Dar es Salaam. Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ametaja maeneo yanayotumiwa vibaya na baadhi ya watumishi na wateja kuiba fedha benki, jambo linaloathiri sekta ya fedha.
Miongoni mwa maeneo hayo ni uuzaji wa dhamana za wateja kwa tamaa kwa kuwawekea masharti magumu ya kumalizia kiwango cha mkopo kilichosalia, na utoaji wa mikopo ambayo haina uwezekano wa kulipwa, jambo linalochochea mikopo chechefu.
Ameyasema hayo leo katika Jukwaa la sekta ya fedha 2024 lililowakutanisha wadau kutoka benki, bima na watoa huduma za kuweka na kukopa.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Dk Mwigulu amesema pamoja na mafanikio yanayoshuhudiwa katika ukuaji wa huduma za kifedha, yapo mambo si ya kufumbia macho kwa kuwa hayana afya kwa sekta hiyo.
Moja ya maeneo ni katika kudai mikopo kwa wateja ambao wameshaanza kulipa, huku wakiwa wameweka dhamana mbalimbali.
Alitolea mfano wa mteja ambaye amelipa asilimia 80 na kubakisha asilimia 20 ya deni, na akuwa baadhi wamekuwa wakipoteza dhamana zao kutokana na watumishi wasiokuwa waaminifu kuingia njama na wateja wapya.
“Sasa mtu ameshalipa asilimia 80, anakuja mteja mwingine amependa dhamana ya mteja ambaye amekaribia kumaliza deni lake anaongea na mtumishi wa benki, kinachotokea yule mteja wa kwanza anapigwa presha alipe mkopo ndani ya siku kadhaa,” amesema.
“Huu siyo utaratibu mzuri wa kuendeleza sekta ya fedha na kujenga ustawi wa jamii, mnapokaa peke yenu hili ni eneo lingine la kufanyia kazi ili tusiwatie umaskini wananchi wetu. Mtu ambaye ameshalipa asilimia 80 halafu unauza dhamana yake kwa ajili ya kupata 20 huku ni kumfanya awe maskini,” amesema.
Amewataka viongozi wa benki kufanya mapitio ya kina kabla ya kufanya minada, ili kuepuka kuwa na sifa ya kuwa wakusanyaji wazuri wa madeni bila kujua kuwa wanabariki ‘upigaji’ wa watu.
“Tukilitatua hilo tutasaidia wananchi wasiogope benki, kuna tatizo la watu kuona wanaweza kuwa salama kupata mikopo katika taasisi bubu, mikopo kausha damu kwa kuhisi nikienda benki sitakuwa salama, lazima tuwaonyeshe wananchi kuwa hawako salama wanapokwenda kausha damu na wako salama kwenye taasisi rasmi za fedha,” amesema.
Sehemu nyingine inayopaswa kufanyiwa kazi ni njama wanazofanya wateja ili wasilipe mikopo wanayopewa, huku akisema jambo hilo wakati mwingine huanzia tangu mkopo unapotolewa.
Amesema wapo watu ambao wanachukua fedha wakiwa wamepanga kutolipa, wakijiita wajanja wa mjini, bila kujua wanaua uchumi wa nchi.
Amesema baadhi yao wanapoguswa hukimbilia mahakamani kwa sababu wanajua mchakato wake hautachukua wiki moja.
“Hili kundi pia nalo kama nchi hatupaswi kulifumbia macho, unachukua fedha na unapanga kutolipa kwa makusudi, unaanza janjajanja na kona nyingi.
“Hili lipo, tukifuatilia katika baadhi ya mikopo ambayo mingine imeishia katika mikono ya sheria na mingine kuwa mikopo chechefu, ikiangaliwa ilivyotoka inaonekana lazima kulikuwapo na njama ovu tangu mkopo unapotengenezwa,” amesema.
Alitumia nafasi hiyo kuwapongeza kinamama kwa kufanya vizuri katika kurejesha mikopo na kuelekeza fedha wanazochukua katika shughuli walizokusudia kwa asilimia 90 tofauti na wanaume.
“Kina baba wakikopa fedha subirieni kuona makochi yanabebwa na TV, asilimia kubwa haipelekwi katika sehemu iliyokusudiwa. Tuendelee pia kusisitiza kuwa pesa ya mkopo inatakiwa kufanya kazi inayoweza kuzalisha,” amesema.
Ametolea mfano Tanzania inapokopa zote fedha hizo huelekezwa katika miradi mahususi ya maendeleo na hakuna siku inayokopa kwa ajili ya mishahara.
Akijibu hoja zilizotolewa na Waziri wa Fedha, Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), Theobald Sabi amesema watakwenda kufanyia kazi yale yaliyosemwa ili kujenga imani kwa Watanzania na kuwashawishi kutumia mifumo rasmi ya kifedha kutoa huduma.
Amesema anaamini kuwa benki bado ni sehemu salama kwa wananchi kukopa pasipo kupata matatizo, huku akisisitiza kuwa hilo litafanyika kwa kuwapatia elimu wananchi.