Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemruhusu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33), anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka mawili, kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Gasaya anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka katika Saccos ya Jatu kwa madai kuwa fedha hizo atazipanda kwenye kilimo cha mazao ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua ni uongo.
Mshtakiwa huyo atahojiwa na maofisa wa Takukuru kwa sababu kuna taarifa wanataka kutoka kwake na baada ya mahojiano, atarudishwa mahakamani hapo.
Uamuzi huo umetolewa leo, Jumanne Desemba 10, 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini, baada ya upande wa mashitaka kuwasilisha ombi mahakamani hapo la kutaka mshtakiwa huyo kuhojiwa na maofisa wa Takukuru.
Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele ameiambia Mahakama kuwa kesi hiyo bado ipo kwenye hatua ya upelelezi na ilipangwa kutajwa mahakamani hapo Desemba 16, 2024 lakini upande wa mashitaka waliomba mshtakiwa aletwe mahakamani hapo leo.
“Tuliomba mshtakiwa aletwe leo kwa sababu mamlaka husika ambao ni Takukuru, waliomba kufanya naye mahojiano kwa kuwa kuna taarifa wanataka kutoka kwake, hivyo tunaomba amri ya Mahakama ili tumkabidhi kwa maofisa wa Takukuru,” amesema Wakili Mwakamele.
Mwakamele baada ya kutoa maelezo hayo, Hakimu Mhini alikubaliana na upande wa mashitaka na kuruhusu mshtakiwa huyo kwenda kufanyiwa mahojiano na maofisa wa Takukuru.
“Haya ni maombi ya kawaida na Mahakama imekubali mshtakiwa kwenda kuhojiwa na atatakiwa kurudishwa mahakamani hapa baada ya kumaliza kuhojiwa muda wa kazi akiwa salama na afya njema,” amesema Hakimu Mhini.
Hakimu Mhini baada ya kueleza hayo aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 16, 2024 itakapotajwa.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni kujipatia Sh5.1 bilioni na kuzitakatisha katika kesi ya uhujumu uchumi namba 8/2023.
Katika shitaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa, kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5,139,865,733 kutoka Saccos ya Jatu kwa njia ya udanganyifu.
Shitaka la pili ni kutakatisha kiasi hicho cha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 jijini Dar es salaam.
Siku hiyo ya tukio na eneo hilo, mshtakiwa akiwa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa Jatu Saccos, alijihusisha na muamala wa Sh5,139,865,733 kutoka katika akaunti ya Jatu saccos iliyopo benki ya NMB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya Jatu PLC Iliyopo katika benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kuzipata kwa njia ya udanganyifu.