Wapalestina hao ni wanachama wa Hamas kutoka Gaza, wanaoshutumiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi na waliofanya mashambulizi nchini Israel dhidi ya raia na vikosi vya usalama.
Maafisa wa Israelwamesema uchunguzi umekamilika na ofisi ya mwendesha mashtaka wa kijeshi iliwasilisha Jumatatu mashtaka dhidi ya raia hao wa Palestina.
“Tuko makini na nia yetu ya kufikia makubaliano”
Wakati huohuo, waziri wa mambo ya nje wa Israel, Gideon Saar amesema kuna matumaini ya uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya kuachiwa mateka wote wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas.
Hata hivyo alisema ni mapema mno, lakini kuna matarajio makubwa. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Israel amesema hakutakuwa na usitishaji vita huko Gaza bila mpango wa kuachiliwa huru mateka.
“Sitaki kusema mambo ambayo yatadhuru mazungumzo, lakini kuna mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja, tunaweza kuwa na matumaini zaidi kuliko hapo awali lakini bado hatujafika, natumai tutakuwepo, tuko makini na nia yetu ya kufikia makubaliano. Makubaliano ya kuachiliwa huru mateka yataunganishwa na usitishaji vita huko Gaza.”, alisema Saar.
Mashambulizi mapya ya Israel
Afisa mmoja wa Palestina ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba uongozi wa Hamas uliomba makundi mengine huko Gaza kuanza kuorodhesha majina ya mateka wa Israeli na wageni wanaoshikiliwa wakiwa hai au wamekufa.
Hata hivyo Afisa huyo hakutoa maelezo zaidi ya juhudi za upatanishi lakini alisema wasuluhishi wanaoungwa mkono na Marekani wamepiga hatua katika mawasiliano na Israel na Hamas. Hamas haikutoa taarifa yoyote kuhusu mazungumzo au taarifa hiyo.
Mashambulizi ya Israel kote Gaza yaliendelea usiku kucha na hadi leo Jumatatu. Takriban watu sita waliuwaawa katika kambi ya Jabalia kwenye ukingo wa kaskazini mwa Gaza.
Huko Rafah, karibu na mpaka wa kusini wa Gaza, maafisa walisema timu za uokoaji zimefanikiwa kupata angalau miili 11 ya Wapalestina waliouawa katika mashambulizi ya anga ya Israel.