiki mkoa) kazuia gari kwamba dereva kaover speed (mwendo kasi) alipotakiwa kwenda spidi 85 kaenda spidi 90,”anasikika ofisa huyo.
“Kazuia gari tangu saa tano tumerudishwa kutokea Ifunda na hapa Watanzania wa Tanzania Prisons tuko kituo cha Polisi Iringa. Tumejaribu kuongea naye, tumejaribu kufanya kila kitu lakini ikashindikana. Hatukutaka kutumia nguvu.”
“Ni kwa sababu uwezo wa kutuchukua hawakuwa nao, lakini ilibidi tutii sheria maana wamekuja na mabunduki na mabomu kama vile tumeua. Wanasahau kwamba sisi wote ni wizara moja, sisi wote ni askari.”
“Hatuna shida na Jeshi la Polisi lakini wanachokitafuta iko siku watakipata. Yaani kuna muda ifike tuheshimiane. Wanachokitafuta polisi iko siku watakipata kwa sababu kama tunataka kudhalilishana na tumeshindwa kuheshimiana waseme.”
Mratibu wa Mtandao wa Kutetea Haki za Binadamu (THDRC), Onesmo Ole Ngurumwa amesema tukio hilo linaonyesha sura halisi ya namna baadhi ya madereva wa taasisi za Serikali wanavyojiona wako juu ya sheria.
“Hiyo inatuonyesha picha halisi ya kile tunachokutana nacho barabarani. Mahali pa spidi 50 wao wanakwenda hata 120 na ku overtake vibaya na kuhatarisha maisha ya wengine.”
“Hakuna mtu anatakiwa asifuate sheria isipokuwa misafara ya viongozi, lakini wengine wote wanapaswa kufuata. Jeshi la Polisi wamefanya kazi yao vizuri. Haijalishi wewe ni jeshi lingine, wamefanya kazi vizuri,”amesisitiza Ngurumwa.
Ameongeza kusema kuwa, “wangekuwa wanatembea wenyewe huko barabarani (madereva wa Serikali) tungesema tuwaache wenyewe wafe, lakini kuna watumiaji wengine wa barabara, waache ubabe na mimi nawapongeza sana Polisi Iringa,”amesema wakili huyo.
Wakili Moses Mahuna wa Jijini Arusha amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 13 (1) inasema watu wote ni sawa mbele ya sheria bila kujali huyo anayelengwa na sheria ni nani na ana wadhifa gani.
“Unajua kuna kitu kinaitwa usawa mbele ya sheria, katika nchi hii hakuna mtu aliye juu ya sheria hata wale wanaoitekeleza kama Polisi, Magereza na vyombo vingine. Sheria ikishatungwa na kupitishwa na Bunge inatufunga wote,”amesema wakili huyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe amesema kama Taifa kuna haja ya kuanzisha mjadala wa kitaifa juu ya uwepo wa watu au taasisi zinazojiona zenyewe hazibanwi na sheria.
“Kilichofanyika ni uvunjifu wa sheria na unasimamishwa na trafiki husimami halafu unarekodi video na kurusha mitandaoni kuonyesha kama mlipaswa kupewa upendeleo. Bahati nzuri sheria haina excuse (haipendelei),” amesema Wangwe na kuongeza;
“Ingekuwa ina excuse ingesema wote wanapaswa kufuata sheria isipokuwa Polisi au Magereza. Mimi nafikiri lazima sheria ifuatwe. Kama Taifa tunapaswa kutafakari kwa nini baadhi ya watu wanajiona wako juu ya sheria. Si sawa,” amesisitiza.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), Anna Henga amesema katika nchi inayoheshimu utawala wa sheria kama Tanzania, hakuna mtu anayetakiwa awe juu ya sheria.
“Sheria zinatungwa kwa watu wote bila kujali huyu anafanya kazi taasisi gani. Hiyo ndio nchi inayofuata sheria. Mara nyingi baadhi ya madereva wa Serikali wanajifanya wako juu ya sheria, wanapita njia isiyostahili, mwendo kasi,” amesema.