Musoma. Kesi inayomkabili aliyekuwa Padri wa Kanisa Katoliki jimbo la Bunda mkoani Mara, Carol Mwibule na Mhasibu wa Parokia ya Bunda, Gerold Mgendigendi imeahirishwa hadi Desemba 23 mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani hapo.
Padri huyo ambaye pia alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Bunda na mwenzake wanakabiliwa na mashitaka 178 ikiwemo ya uhujumu uchumi.
Akiahirisha kesi hiyo yenye namba 22036/2024, leo Desemba 10, 2024 Hakimu Mkazi Mkuu, Eugenia Rujwahuka ameutaka upande wa mashitaka kumaliza haraka upelelezi wa shauri hilo ili hatua nyingine ziweze kuendelea, baada ya shauri hilo kushindwa kuendelea kutokana upelelezi kutokukamilika.
“Kesi imevuka muda wa upelelezi kama inashindikana basi futeni kesi kisha mkimaliza mtarudi tena,” amesema.
Awali Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Jonas Kivuyo aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo iliyokwenda mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa bado haujakamilika.
“Mheshimiwa tunaiomba mahakama yako iweze kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kesi kuja kutajwa kwa sababu upelelezi bado haujakamilia.”
Akizungumza na Mwananchi Digital Wakili wa Utetezi, Method Kagoma ameiomba mahakama hiyo kufuta kesi hiyo kutokana na upelelezi kuchukua muda mrefu bila kukamilika.
“Wateja wangu wamekaa ndani tangu Agosti hadi sasa kila tukija mahakamani tunaambiwa upelelezi bado, kama wanajua hawakuwa tayari walileta kesi mahakamani ili iweje, ni vema kesi ikafutwa kama alivyosema mheshimiwa na siku wakiwa tayari watakuja mahakamani,” amesema Kagoma
Ameongeza wateja wake wamekuwa wakifika mahakamani hapo mara kadhaa kwa ajili ya kesi yao kutajwa huku ikishindikana kuendelea katika hatua nyingine kwa madai ya upelelezi kutokamilika.
Padri Mwibule na Mgendigendi wanashtakiwa kwa wizi wa zaidi ya Sh1.7 bilioni, zaidi ya Dola 100,000 na yuro (Euro) zaidi ya 20,000. Wawili hao wanashtakiwa kwa jumla ya makosa 178 likiwamo la kuongoza genge la uhalifu kinyume na sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200 marejeo ya mwaka 2022, makosa mengine ni utakatishaji wa fedha kinyume na sheria ya adhabu sura ya 16.
Watumishi hao wa kanisa pia wanadaiwa kughushi nyaraka kinyume na sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.