Tabora. Mkazi wa mkoani hapa, Zainab Abas amefariki dunia baada ya kudaiwa kuchomwa kisu na mkwe wake, Shaban Juma.
Tukio hilo limetokea katika Mtaa wa Mlenda kata ya Ipuli Manispaa ya Tabora wakati akijaribu kusuluhisha mgogoro wa kifamilia baina ya mtoto wake na mkwewe.
Tukio hilo lilitokea Desemba 5, 2024, wakati Aisha Ramadhan ‘Batuli’ mkewe na Juma alipokuwa akijiandaa kusafiri kuelekea mkoani Kigoma akidaiwa kukimbia ugomvi wake na mumewe huyo.
Inaelezwa kuwa katika harakati hizo, ndipo Juma alipowavamia na kuanza kumchoma visu mama mkwe wake, kisha kumjeruhi Batuli na akatokomea kusikojulikana.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Desemba 10, 2024 kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amekiri kuwa Zainab ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kifuani na upande wa titi la kulia, huku akidai kuwa aliyetekeleza mauaji hayo ni Shaban Juma mume wa Aisha Ramadhan, maarufu ‘Batuli’.
Abwao amesema chanzo cha kifo hicho ni wivu wa mapenzi, mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu mama mkwe wake kwamba anaivuruga ndoa yake.
Kamanda huyo amesema kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, mgogoro huo ulianza mwaka mmoja uliopita. “Jeshi la linaendelea na juhudi za kumtafuta mtuhumiwa anayedaiwa kufanya mauaji hayo na akikamatwa atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili kujibu tuhuma zinazomkabili.”
Aisha aeleza tukio lilivyokuwa
Mwananchi limezungumza na Aisha akiwa amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora ‘Kitete’ ambapo amesema anaendelea vizuri.
Aisha ameelezea tukio lilivyokuwa. “Shaban Juma kwa sasa siyo mume wangu nilishampa talaka na hiyo ilitokana na kupigwa kila siku maana ilifikia hatua nafanya kazi, nahemea mahitaji yote nyumbani wakati yeye yupo kama baba wa familia, baada ya kuchoka nilimfuata sheikh aliyetufungisha ndoa kumwambia sitaki kuendelea na mume wangu, akaelekeza nimrejeshee mahari yake nikachukua Sh80,000 nikaandika talaka tukamalizana”
Batuli anadai kuwa baada ya kupeana talaka na Shaban alichukua vitu vichache ndani ya nyumba hiyo, vingine mwenzake huyo akavikatalia, baada ya muda alipigiwa simu ya kutakiwa kwenda kuchukua vitu vyake na alipofika ndani kwa aliyekuwa mumewe akapigwa, akachukua kisu akitaka kumchoma, akambembeleza akamuacha.
“Nilivyonusurika kuuawa kwa kuchomwa na kisu baada ya kutoka kwake nikaenda kuripoti Kituo cha Polisi Ipuli kuhusu yaliyotokea maana kama aliweza kunishikia kisu angeweza kunidhuru, nilipofika kituoni nikatoa maelezo, likafunguliwa jalada la kesi Juma akaitwa akawekwa mahabusu, mimi nikaruhusiwa kurudi nyumbani lakini baada ya muda akaachiwa baada kwa dhamana” anadai.
Batuli anadai kuwa baada ya kufungua jalada hilo, baadaye alitakiwa kwenda polisi ili kesi iende mahakamani, lakini cha kustaajabisha jalada hilo lilifichwa ambapo alipigwa danadana na halikupatikana, ndipo akaamua kuhama mkoa ili asije akauliwa na aliyekuwa mume wake.
Tukio la Mama yake kuuawa lilivyokuwa
Batuli anadai siku ambayo mama yake aliyochomwa kisu alikuwa akijiandaa kusafiri kuelekea mkoani Kigoma, alipotoka nje ya nyumba kwa ajili ya kupanda bodaboda ili kuwahi kituo cha mabasi Tabora hakupata, ikamlazimu atembee kwa mguu kutafuta bodaboda.
“Kabla hatujapanda kwenye ile bodaboda nikamuona aliyekuwa mume wangu amesimama mbele yetu maana tulikua jirani na kijiwe anachofanyia kazi kwani yeye pia ni bodaboda. Mama alivyomuona Shaban akaamua kunisindikiza kwenda stendi kuu ya mabasi Tabora maana akasema akiniacha sitafika sababu ya ukorofi wake.”
Batuli anaendelea kudai kuwa baada ya kupanda bodaboda kwa ajili ya kuelekea kituo cha mabasi Tabora, ghafla Shaban akaja mbio anaisimamisha ile bodaboda iliyombeba yeye na mama yake, waliposimama akahoji wanaelekea wapi?
“Mama akamjibu Shaban, wewe unaniuliza kama nani? Wakati mama anauliza maswali hayo niliona anafungua koti akatoa leso yenye kisu, kwenye boda nilikaa katikati akataka kunichoma kisu tumboni nikakinga mkoba kisu hakikuzama tumboni kwangu, ile mama kunitetea nisichomwe ndipo akamfuata akamchoma kisu shingoni mara mbili, na kisha akachoma kwenye titi mama akaanguka” anadai Batuli
Batuli anadai kuwa baada ya mama yake kuanguka Shaban akamrudia akamchoma kisu cha shingo akiamini amewaua wote kisha akawasha pikipiki yake akakimbia kusikojulikana.
“Nilikuwa alfajiri nilijikongoja kutembea kuomba msaada ndipo tukapelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete kwa ajili ya matibabu ambapo muda wote sikuwa nikijua kama mama amepoteza maisha,”anadai Batulia.
Akizungumzia tukio hilo na matukio ya mauaji kwa ujumla, Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Magharibi kati Tabora, Isaac Laizer anasema iko haja kwa mauaji kuombewa ili kuwafanya wananchi kuishi kwa amani kwenye maeneo yao.
“Ndugu zangu mauaji kwa sasa limekuwa jambo la kawaida na hili pepo tunahitaji kulikemea kwa nguvu zote, kwenye mkoa wetu wa Tabora watu wanauana bila kuogopa, hivyo sisi viongozi wa dini tunao wajibu wa kuliombea Taifa ili mauaji kama haya yakome kwenye maeneo yetu” anasema