Dar es Salaam. Wakati leo Jumatatu, Desemba 9, 2024 mwili wa aliyekuwa Mfamasia wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke (THHR), Dar es Salaam, Magdalena Kaduma ukiagwa, swali linaloulizwa na waombolezaji ni nani aliyemuua mfamasia huyo.
Desemba 4, 2024, familia ya Kaduma ilipokea taarifa za kupotea kwa binti yao Magdalena kupitia simu ya mumewe, Kenan Mwandalima na jtihada za kumtafuta zilifanyika na Desemba 6, 2024 mwili wake ulipatikana nyuma ya nyumba yao Kibamba, jijini Dar es Salaam walipokuwa wakiishia ukiwa umefukiwa kwenye shimo.
Polisi bado haijatoa taarifa juu ya tukio hilo, huku ndugu wa marehemu wakieleza waliripoti tukio hilo kituo cha polisi Gogoni na mumewe, Mwandalima anashikiliwa kwa uchunguzi zaidi.
Leo Jumatatu, Desemba 9, 2024 ndugu, jamaa na marafiki wamejitokeza nyumbani kwa wazazi wake, Tabata- Sanene, Dar es Salaam kumuaga mpendwa wao kabla ya kusafirishwa kwenda Makambako, Mkoa wa Njombe kwa maziko kesho Jumanne.
Mwananchi limezungumza na waombolezaji mbalimbali ambao licha ya kusikitishwa na tukio hilo, swali wanaloibua ni nani aliyemuua Magdalena (36).
“Wazazi siku zote wanaona ni heri mtoto augue na kufa kuliko kuuliwa na mtu halafu hawajui aliyefanya hivyo ni nani, inaumiza zaidi kwani muda wote watawaza alimkosea nini muuaji hadi akaamua kukatisha uhai wa mtoto wao,” amesema Judith Kalenga.
Mfanyakazi mwenzake ambaye hakutaka jina liandikwe amesema tangu amfahamu Magdalema mwaka 2017 hajawahi kumuona kwenye ugomvi, alikuwa akifanya kazi zake na kuondoka.
“Tangu nimfahamu Mage sijamuona akiwa na makundi, sema amekuwa msiri mno kwenye mambo yake, maana baada ya kuolewa tuliona mabadiliko ambayo hatukumuelewa, alianza kupauka na alikuwa na gari lakini akawa anakuja kazini na daladala,” amesema.
Amesema kwa kuwa hakuwa anasema kwa watu changamoto zake, hivyo ilikuwa ngumu kumuuliza kwa kuwa alikuwa anacheka na kufurahi na wafanyakazi wake na yeye akiwa msimamizi wa kitengo cha dawa katika Hospitali ya Temeke.
Kwa upande wa waumini wa Kanisa la Efatha tawi la Kibamba, Alice John amesema wameshangazwa na mauaji hayo na kushikiliwa kwa kiongozi wao ambaye ni katibu wa kanisa hilo, hivyo wameamua kumkabidhi Mungu kwa ajili ya familia ya marehemu.
“Hatujui muuaji ni nani na kushikiliwa kwa kiongozi wetu tumebaki na maswali hili linawezekana vipi kutendeka,” amehoji.
Mbali na hilo, swali lililopo ni kukimbia kwa aliyekuwa mfanyakazi wao aliyejulikana kwa jina moja la Hans ambaye mume wa marehemu amekuwa akilitaja jina hilo akiwa polisi.
“Sisi hatujui muuaji ni nani, lakini Mungu ndiye anayejua maana tangu umeuliwa mumewe amekuwa akitaja jina la Hans, ajitokeze kusema ukweli hakika nafsi itapumzika ukweli utakapojulikana,” amesema mmoja wa shangazi wa marehemu alipokuwa akilia.
Magdalena alizaliwa Januari 30, 1988 na alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chang’ombe, Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1995 hadi 2002.
Mwaka 2003 hadi 2007, alisoma sekondari ya wasichana St. Francis, Mbeya. Baadaye alijiunga na Shule ya Wasichana Marian, mkoani Pwani.
Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, alijiunga na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) mwaka 2007, na alihitimu mwaka 2011. Alianza kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili mwaka 2011 hadi 2012, kabla ya kujiunga na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke mwaka 2013 kama mfamasia hadi umauti ulipomkuta.
Marehemu Magdalena alifunga ndoa na Kenan Mwandalima katika Kanisa la Efatha Novemba 17, 2018.