KOCHA wa Mashujaa, Mohamed Abdallah ‘Bares’, ameweka wazi malengo yake kwa timu hiyo ya Ligi Kuu Bara, akisema anataka kumaliza msimu huu 2024/25 katika nafasi nne za juu.
Kwa sasa, Mashujaa wanashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi, wakiwa na pointi 17 baada ya kushinda mechi nne, sare tano, na kupoteza tatu. Katika msimu uliopita, timu hiyo ilimaliza nafasi ya nane, na Bares anasema lengo lake ni kuleta mafanikio makubwa msimu huu.
Bares alisema kuwa amefurahishwa na maendeleo ya timu yake, ingawa anajua kwamba kuna changamoto nyingi za kukutana nazo katika mechi zijazo. “Ni jambo la muhimu kwetu kumaliza msimu huu katika nafasi ya juu. Lengo letu ni kumaliza katika top four, na tutapigana kufikia hilo,” alisema kocha huyo mwenye uzoefu.
Mashujaa kwa sasa wanajiandaa kwa mechi yao inayofuata dhidi ya KMC, itakayochezwa Desemba 12, na Bares anaamini kuwa licha ya rekodi ya kushindwa kwa mabao 3-2 walipokutana mara ya mwisho, timu yake itakuwa imara zaidi. “Tumejizatiti na tunatumai tutapata matokeo bora. Huu ni mtihani mwingine, lakini tuko tayari,” alisema kocha huyo.
Mashujaa wanahitaji ushindi ili kuendelea kupigania nafasi zao katika kumi bora.
Wakati huo huo, kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar na Gwambina, Mohamed Badru, alizungumzia uwezo wa Bares na timu ya Mashujaa. Badru, alisema kuwa kocha Bares ni mmoja wa makocha bora katika ligi, akijivunia mbinu na uongozi wake.
“Bares ana ujuzi mkubwa na ana mtindo wa kipekee wa kuongoza timu. Anaweza kuiongoza Mashujaa kufikia malengo yao, nimewatazama wapo na msingi mzuri katika kuzuia, ambapo anatakiwa kufanyia kazi ni katika kushambulia.”
Katika michezo 12 ambayo Mashujaa imecheza kwenye ligi, wamefunga mabao 11 na kuruhusu mabao manane.