Katika miaka ya hivi karibuni, uendeshaji wa shule binafsi nchii umeibua mjadala kuhusu utaratibu wa kuweka wastani wa juu wa ufaulu kama sharti la kuwapokea wanafunzi wapya au kuwaendeleza wale waliopo.
Wamiliki wa shule binafsi wanatetea hatua hii kwa kudai kuwa inalenga kuongeza ubora wa elimu, lakini kwa upande mwingine utaratibu huo umeibua maswali kuhusu usawa, haki, na athari za kisaikolojia kwa wanafunzi achilia mbali zile za kiuchumi kwa wazazi.
Kwa wadau wa elimu, mfumo huu pia umeonekana kuwa mzigo mkubwa kwa wazazi, huku ukihatarisha dhamira ya elimu jumuishi ambayo Serikali imekuwa ikihamasisha.
Hata hivyo, mfumo huu umekuwa ukilalamikiwa kwa kuwa unawabagua wanafunzi wenye uwezo wa wastani au wa chini. Na mara nyingi unaleta athari kubwa kwa familia nyingi.
Grace Simon, mzazi wa mkoani Shinyanga, amewahi kuonja machungu ya wastani, hali iliyomlazimu mwanawe kufukuzwa licha ya kuwa alikuwa na uwezo.
“Mtoto wangu alifukuzwa shule kwa sababu ya ufaulu mdogo. Lakini nilipompeleka shule nyingine, alifanya vizuri sana. Hii inaonyesha kwamba tatizo halikuwa mtoto, bali mfumo wa shule uliomtenga.”
Joseph Mushi, mzazi kutoka Kilimanjaro, anasema: “Mtoto wangu alifukuzwa kidato cha pili kwa sababu hakufikisha wastani wa shule. Tulilazimika kumhamishia shule nyingine, jambo ambalo liliharibu bajeti ya familia.”
Edin Mjuzi, mzazi anayeishi Dar es Salaam, anasema aliwahi kwenda shule moja jijini hapo na kukutana na kilio cha wazazi ambao watoto walizuiwa kuendelea na darasa jingine kwa sababu ya kutofika wastani.
‘’Unajua unauma nilienda shule anayosoma mwanangu, wazazi wawili wakawa wanalalamika watoto wao kukosa wastani. Kinachowauma zaidi ni kuwa wanalazimika kutumia muda mchache wa likizo ya Desemba kutafuta upya shule kwa ajili ya watoto wao. Huu ni usumbufu,’’ anasema.
Wamiliki wa shule binafsi wanaamini kuwa, kuweka viwango vya juu vya ufaulu, ni hatua inayosaidia kudhibiti ubora wa elimu inayotolewa.
Kwa mfano, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco), Benjamin Nkoya, aliwahi kusema kuwa viwango vya juu vya ufaulu, vinahakikisha kuwa shule binafsi zinatoa elimu yenye ushindani kitaifa na kimataifa.
“Malengo yetu ni kutoa elimu bora, na ushirikiano wa wazazi katika kuweka viwango vya ufaulu, unalenga kuimarisha mustakabali wa elimu,”alisema.
Shule binafsi nyingi zimekuwa zikisisitiza kuwa mitihani yao ya mchujo ni ya kawaida, na kwamba inahakikisha wanafunzi wenye uwezo tu ndio wanakubaliwa.
Aliyekuwa mwalimu mkuu wa shule moja maarufu jijini Arusha anasema: “Tukiwaweka wanafunzi wasio na uwezo, tunakuwa na changamoto kubwa katika kuhakikisha wanatimiza viwango vya ufaulu vinavyotarajiwa na shule.”
Pamoja na utetezi huu, wataalamu wa saikolojia wanahoji mantiki ya kutumia wastani wa juu, kama kigezo cha kuchagua au kuwaendeleza wanafunzi.
Katika baadhi ya shule, wanafunzi wasiofikia wastani wa ufaulu hufukuzwa shule, jambo ambalo limeonekana kuwa mzigo kwa wazazi.
Shule nyingi binafsi zimeanza kutenga madarasa kwa misingi ya uwezo wa kitaaluma wa wanafunzi.
Wanafunzi wenye uwezo wa juu huwekwa katika madarasa maalum yenye walimu bora zaidi na rasilimali nyingi, wakati wale wa uwezo wa chini huwekwa katika madarasa yenye rasilimali za kawaida.
Hili linaibua maswali kuhusu haki na usawa. Mzazi wa mkoani Kilimanjaro, Joseph Mushi, anaeleza: “Hii ni njia ya kuwagawa watoto. Badala ya kuwasaidia wale wenye changamoto, wanawafanya wajione kama ni daraja la pili. Mtoto wangu alianza kupoteza ari ya kusoma baada ya kugawanywa katika darasa la wastani wa chini.”
Wataalamu wa elimu duniani kama vile Profesa John Hattie kutoka Chuo Kikuu cha Melbourne na Profesa Linda Darling-Hammond kutoka Chuo Kikuu cha Stanford, wanasisitiza kuwa viwango vya juu vya ufaulu vinavyowekwa na shule binafsi vinaweza kuwa na madhara makubwa kwa wanafunzi, hasa wale wenye changamoto za kielimu.
Wabobezi hawa wanasema kuwa viwango hivyo, ingawa vinatoa changamoto kwa wanafunzi, pia vinawafanya washindwe kufikia malengo yao kutokana na kutokuwa na msaada wa kutosha
Profesa Nsibagana Nkurunziza kutoka nchini Burundi, anasema kuwa elimu inapaswa kuwa jukwaa la kuwasaidia watoto kufikia uwezo wao kamili, na siyo kuwa sehemu ya kuwabagua na kuwaachilia nje ya mfumo wa elimu.
Anaendelea kusema kuwa mfumo wa elimu unapaswa kuwa na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kisaikolojia ili watoto wote waweze kufikia malengo yao.
Wataalamu wa elimu wanaeleza kuwa kumfukuza mtoto shule kunaweza kusababisha athari kubwa za kisaikolojia.
Daktari wa saikolojia ya watoto, Stephen Mwakalinga, anasema: “Kufukuzwa shule kunaweza kuathiri vibaya hali ya kujiamini kwa mtoto. Wanaweza kujiona kama wamefeli maisha na kupoteza mwelekeo.”
Daktari wa saikolojia, Mariam Shauri, anasema kuwa mtoto anayehisi ameshindwa kufikia viwango vinavyotarajiwa na shule anaweza kupoteza hali ya kujiamini na kuhisi hana thamani.
‘’Hali hii inaweza kuathiri vibaya maendeleo yake ya kitaaluma na kijamii,”anaongeza.
Michael Newman, mtaalamu wa elimu kutoka Uingereza, anasema kuwa mfumo wa tathmini endelevu, unatoa nafasi kwa mwanafunzi kujifunza kutokana na makosa na kuboresha uwezo wake.
‘’Mtihani mmoja wa mwisho wa mwaka huathiri watoto wengi hasa wale wasio na uwezo mzuri wa kufanya mitihani, na ndio maana nchini kwetu tumekwishaachana na masula ya mitihani kwa wanafunzi, hasa wa shule za msingi na sekondari,”anaeleza.
Mfumo wa elimu wa Rwanda na Kenya unaweza kutupa mwanga kuhusu changamoto hizi. Rwanda, kwa mfano, imewekeza katika kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anapata nafasi ya kusoma, bila kujali uwezo wake wa kitaaluma.
Serikali ya Rwanda imeweka mkazo katika mifumo ya tathmini endelevu inayolenga kufuatilia maendeleo ya wanafunzi kwa muda mrefu badala ya kutegemea mitihani ya mwisho pekee.
Hii imepunguza mzigo wa kisaikolojia kwa wanafunzi na kuwapa nafasi ya kujifunza kutokana na makosa yao.
Kenya nayo imepiga hatua katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapata elimu sawa. Ingawa shule binafsi nchini Kenya bado zina viwango vyao vya ufaulu, serikali imeweka mikakati ya kudhibiti ubaguzi kupitia sera madhubuti za elimu.
“Mfumo wa tathmini ya kitaifa umeimarishwa ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapimwa kwa viwango sawa, bila kujali aina ya shule wanayosoma,”anasema Kamau Njuru mkazi wa Manispaa ya Shinyanga ambaye ana asili ya Kenya.
Serikali na kigezo cha wastani
Kwa upande wa Tanzania, Serikali imekuwa ikipinga vikali hatua za shule binafsi kufukuza wanafunzi kwa sababu ya kutofikia wastani wa ufaulu.
Mawaziri wenye dhamana ya elimu kwa nyakati tofauti wamekuwa wakipinga suala hili kwa kutoa waraka tofauti.
Aliyekuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, aliliambia Bunge Januari 2014 kuwa shule binafsi zitakazotumia viwango vya juu vya ufaulu visivyokubalika zitaadhibiwa kwa mujibu wa Sheria ya Elimu ya mwaka 2011 (Kifungu cha 6). Dk Kawambwa alitoa kauli hiyo wakati akijibu maswali ya wabunge, waliolalamikia kuwa baadhi ya shule binafsi, zinalazimisha wanafunzi kurudia darasa au kuhamia shule nyingine ikiwa hawafikii wastani wa ufaulu wa shule hizo.
Januari 2018, aliyekuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alifanya kikao na baadhi ya viongozi wa shule binafsi za sekondari kujadili utekelezaji wa Waraka Namba 7.
Waraka huo unakataza shule kuwafukuza wanafunzi kwa sababu ya kushindwa kufikia wastani wa ufaulu uliowekwa na shule.
Profesa Ndalichako alieleza kuwa msingi wa waraka huo ni kutokana na tabia ya baadhi ya shule kufukuza idadi kubwa ya wanafunzi hasa mwaka wao wa mwisho wa masomo kwa kigezo cha ufaulu mdogo.
Alisema: “Hili ni jambo la kibaguzi na la unyanyasaji. Ni wajibu wa shule kuwasaidia wanafunzi wanaokabiliwa na changamoto badala ya kuwafukuza.”
Pia alionesha masikitiko kwamba wakati Serikali na jamii zinapambana kupunguza changamoto za wasichana kuacha shule kwa sababu ya ujauzito, baadhi ya shule ziliripotiwa kufukuza wanafunzi wa kike kwa sababu ya ufaulu mdogo.
Profesa Ndalichako alisisitiza kuwa wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa waraka huo kwa nguvu zote.
Alitoa wito kwa wamiliki wa shule binafsi kuunda utaratibu wa kuwasaidia wanafunzi wenye uwezo mdogo badala ya kuwafukuza, hatua ambayo inawaacha watoto hawa wakihangaika bila kujua pa kwenda.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa shule binafsi walionesha wasiwasi kuwa utekelezaji wa waraka huo, unaweza kushusha ubora wa ufaulu wa shule zao. Walidai kuwa kuwaacha wanafunzi wenye uwezo mdogo, kunaweza kuathiri rekodi ya shule na matarajio ya wazazi wanaotaka matokeo bora.