Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma amesema mashauri ya mirathi yanagusa uchumi mkubwa, akibainisha kuwa katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia Temeke pekee, katika kipindi cha miaka mitatu, kimeshughulikia mashauri ya mirathi yenye thamani ya Sh101.8 bilioni.
Hivyo, amewataka watumishi wa ngazi zote wa kuzingatia dhana ya kuanzishwa kwake, ikiwa ni kuwahudumia wananchi kwa haraka na kuwapunguzia muda ili wakafanye shughuli za kiuchumi.
Profesa Juma ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa ripoti ya miaka mitatu ya hico, leo Jumanne, Desemba 10, 2024, jijini Dar es Salaam.
Kituo hicho kilianzishwa mwaka 2021 maalumu kwa ajili ya mashauri ya ndoa, mirathi, watoto na haki zao yakiwemo matunzo, kikijumuisha ngazi ya Mwanzo ya Mahakama mpaka Mahakama Kuu ndani ya jengo moja.
Katika hotuba yake, Profesa Juma amesema kituo hicho ni moja ya vituo jumuishi sita vilivyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kutokana na kutambua kuwa utoaji haki kwa weledi, ufanisi, na uwazi ni wezeshi kwa ukuaji wa uchumi, biashara na ustawi wa wananchi.
Amesema kuwa kwa kuangalia takwimu za fedha zinazohusisha mashauri ya mirathi zinagusa uchumi mkubwa sana wa mtu mmojammoja na wa Taifa kwa ujumla.
“Katika kipindi cha miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa kituo hicho kati ya mwaka 2021/2022 na 2024/2025, jumla Sh101,876,509,671.81 (zaidi ya Sh101.8 bilioni) zilipokelewa kwenye akaunti ya mirathi.”
“Jumla ya Sh77,846,349,370.59 (asilimia 76) zililipwa kwa warithi. Jumla Sh24,030,169,397.00 zinasubiri kulipwa.”
Hata hivyo, Profesa Juma amesema ipo changamoto kubwa ya baadhi ya wasimamizi wa mirathi kukiuka masharti ya kisheria juu ya majukumu yao ya usimamizi wa mirathi, jambo ambalo limekuwa likisababisha migogoro mikubwa.
Akizungumzia uamuzi wa kutenga kituo hicho kuwa maalumu kwa masuala ya kifamilia, Profesa Juma amesema ulitokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya mashauri ya mirathi, ndoa na talaka.
“Mfano kati ya mwaka 2017-2019 kulikuwepo na mashauri 7,600 ya mirathi ambapo kati yake mashauri 3,765 yalikuwa katika ngazi ya mahakama za mwanzo. Mashauri ya ndoa na talaka yalikuwa takribani 4,200 kati ya mwaka 2017-2019,” amesema.
Amebainisha kuwa uamuzi huo ulisukumwa na asasi za kiraia na wadau wengine wa haki za binadamu kama Chama Cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla), Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) na Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (Tawja) ambazo ziliwasilisha hoja zao kwa uongozi wa Mahakama.
Hivyo, amesema kuwa Mahakama kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 pamoja na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, iliona ni muda muafaka wa kuimarisha na kuboresha ushughulikiaji na usimamizi wa mashauri ya mirathi kwa kuyapa kipaumbele.
Amesema kuwa hatua hiyo ililenga kuhakikisha wananchi na jamii kwa ujumla wanapata huduma na elimu ya usimamizi wa mirathi na utatuzi wa migogoro ya kifamilia, ili kutumia muda wao zaidi katika shughuli za kiuchumi na kimaendeleo.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa kituo hicho, Mwanabaraka Mnyukwa amesema tangu kuanzishwa kwake, kituo kimefanikiwa kuhudumia idadi kubwa ya wananchi ambao wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku.
“Kitakwimu, mwaka wa kwanza wa kutoa huduma, 2021/2022, kituo kilipokea wastani wa wateja 700 kwa siku, 2022/2023 kilikuwa kinapokea wastani wa wateja 971 na 2023/2024 kimekuwa kinapokea wastani wa wateja 890 kwa siku,” amesema Jaji Mnyukwa.
Amefafanua kuwa kitakwimu tangu kuanzishwa kwa kituo hadi kufikia Agosti 26, 2024 kimehudumia wateja wapatao 580,610; kati ya hao wanaume wakiwa 265,985 sawa na asilimia 45 na watoto 3,442 sawa na asilimia 0.6
Kwa upande wa mashauri, kwa kipindi cha mitatu kuanzia Agosti 27, 2021 mpaka Agosti 26, 2024 kituo kimesajili jumla ya mashauri 22,929, kati ya hayo kimefanikiwa kuamua jumla 20,077 sawa na asilimia 88 ya yote yaliyofunguliwa.
Hivyo, amesema mpaka kufikia Agosti 26, 2024 mashauri ambayo hayakusikilizwa ni 2,852 ambayo ni sawa na asilimia 12, na wanajivunia takwimu hizo kwa kuwa zinaonyesha ishara kwamba wanaridhika na huduma zinazotolewa kituoni hapo.
Jaji Mnyukwa amesema kwa kipindi cha miaka mitatu ya kituo katika kushughulikia mashauri ya familia, uzoefu unaonyesha usuluhishi unahitajika sana ili kupunguza migogoro ya familia na kuongeza kasi ya umalizaji wa mashauri ya familia.
Amesema wapo wadaawa ambao kwa hiari yao wanaomba kusaidiwa kufanya usuluhishi mbele ya Jaji au Hakimu ili kumaliza shauri kwa maridhiano na kupunguza uadui, chuki na kuleta upendo baina yao.
Hata hivyo, amesema japo usuluhishi umekuwa ukiombwa na wadaawa, sheria zinazoongoza usikilizwaji wa mashauri ya mirathi haijaweka bayana kwa wadaawa kupitia usuluhishi kama yalivyo mashauri mengine ya madai.
Amesema migogoro ya mirathi husababisha chuki miongoni mwa wanafamilia na kuchelewesha umalizikaji wa baadhi ya mashauri, hivyo kusababisha warithi kushindwa kupata haki zao kwa wakati.
“Ni rai yetu kwamba, iwapo usuluhishi utaruhusiwa katika kushughulikia mashauri haya, itachagiza wananchi kupata haki zao kwa wakati na bila ya kuacha kovu la chuki kwa wanafamilia.”
Amesema kwa kutambua umuhimu wa usuluhishi katika kushughulikia mashauri ya mirathi, kituo hicho kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kimetoa mafunzo kwa mabaraza ya usuluhishi ya ndoa na viongozi wa dini juu ya mbinu bora za usuluhishi.
Akizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo amesema kuwa ni pamoja na kuchelewa kuhamisha mali za marehemu kwenda kwa warithi, jamii kutokuwa na uelewa wa kutosha wa masuala ya mirathi, umuhimu wa wosia na makubaliano ya wadaawa katika masuala ya ndoa.
Akizungumzia maudhui ya ripoti ya miaka mitatu ya kituo hicho, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Simon Swai amesema kuwa pamoja na mambo mengine inaonyesha mashauri yanayoongoza, ambayo ni ya mirathi, yakifuatiwa na ya ndoa.
Pia amesema kuwa ripoti hiyo inaonyesha idadi ya ndoa zilizovunjika na sababu zinazoongoza kuvunjika kwa ndoa.