Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu wanne, wakiwamo kondakta na utingo wa basi la kampuni ya Abood kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga ameiambia Mwananchi Digital leo Jumatatu, Desemba 9,2024 kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti Novemba 21,2024 katika kijiji cha Igawa mpakani mwa Mkoa wa Mbeya na Iringa.
Amesema katika tukio la kwanza, Itika Bugale (36) na Shamim Maxwell wanashikiliwa kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi kilo 33.5.
Kuzaga amesema watuhumiwa hao ni wakazi wa Kata ya Uyole jijini hapa ambao walisafirisha dawa hizo kwa kuhifadhi kwenye mifuko miwili ya sandarusi kupeleka jijini Dar es Salaam.
Katika tukio la pili, Kamanda Kuzaga amesema wanawashikilia kondakta wa utingo wa basi la kampuni ya Abood, Stanslaus Nyagawa (41) na Erick Methew (46) kwa tuhuma za kusafirisha bangi kilo 20 kupeleka Jijiji Dar es Salaam.
Kuzaga amesema watuhumiwa walikamatwa Novemba 21,2021 wakidaiwa kusafirisha bangi kutoka Mkoa wa Songwe kwenda Dar es salaam kwa kutumia basi la Kampuni ya Abood lenye namba T 823 DXJ.
Kamanda huyo amesema watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.
Mkazi wa Forest jijini hapa, Tausi Azole ameliomba Jeshi la Polisi kuweka mkazo wa doria za mara kwa mara kutokana na kuwepo kwa wimbi la biashara ya bangi ambayo imechangia kupunguza nguvu kazi kwa Taifa.
“Sasa hivi vijana wengi tena wadogo wanavuta bangi hadharani tu, wengine wanaaga majumbani humo wanaenda shuleni, lakini wanaishia kwenye vijiwe vya kuvuta bangi, polisi wawasaidie wazazi, vijana wanapotea,” amesema Azole.
Endelea kufuatilia Mwananchi.