BODI YA EWURA YARIDHISHWA NA HATUA ZA UENDELEZAJI WA MIRADI YA UMEME WA JOTOARDHI

 

Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA Prof.Mark Mwandosya (kushoto) pamoja na wajumbe wa Bodi, Menejimenti na watumishi wa EWURA na TGDC,wakishuhudia Mkurugenzi Mkuu wa TGDC Mathew Mwang’omba akifungua bomba kwenye chanzo cha kuzalisha umeme wa jotoardhi cha Kyejo-Mbaka, mkoani Mbeya leo 10 Desemba 2024 2024

…..

Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), leo tarehe 10/12/2024, imeonesha kuridhishwa na hatua zilizofikiwa katika uendelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme wa jotoardhi kwenye maeneo ya Ngozi (MW 70) na Kyejo-Mbaka (MW 60).

Ziara hiyo, inayoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Prof. Mark Mwandosya, imelenga kuona hatua iliyofikiwa katika uendelezaji wa miradi hiyo muhimu ya kimkakati.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Prof. Mwandosya alisisitiza umuhimu wa kupanua wigo wa vyanzo vya kuzalisha umeme ikiwemo jotoardhi ili kuboresha upatikanaji wa huduma za nishati kwa wananchi. “Ni wakati sasa wa kuwekeza zaidi katika vyanzo vingine vya kuzalisha umeme, hususan jotoardhi, ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata nishati ya uhakika na kwa gharama nafuu. Nishati ni injini ya maendeleo, na tuna kila sababu ya kutumia rasilimali tulizo nazo kwa ufanisi,” alisema Prof. Mwandosya.

Aidha, Prof. Mwandosya aliipongeza Kampuni ya Maendeleo ya Jotoardhi Tanzania (TGDC) kwa juhudi zake za kuhakikisha miradi hiyo inasonga mbele. Alielezea kufurahishwa kwake na msukumo uliopo katika kuendeleza rasilimali watu kupitia mafunzo akisema kuwa juhudi hizo ni muhimu kwa ustawi wa sekta ya nishati nchini.

“TGDC inafanya kazi nzuri si tu kwa kuweka msukumo katika maendeleo ya miradi bali pia kwa kuwekeza katika watu. Uendelevu wa sekta ya nishati unategemea zaidi rasilimali watu wenye ujuzi na weledi,” aliongeza.

Ziara hiyo pia imehudhuriwa na Kaimu Mkurugenzi wa Umeme wa EWURA, Mhe. Aurea Bigirwamungu, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa EWURA. Mha. Bigirwamungu alisisitiza dhamira ya kushirikiana na wadau wote kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa mafanikio, akisema, “Mmeanza, tutashirikiana, na tutamaliza.”

Miradi ya jotoardhi ya Ngozi, Kyejo-Mbaka na Songwe inatarajiwa kuongeza uzalishaji wa nishati safi na ya gharama nafuu, huku ikiwanufaisha wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Bodi ya EWURA ikiwa kwenye chanzo cha kuzalisha umeme wa jotoardhi cha Ngozi (MW 70) mkoni Mbeya, wakati Bodi hiyo ilipotembelea chanzo  hicho  leo 10 Desemba 2024

Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA Prof.Mark Mwandosya (kushoto) pamoja na wajumbe wa Bodi, Menejimenti na watumishi wa EWURA na TGDC,wakishuhudia Mkurugenzi Mkuu wa TGDC Mathew Mwang’omba akifungua bomba kwenye chanzo cha kuzalisha umeme wa jotoardhi cha Kyejo-Mbaka, mkoani Mbeya leo 10 Desemba 2024

Bodi ya EWURA ikiongozwa na mwenyekiti wake, Prof.Mark Mwandosya(katikati) ilipofanya ziara kwenye chanzo cha kuzalisha umeme wa jotoardhi cha  Ngozi pamoja na  Kyejo – Mbaka, mkoani Mbeya leo 10 Desemba 2024.

Related Posts