Na Mwandishi Wetu.
WANAWAKE zaidi ya 300 wa Kijiji cha Marogoro na Mfuru Mwambao wamepatiwa matibabu kinga ya saratani ya mlango wa kizazi kutoka kwa Madaktari bingwa wa Taasisi ya Saratani Ocean road kupitia huduma ya mkoba za Mama.
Katika kampeni ya kuelimisha wananchi katika uchunguzi wa saratani mbali mbali zikiwemo mlango wa kizazi, matiti , tezi dume na saratani ya ngozi kwa watu wenye ualbino.
Akizungumza katika kampeni hiyo Meneja wa huduma za uchunguzi wa saratani na elimu kwa umma kutoka Taasisi ya Saratani Ocean road, Dkt Maguha Stephano, amesema kati ya wanawake 300 watatu wamegundulika kuwa na mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi na wamepatiwa matibabu kinga ili kuzuia athari za ugonjwa huo.
“Tunawapongeza wanawake hao kwa kutumia fursa hiyo na kujitokeza kwa wingi kwani hatua hiyo imesaidia kuwahi matibabu kwani wasingepata matibabu mapema wangeweza kupata saratani ya mlango wa kizazi,”amesema.
Dk. Maguha, ametoa mwito kwa wananchi kujitokeza kupata huduma hızo ambazo zinatolewa bila malipo.
Katika hatua nyingine madaktari hao bingwa wamewezesha utoaji wa chanjo ya saratani ya Papiloma kwa wanafunzi wasichana wa Shule ya Msingi Magodoro.
Chanjo hiyo inakinga dhidi ya maambukizi ya kirusi cha papiloma kinachosababisha saratani ya mlango wa kizazi ambacho huambukizwa kwa njia ya kujamiiana ni maalaum kwa kwa wasichana wenye umri wa 9 hadi 14.