Tarime. Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwaokoa watoto wa kike zaidi ya 180 waliokuwa wanatarajiwa kukeketwa katika msimu wa ukeketaji, unaoendelea katika wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara.
Watoto hao wameokolewa na kupelekwa katika nyumba salama iliyopo katika kituo cha kupinga ukeketaji Masanga wilayani Tarime kuanzia Desemba 3, 2024 hadi sasa kufuatia operesheni maalum inayofanywa na jeshi hilo kwaajili ya kuwanusuru watoto
Takwimu hizo zimetolewa wilayani hapa leo Jumatatu Desemba 9,2024 na Kamanda wa Polisi kanda Maalum ya Tarime/Rorya, Mark Njera kwenye maadhimisho ya kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, ambapo amesema koo tisa kati ya 12 za Wakurya katika kanda hiyo zinafanya tohara mwaka huu kwa mujibu wa mila na desturi zao.
Amesema ukeketaji unafanyika katika msimu wa tohara na kwamba kutokana na koo nyingi kufanya tohara mwaka huu, jeshi hilo liliona ipo haja ya kuongeza nguvu zaidi ili kuwanusuru watoto wa kike ambao wapo katika hatari ya kukeketwa katika msimu huu wa tohara ambao tayari umeanza.
“Jeshi la Polisi makao makuu limekubaliana na sisi na kutuongezea nguvu ya askari 150 ambao walifika kwenye mkoa wetu wa Tarime/Rorya tangu Desemba Mosi mwaka huu na kuanza kazi Desemba 3 na hadi sasa tumefanikiwa kuwaokoa wasichana zaidi 180 waliokuwa kwenye hatari ya kukeketwa,” amesema.
Kamanda Njera amesema askari hao kwa kushirikiana na wenzao wa kanda maalum, wanaendelea kutoa elimu juu ya madhara ya ukatili ikiwepo ukeketaji pamoja na kuendesha doria na kampeni maalum ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya ukeketaji na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa ujumla.
Hata hivyo, Njera amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia katika eneo hilo vinaendelea kupungua kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo jitihada zinazofanywa na Serikali, kwa kushirkiana na wadau kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukeketaji na ukatili wa kijinsia.
“Kwa mwaka huu 2024 jumla ya matukio 1,099 yanayohusu ukatili wa kijinsia yameripotiwa ikilinganishwa na mwaka jana kwa kipindi kama hiki, ambapo jumla ya matukio 1,163 yaliripotiwa hapa tunaweza kuona matukio yamepungua na juhudi bado zinaendelea,” amesema.
Amesema ili kumaliza kabisa vitendo vya ukeketaji ipo haja ya Serikali kutunga sheria maalum inayohusu ukeketaji, tofauti na sasa ambapo sheria inayotumika ina upungufu mwingi hali ambayo kwa namna moja ama nyingine, imekuwa ikichangia kuendelea kwa vitendo hivyo vya ukeketaji.
“Serikali pia ijenge nyumba salama na kufungua vituo jumuishi katika kila wilaya, ili kurahisisha huduma kwa waathirika na manusura wa ukeketaji. Pia kuwepo na madawati ya jinsia katika kila kituo cha Polisi ili iwe rahisi kushughulika na vitendo hivi kwa wakati,” ameongeza.
Akihutubia katika maadhimisho hayo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima amesema licha ya vitendo vya ukeketaji kupungua mkoani Mara, bado ipo haja ya wadau kuongeza nguvu zaidi ili kupambana na vitendo hivyo.
“Kwa mujibu wa utafiti wa masuala ya idadi ya watu na afya uliofanyika mwaka 2022, Mkoa wa Mara ni wa tatu kwa vitendo vya ukeketaji kwa asilimia 28 huku mikoa ya Arusha na Manyara ikiwa na asilimia 43 kila mmoja, hivyo niwapongeze wana Mara lakini tusibweteke jitihada zaidi zinahitajika ili watoto wetu wa kike wawe salama kabisa,” amesema Dk Gwajima.
Amesema utafiti pia unaonyesha kuwa vitendo vya ukeketaji vinafanyika kwa wingi zaidi katika maeneo ya vijijini,hivyo kutoa wito kwa wadau kupanga mikakati juu ya namna ya kufikisha elimu hasa kwa jamii maeneo hayo kuhusu madhara ya ukeketaji.
Amesema wadau hao watumie fursa za uwepo wa shule za msingi katika kila kijiji za sekondari za kata katika kila kata katika kufanikisha kampeni ya elimu dhidi ya ukeketaji hasa maeneo ya vijijini, huku akisema elimu hiyo inapaswa kutolewa kuanzia ngazi ya wanafunzi hadi jamii.
“Ukeketaji ni ukatili na kwa sababu hili jambo linahusisha imani, mila na desturi zipo njia mbalimbali za kupambana nalo mojawapo ni elimu na elimu hii kwasasa hebu tujikite huko vijijini ambapo hali sio nzuri na nina uhakika tukiamua tunaweza kutokomeza ukeketaji,” amesema.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Meneja Mkuu wa Mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko amesema mgodi huo umekuwa ukifanya jitihada mbalimbali kuwezesha suala la usawa wa kijinsia mahala pa kazi kutokana na dhana iliyojengeka katika jamii kuwa sekta ya madini ni ya wanaume.
“Tumefanikiwa kuwa na ongezeko la watumishi wanawake kwa asilimia 4.8 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, ambapo hivi sasa mgodi wetu una watumishi wanawake 461 sawa na asilimia 12.8 kati ya watumishi 3,613 hii yote inatokana na jitihada za makusudi zinazofanya na mgodi katika kuboresha na kuweka mazingira rafiki kwa wanawake kujiunga na kampuni,” amesema Lyambiko.
Lyambiko amesema pia mgodi huo umekuwa ukitekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo miradi inayolenga kuboresha suala la usawa wa kijinsia katika jamii, kama ujenzi wa mabweni ya wasichana na wodi za wanawake ambapo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita mgodi huo umetekeleza miradi 253 yenye thamani ya zaidi ya Sh22 bilioni.
Baadhi ya mabinti wanaohifadhiwa katika nyumba salama ya Masanga, wameiomba Serikali kujenga shule za bweni ili waweze kufikia ndoto zao za kielimu tofauti na ilivyo sasa ambapo baadhi yao wanashindwa kuendelea na shule baada ya kukataliwa na wazazi na walezi.
“Wakati wa ukeketaji kwa wale wanaofanikiwa kukimbilia Masanga wanapata shida baada ya msimu kuisha, kwani baadhi yao wanatengwa na wazazi hivyo wanashindwa kuendelea na masomo kwahiyo kama tutajengewa shule za bweni tutakuwa na uwezo wa kuzifikia ndoto zetu hata tukikataliwa na wazazi,” amesema Rhobi Marwa.