Viongozi Manispaa ya Songea wabebeshwa zigo la taka

Songea. Viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, wameelekezwa kuhakikisha wanatoa kipaumbele kwa kuondoa uchafu unaotoa harufu mbaya kwenye mitaro ya mabucha ndani ya soko kuu kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa eneo hilo.

Agizo hilo limetolewa leo Jumatatu, Desemba 9, 2024 na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mary Makondo ambaye pia ni katibu tawala wa mkoa, wakati wa maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru yaliyoandaliwa kimkoa katika Manispaa ya Songea.

Makondo amewataka viongozi wa manispaa kuweka mikakati madhubuti ya kuondoa taka kwenye maeneo ya biashara na makazi kwa kushirikiana na wananchi, ili kuhakikisha mazingira yanakuwa safi wakati wote.

“Ndugu zangu wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, tujiepushe na uchafu na tushirikiane na Serikali kuhakikisha maeneo yetu ni masafi muda wote. Uchafu ndio chanzo kikuu cha magonjwa ya mlipuko. Viongozi waendelee kuhimiza wananchi kuzoa taka mara kwa mara,” amesema Makondo.

Aidha, amewashauri wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi wa mazingira yao kwa lengo la kulinda afya zao na kuimarisha ustawi wa jamii.

Kwa upande wake, Naibu Meya wa Manispaa ya Songea, Jeremiah Mlembe amekiri kuwepo kwa changamoto ya taka katika maeneo ya biashara, na ameahidi kuyatekeleza maagizo yaliyotolewa.

Kaimu mkurugenzi wa manispaa hiyo, Furaha Mwangakara naye amesema maeneo yanayohitaji usafi wa haraka yatawekewa mikakati maalumu kwa lengo la kuzuia magonjwa ya mlipuko.

 Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Ruvuma (TRA), Nicodemus Mwakilembe amewapongeza wananchi kwa kushiriki maadhimisho hayo na kuwataka waendelee kulipa kodi kwa hiari ili kuimarisha maendeleo ya nchi, huku akionya kuwa tozo za penati zitaanza kutekelezwa Januari mwakani.

Related Posts