MAAFANDE wa JKT Tanzania wataikaribisha Pamba Jiji leo kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, huku wakijivunia rekodi waliyonayo ya ushindi kwa asilimia kubwa wakiwa nyumbani.
JKT Tanzania ndiyo timu pekee msimu huu ambayo haijapoteza mchezo wowote wa ushindani ikiwa nyumbani, imeshinda nne moja ikiwa ya Kombe la FA na sare mbili katika michezo sita waliyocheza msimu huu na hii itakuwa mara ya kwanza kwa timu hizi kukutana.
Akiongelea maandalizi ya kikosi chake kocha wa JKT Tanzania, Ahmady Ally ambaye kikosi chake kipo nafasi ya nane na pointi 16, alisema wapo tayari kwa mchezo huo.
“Tumekuwa na maandalizi bora kwa mchezo huu na tunataka kuendelea kusogea nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi. Wachezaji wangu wapo katika hali nzuri na wameshaonyesha nia ya kushinda,” alisema kocha Ally.
Wakati JKT Tanzania ikiwa na rekodi nzuri nyumbani, Pamba Jiji itakuwa na wakati mgumu kutokana na kupoteza kwao michezo minne kati ya mitano ya mwisho wakiwa ugenini. Wamefungwa jumla ya mabao tisa huku wakifunga matatu katika mchezo wao wa mwisho wa ligi dhidi ya Fountain Gate (3-1) kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa.
Pamoja na hali waliyonayo, Pamba ambao wapo nafasi ya 13 wakiwa na pointi 11, kocha wa kikosi hicho, Fred Felix Minziro alieleza ingawa wanakutana na changamoto, bado wana matumaini ya kufanya vizuri.
“Tunajua itakuwa kazi ngumu kucheza ugenini, lakini hatutaki kurudi mikono mitupu. Tumefanya maandalizi ya kutosha na tutapigania kila pointi,” alisema Minziro.
Katika michezo waliyocheza JKT Tanzania yenye mastaa kama vile Said Ndemla, Hassan Dilunga na John Bocco wamefunga mabao tisa na kuruhusu manane, Pamba yenye George Mpole, imefunga mabao saba na kufungwa 14.
Nani kumshusha mwenzake? ndiyo kitu kinachosubiriwa katika mchezo huu mwingine wa Ligi Kuu Bara ambao Kagera Sugar ikiwa nyumbani itaikaribisha Namungo, wote wapo katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa ligi.
Mwenyeji Kagera Sugar ambaye yupo nafasi ya 14 akiwa na pointi 10, ataingia na ahueni kwenye mchezo huo kutokana na kukusanya kwao pointi tano katika michezo minne iliyopita tofauti na wapinzani wao.
Namungo inayonolewa na Juma Mgunda ikiwa nafasi ya 15 na pointi tisa, imetoka kufungwa katika michezo mitatu mfululizo, imekusanya pointi tatu katika michezo mitano iliyopita. Kagera imetoa sare katika michezo miwili iliyopita.