Dar es Salaam. Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian amesema urafiki wa muda mrefu uliopo kati ya China na Tanzania, umekuwa fursa ya lugha ya Kiswahili kupendwa na kuzidi kukua nchini mwake.
Hatua hiyo alisema imesababisha vyuo sita nchini humo kuanzisha vitivyo maalumu vya kufundisha Kiswahili.
Balozi Mingjian aliyasema hayo hivi karibuni kwenye hafla ya mashindano ya kimataifa ya walimu wa lugha ya Kichina nchini Tanzania yaliyofanyika katika Taasisi ya Kichina (CI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Alisema mpaka sasa tayari vyuo sita vimeanzisha vitivo vya kufundisha lugha hiyo na ana imani kadri siku zinavyokwenda, vyuo vingi vitafanya hivyo.
“Hii ya vyuo kuanzisha vitivo vya Kiswahili sio tu kumechangiwa na urafiki tulionao na Tanzania, bali na lugha hiyo kukubalika duniani kwa sasa, huku mwitikio wa wanafunzi kupenda kujifunza ukiwa mkubwa,”alisema balozi huyo.
Kuhusu umuhimu wa shindano hilo, alisema litasaidia walimu kupata mbinu za kufundishia, kuboresha ustadi wa kufundisha lugha ya Kichina.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga , ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, aliwataka Watanzania nao kuchangamkia kujifunza lugha ya Kichina kwa kuwa ina mchango katika kuwezesha diplomasia ya uchumi.
Alisema kujifunza Kichina kutafungua milango ya fursa pamoja na mawasiliano rahisi na Wachina katika nyanja mbalimbali, ikizingatiwa kuwa kwa sasa ni taifa la pili kwa uchumi mkubwa duniani.
“Kwa kujihusisha na mawasiliano kama haya, unafungua milango ya maendeleo yako ya elimu, taaluma ya biashara na kukuza utalii wa lugha. Hivyo kutokana na diplomasia ya lugha unajenga pia diplomasia ya kiuchumi,” alisema Kipanga.
Awali Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye, alisema taasisi hiyo inalenga kukidhi haja ya Tanzania ya kuelewa utamaduni, teknolojia na ujuzi wa lugha ya Kichina na kuongeza maelewano kati ya watu wa China na Tanzania.
Alisema ushirikiano huo umesaidia kuwaunganisha wanafunzi wa vyuo vikuu na kampuni za China nchini Tanzania, ili kupendekeza nafasi zao za kazi kwa wahitimu.
“Juhudi hizi zimewawezesha wanafunzi wetu na kitivo, kupanua mtandao wetu wa kimataifa na kuimarisha sifa yetu ndani na nje ya Tanzania,” alisema Profesa Anangisye.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa CI, Profesa Zhang Xiaozhen, alisema mashndano hayo ni mara yake ya kwanza kufanyika nchini Tanzania huku walimu 54 wakishiriki kutoka nchi 11.
Aliyeibuka mshindi katika mashindano hayo ni Andersen Sylviano kutoka nchini Madagascar, aliyesema yamempa hamasa ya kwenda kuwasahawishi walimu wengine kujifunza lugha hiyo.