MATUMIZI YA SIMU KAZINI YATAJWA KUATHIRI UFANISI WA WAFANYAKAZI

 Matumizi yasiyo sahihi ya simu mahali pa kazi yameelezwa kuwa changamoto kubwa inayoathiri ufanisi wa wafanyakazi. 

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Taifa, Joel Kaminyonge, amesema matumizi haya yanapunguza uwajibikaji na kuzorotesha utendaji wa taasisi.

Akizungumza leo, Desemba 10, 2024, wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Idara ya Uhamiaji katika Ukumbi wa Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji (TRITA) Moshi, Kaminyonge amesema:

“Tunazungumza haki na wajibu. Mfanyakazi lazima awajibike ili kuongeza tija. Kulipwa vizuri hutokana na kufanya kazi kwa bidii, si kutumia muda mwingi kuchati kwenye simu.”

Ametoa wito kwa mabaraza ya wafanyakazi kushirikiana katika kupanga na kutekeleza mikakati ya kuimarisha uzalishaji.

“Tukijadiliana na kushirikiana, tunaweza kuondoa migogoro na kuongeza ufanisi. Hii itaboresha maslahi ya wafanyakazi wote,” alisema Kaminyonge.

Wakati huohuo Kaimu Mwenyekiti wa Tughe Idara ya Uhamiaji, Kamishna Gerald Kihinga, amesisitiza umuhimu wa mabaraza ya wafanyakazi katika kutatua changamoto za watumishi.

“Wafanyakazi wakiwa na malalamiko, ufanisi unashuka. Lakini tukihakikisha maslahi yao yanatatuliwa kwa wakati, tunajenga mazingira bora ya kazi,” amesema Kihinga.

Kamishna huyo amebainisha kuwa Idara ya Uhamiaji imeimarisha mahusiano ya kikazi na kuhakikisha maslahi ya wafanyakazi, hususan wanawake, yanashughulikiwa ipasavyo.

“Hivi sasa, changamoto za watumishi, hasa wanawake, zimepungua kwa kiasi kikubwa na mazingira ya kazi yameboreshwa,” amesema.

Mfanyakazi wa shirika lisilo la kiserikali mjini Moshi, Consolata Lyimo, amesema matumizi mabaya ya simu yanachelewesha huduma kwa wateja.

“Wafanyakazi wengi wameathirika kwa matumizi ya simu kiasi cha kushindwa kutoa huduma bora au kuwa makini kutokana na mambo mengi ya mitandaoni,” amesema.

Kauli za viongozi hawa zinaonyesha umuhimu wa kudhibiti matumizi ya simu mahali pa kazi ili kuongeza ufanisi, kujenga mahusiano mazuri ya kikazi, na kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

Chama hicho kinaadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1994, kikijivunia mafanikio mbalimbali katika kulinda na kuboresha maslahi ya wafanyakazi nchini.

Tangu kuanzishwa kwake,Tughe imekuwa mstari wa mbele kushughulikia changamoto za kikazi, kuimarisha uwajibikaji, na kuhimiza majadiliano ya pamoja kati ya waajiri na waajiriwa, hatua ambazo zimechangia kuboresha mazingira ya kazi na ustawi wa wanachama wake. 

Maadhimisho haya ni ishara ya uthabiti wa chama hicho katika kutetea haki na wajibu wa wafanyakazi kwa miongo mitatu.

Related Posts