Hii ndiyo sababu ya Wachaga kupenda bishara, fedha

Moshi.Ni maneno ya kawaida kwa walio wengi kuwa Wachaga wanapenda biashara na hata wengine wakaenda mbali zaidi na kusema watu wa kabila hilo maarufu nchini, wanapenda pesa.

Jambo hili limepata umaarufu mkubwa zaidi kutokana na watu wa kabila hilo kutapakaa maeneo mbalimbali nchini na kuanzisha biashara ambazo zimewapa umaarufu katika maeneo hayo.

Hilo linadhihirishwa na ukweli kwamba Wachaga walio wengi  ambao hujulikana kwa jina maarufu ‘Mangi’ wamejikita katika biashara tofauti.

Kwa kabila hilo, sio ajabu ukienda dukani ukamkuta  baba, mama na watoto wakichakarika kutafuta riziki.

Uchakarikaji huo unatajwa ni moja ya kichocheo kikubwa cha maendeleo katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kilimanjaro ambao ndio eneo la asili la Wachaga. Ni maendeleo yanayotajwa kuwapo mkoani humo   tangu enzi za ukoloni.

Mwananchi limezungumza na baadhi ya  wakazi wa Mkoa huo wakiwemo wafanyabiashara, wanaosimulia chimbuko la watu wa mkoa huo kuwa maarufu katika biashara.

Elisaria Mrema, mkazi wa Mbokomu Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, anasema tangu  enzi za utawala wa kikoloni,  Wachaga walijifunza biashara hali ambayo iliwawezesha kuifahamu fedha vizuri.

Mrema ambaye ni mwalimu mstaafu, anasema wakati wa ukoloni, Wachaga walijifunza kilimo biashara na hata kubadilishana bidhaa na fedha hali ambayo iliwajenga kufahamu biashara na kuwa na nidhamu ya fedha.

“Wachaga wengi hata wale ambao hawakwenda shule waliweza kuhesabu fedha na hii inatokana na namna walivyokuwa wameelekezwa na kuaminishwa thamani ya fedha na matumizi yake katika kukidhi maisha ya kila siku,”anasema Mrema.

Anaongeza: “Lakini pia mali nyingi ziliingizwa na wakoloni ikiwemo magari na bidhaa kutoka viwandani na Wachaga walifanya jitihada kutafuta fedha ili kupata vitu hivyo na iliwafanya kuwa na uelewa wa kutafuta fedha kununua vitu mbalimbali.”

Aidha, anasema hali hiyo iliwasukuma kulima mazao ya biashara ikiwemo kahawa ambapo watu wengi walilima na kupata fedha.

“Walifanya kilimo biashara cha kahawa na baadaye wakalima migomba, mbogamboga na mazao mengine na hata  kufuga, hali ambayo iliwapa mbinu ya kubadilishana bidhaa kwa fedha na kuwafanya waendelee kibiashara, ” anaeleza.

Anasema hali hiyo ilikuza kizazi cha biashara na ndilo chimbuko la Wachaga kutapakaa maeneio mbalimbali nchini kufanya biashara kwani walirithi kutoka kwa mababu zao.

Anasema hali hiyo pia ilipata nguvu kutokana na watu wa eneo hilo kuthamini elimu. Anasema  kwa sababu watu walisoma na kuelimika, waliweza kuiga yale mazuri ya wakoloni na kutambua thamani ya fedha na namna ya kuitafuta.

 “Wachaga walijua kutafuta fedha kuanzia zamani, walijua fedha ina nguvu katika kukuza maendeleo, hivyo waliweza kusomesha watoto wao, kujenga nyumba nzuri na kila siku walitafuta fursa za kupata hela.”

“Elimu na malezi vilichangia Wachaga wengi kuingia kwenye buashara,  kwani tangu zamani watoto tulikua tunafundishwa nidhamu ya matumizi ya fedha. Tulifundishwa ukipata fedha unapeleka kwenye kitu gani ili kuzalisha na kupata maendeleo na tulijifunza pia kuweka akiba na kutafuta fursa, ” anafafanua Mrema.

Mmoja wa wafanyabiashara mjini Moshi,  Boniface Mariki, anasema chimbuko la biashara mkoani hapo,  lilitokana na ujio wa Wamisionari waliokuja miaka ya 1880,  waliolitambulisha zao la kahawa na ndipo wananchi walipoanza kulima zao hilo na kuliuza na kupata fedha kutoka kwenye vyama vyao vya ushirika.

Anasema baada ya Wamisionari kulitambulisha zao hilo la kahawa, wazee wa mkoa huo  walichakarika kwenye kilimo hicho na walipata fedha nyingi baada ya kuuza.

“Wamisionari walipokuja miaka ya 1880 hadi 1893 walileta zao la kudumu la kahawa, ambapo ilikuwa ni lazima upate kibali ili uweze kulima,  hivyo Wachaga ndio wakaanza kuchakarika kwenye biashara kupitia zao la kahawa na ndipo vyama vya ushirika vilipoanza  na watu wakawa wanapeleka mazao yao kuuza na kupata fedha,”anasema.

Hata hivyo, anasema  kabla ya kuja kwa Wamisionari hao, Wachaga walikuwa na utamaduni wa kwenda gulioni kubadilishana bidhaa.

“Magulio yalianza hata kabla ya ukoloni na hayo watu walikuwa wanakwenda kwenye magulio kwa ajili ya  kubadilishana vitu. Huwezi kuwa na kila kitu kipindi kile, mtu  alikuwa ni lazima apeleka mahindi debe moja, viazi, magimbi anarudi na mboga, kwa hiyo ukawa ni utamaduni wao wa kila siku, ndio maana mpaka leo Wachaga wanapenda biashara,’’ anaeleza.

Sababu nyingine anasema,  ni kwamba mkoa huo  upo mpakani na nchi jirani ya Kenya,  hivyo ilisaidia sana kwa sababu ilifika mahali ndani hakuna bidhaa za kutosha hivyo watu walikuwa wanavuka kwenda Kenya na kuleta bidhaa kama dawa za meno, mafuta ya kupaka na kuja kuziuza hapa nchini, hii ilisaidia sana watu wa maeneo hususani Wilaya ya  Rombo ambayo ipo mpakani.

“Sababu nyingine ni uhaba wa ardhi kwa Wachaga, baada ya kuona kuna changamoto ya  ardhi waliona  suluhu ya  kutatua changamoto hiyo ni kuanzisha biashara tu maana hakukuwa na maeneo ya kutosha kulima, hivyo kununua bidhaa na kuuza ikawa ndio ardhi ya Wachaga,”anasema.

Akizungumzia chimbuko la Wachaga na baishara, mfanyabiashara, Glorious Shoo anasema biashara ni asili ya Wachaga ambayo ipo kwenye damu.

Anasema mapenzi ya biashara yalitokana na ufinyu wa ardhi uliosababisha watu wa jamii hiyo, kufikiria njia mbadala badala ya kutegemea kilimo na ufugaji.

“Katika mkoa ambao una maeneo madogo ni Kilimanjaro, ukiangalia maeneo ya vijijini watu wamesongamana sana,  kwa sababu hiyo na mazingira hayo inamlazimisha mtu kufikiria vitu mbadala,  badala ya kutegemea kilimo,’’ anasimulia Shoo.

Anaongeza: “Kwa hiyo Kilimanjaro ilianza mapema kusongamana hivyo vijana  kipindi kile  wakafikiria kutoka haraka sana na kutafuta  kitu mbadala cha kufanya badala ya kilimo na mifugo,  wakafikiria biashara,”anaeleza Shoo.

Related Posts