Tabora. Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mohamed Mtulyakwaku, ameagiza wananchi wanaofanya shughuli za kilimo na ufugaji ndani ya maeneo ya hifadhi kuondoka mara moja, kabla ya oparesheni ya kuwaondoa kwa nguvu haijaanza.
Akizungumza leo Jumatatu, Desemba 9, 2024, wakati wa maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru yaliyofanyika kituo cha afya Maili Tano, Manispaa ya Tabora, Mtulyakwaku ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui, amesema Serikali imepokea taarifa za watu wanaoendesha shughuli katika maeneo ya hifadhi, hivyo wanatakiwa kuondoka kwa hiari kabla ya hatua nyingine hazijachukuliwa dhidi yao.
“Ndugu zangu wanaoendesha shughuli ndani ya maeneo ya hifadhi ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji na hata kujenga nyumba za kudumu, nawasihi waondoke mara moja. Agizo hili sio ombi, bali ni lazima na wote watakaokaidi wataondolewa kwa nguvu,” amesema.
Amesema tayari Serikali ilishatoa notisi kwa wakazi waliovamia maeneo kama ya Kigwa Lubuga, Igombe River, huku akisema maeneo mengine maalumu kwa ajili ya kilimo yaliyotengwa na yanatosha kwa matumizi ya wananchi.
“Hatutavumilia kuona mtu yeyote akilima au kufuga ndani ya hifadhi. Wavamizi wengi ni wahamiaji kutoka nje ya mkoa huu, si wenyeji wa Tabora, kwa hiyo wanapaswa kufuata utaratibu na sheria,” amesema kaimu mkuu huyo wa mkoa.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dk John Mboya ameunga mkono agizo hilo huku akionya juu ya athari za ukataji miti na uharibifu wa misitu.
Amesema vitendo hivyo vinachangia uharibifu wa mazingira na Serikali haitalivumilia.
“Utunzaji wa mazingira ni jukumu letu sote. Hata hivyo, wapo wachache wanaoharibu misitu kwa ukataji miti hovyo. Serikali itachukua hatua kali kwa yeyote atakayekamatwa akiendesha vitendo hivi,” amesema Dk Mboya.
Ametolea mfano wa kauli ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyewahi kukataa ombi la wakazi wa Isawima, wilayani Kaliua, waliotaka kufanya shughuli za kilimo na ufugaji ndani ya hifadhi, hivyo kusema viongozi na wananchi wanapaswa kujifunza kutokana na mfano huo wa kulinda mazingira.
Mhifadhi mkuu daraja la kwanza kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Nuru Tengeza amesema Mkoa wa Tabora una hifadhi 12 zenye ukubwa wa hekta 1,784,429.
Akizungumza na Mwananchi Digital, mkazi mmoja wa kijiji cha Mpandamlowoka, wilayani Kaliua, Simon Mrutu amesema kuna mgogoro wa muda mrefu kati ya wanakijiji na hifadhi ya Kigosi Muyowosi na kwamba tatizo la ukosefu wa uelewa wa mipaka lina mchango mkubwa katika hayo yanayoendelea kutokea.
“Changamoto kubwa inayotufanya tukutwe tunafanya shughuli hifadhini ni kutokujua mipaka sahihi ya vijiji na maeneo ya hifadhi yanayotuzunguka. Ikiwa Serikali itaongeza juhudi za kutoa elimu na kuweka mipaka inayoeleweka, migogoro hii inaweza kupungua kwa kiasi kikubwa,” amesema Mrutu.
Amesema licha ya agizo la Serikali la kuwaondoa watu waliovamia hifadhi, jitihada za kutoa elimu na kuweka mipaka wazi ni muhimu ili kuondoa hali ya sintofahamu miongoni mwa wananchi.
Hayo yanatokea siku chache baada ya kifo cha mtoto Grace Mussa (4) kilichotokea Desemba 5, 2024, aliyeuawa kwa risasi wakati wa operesheni ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) dhidi ya kilimo hifadhini Kigosi Muyowosi.
Inadaiwa tukio hilo lilitokea baada ya wakazi wa Kijiji cha Mpandamlowoka kuwazingira askari wa TFS waliokuwa wamekamata trekta lililokuwa likifanya shughuli za kilimo ndani ya hifadhi ya taifa ya msitu wa Kigosi Muyowosi.
Askari hao walipoona hali ya hatari, walifyatua risasi ambazo zilisababisha kifo cha mtoto huyo na kumjeruhi mtu mmoja.