Wito wa amani, uwajibikaji na usafi vyatawala maadhimisho ya uhuru mikoani

Mikoani. Sherehe za maadhimisho ya uhuru zimefanyika kwa njia tofauti katika mikoa mbalimbali nchini ambapo wananchi na viongozi wameshiriki kufanya usafi huku wito wa amani ukitolewa kwa Watanzania wote.

Maadhimisho hayo yamefanyika kwa njia hizo kufuatia uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuahirisha sherehe hizo kwa mwaka huu, huku akielekeza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili hiyo kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Wakati maadhimisho hayo yakiendelea mikoani, Rais Samia ameandika kwenye ukurasa wake wa X akiwakumbusha Watanzania kumshukuru Mungu kwa hatua za maendeleo wanazopiga sambamba na kuzitunza tunu za taifa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, Kwangwala Misana wakati akipanda mti katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanzania Bara katika shule ya Sekondari ya wasichana Rukwa

“Kheri ya Miaka 63 ya Uhuru kwetu sote. Tutumie siku hii njema kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua kubwa tunazoendelea kupiga kimaendeleo kama Taifa.

“Tujivunie, na kwa pamoja tuendelee kufanya kazi ya kuzilinda na kuzitunza tunu za amani, umoja na mshikamano ambazo ndizo nguzo za mafanikio yetu,” ameandika Rais Samia kwenye ukurasa wake wa X.

Mkoa wa Arusha umeadhimisha siku ya uhuru kwa viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali na wananchi kufanya matembezi na maombi maalumu ya kuliombea Taifa na Mkoa wa Arusha.

Shughuli mbalimbali katika Jiji la Arusha zimesimama kwa zaidi ya saa tatu kupisha matembezi hayo ambayo yameongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda na viongozi wa dini kutoka madehebu mbalimbali mkoani hapa.

Matembezi hayo yaliyoanza saa 3 asubuhi leo Jumatatu Disemba 9, 2024, yameanzia eneo la Impala, ambayo yanapita sehemu mbalimbali na kuhitimishwa eneo la Mnara wa Azimio.

Barabara mbalimbali zimefungwa ambazo matembezi hayo yanapita huku mamia ya wananchi wakijitokeza kushiriki matembezi hayo huku wakiwa wanapeperusha bendera za Taifa.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala akisalimiana na baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo.

Viongozi hao wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Dk Maasa Ole Gabriel, walishirikiana kuongoza maombi hayo maalum kwa Taifa na viongozi wake.

Akizungumza katika maombi hayo, Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Shaban Bin Juma amesema amani ni muhimu na kuwa ni vema waumini wa dini zote nchini wakaomba Mungu ailinde Tanzania na kuificha na maaduni wa ndani na nje.

“Leo tumesimama kuitangaza amani na hii ni tafsiri halali ya uzalendo wa nchi yetu, kila nchi inayo mambo imeyaweka kama tafsiri ya uzalendo wa nchi hiyo na sisi kwa kushehereke siku ya Uhuru ni ishara ya kuonyesha upendo na uzalendo wetu,” amesema.

Huko Kilimanjaro, maadhimisho yamefanyika katika wilaya tofauti ambapo viongozi wa wilaya hizo wamehamasisha utunzaji wa amani kama jambo muhimu la kuchunga huku wananchi wakihamasisha kufurahia siku hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala amewataka wananchi katika wilaya hiyo kuitumia sherehe za maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika kama siku ya ‘mtoko’ na kuhakikisha wanaume na wanawake wanakuwa na uhuru wao katika kusherekea siku hiyo.

“Sherehe ya uhuru mwaka huu furahini, pendezeni, ile nguo ambayo umeisahau muda mrefu toka nayo, iwe ni siku ya mtoko katika wilaya yetu ya Rombo,” amesema Mwangwala.

Ameongeza kuwa: “Wazee siku hii ya leo msiwabane kinamama nyumbani, waacheni watoke kisha baadaye warudi nyumbani, na ninyi akina mama vilevile msiwabane waume zenu waacheni waende nao wakasherekee siku hii ya leo.”

Wafanyakazi wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Pwani wakifanya usafi kwenye mazingira ya Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi Kibaha ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya uhuru. Picha na Sanjito Msafiri

Katika Wilaya ya Moshi, mkuu wa wilaya hiyo, James Kaji amesema hatawavumilia watumishi wazembe wasiowajibika kazini wakiwemo wasioshiriki maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika, mwaka huu.

Kaji ameagiza majina ya waliokwepa kushiriki maadhimisho hayo yawasilishwe kwake mara moja ili wachukuliwe hatua.

“Watumishi wengi hawawajibiki mpaka wasukumwe au kushikiwa fimbo. Nchi hii ni yetu sote, sitavumilia uzembe huu. Wapo watu mitaani wanazunguka na vyeti lakini hawana kazi, ninyi mmepata nafasi msichezee nafasi hizi,” amesema.

Kwingineko mkoani Ruvuma, Kaimu Mkuu wa Mkoa huo, Mary Makondo ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa, wamewataka viongozi kuweka mikakati ya kuondoa taka kwenye maeneo ya biashara na makazi ya watu kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo hayo.

“Niwaombe sana ndugu zangu wananchi wa Ruvuma, chukieni uchafu na mshirikiane na Serikali kuhakikisha maeneo yenu ni masafi muda wote, maana uchafu ndio unaoleta magonjwa ya mlipuko. Viongozi wasimamie wananchi kuzoa taka,” amesema Makondo.

Wakati huohuo, wakazi wa Mkoa wa Pwani wameiomba Serikali kuanzisha adhabu kali ya kifungo cha maisha jela kwa wanaokutwa na makosa ya uharibifu wa mazingira, jambo ambalo wamesema litasaidia kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kupunguza magonjwa ya mlipuko.

Mkazi wa Kibaha, Alfa Samson amesema uharibifu wa mazingira ni tishio kwa taifa na adhabu kali dhidi ya waharibifu wa mazingira ingeweza kuwa fundisho kwa watu wanaoharibu makazi ya asili kwa faida yao binafsi.

“Mazingira ni kila kitu kinachomzunguka mwanadamu, ikiwemo miti. Lakini kuna watu wanakata miti kwa makusudi kwa faida zao na kuleta madhara kwa taifa zima. Hii ni hasara kubwa, sasa ni vema Serikali ikaweka adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa waharibifu wa mazingira. Hii itakuwa fundisho kwa wengine,” amesema Samson.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, James Kaji, akizungumza katika viwanja vya Mashujaa Manispaa ya Moshi, wakati wa maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru.

Katika hatua nyingine, Kaimu Mkuu wa mkoa wa Tabora Mohamed Mtulyakwaku ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui, amewataka wakazi wa mkoa huo wanaofanya shughuli za kilimo na ufugaji kwenye maeneo ya hifadhi ndani ya mkoa huo, kutoka mara moja kabla ya oparesheni ya kuwaondoa kwa nguvu haijaanza.

“Hatutakubali kumuona mtu akilima au kufuga ndani ya hifadhi na wale wote waliokuwepo watoke maana taarifa za walioko kwenye hifadhi taarifa zao tunazo na kibaya zaidi wanaovamia hifadhi zetu ni wale wanaohamia katika mkoa huu na sio wale waliozaliwa hapa,” amesema.

Imeandikwa na Janeth Mushi (Arusha), Janeth Joseph na Flora Temba (Kilimanjaro), Joyce Joliga (Ruvuma), Sanjito Msafiri (Pwani) na Johnson James (Tabora).

Related Posts