Mbowe avunja ukimya kuhusu uenyekiti wake

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amevunja ukimya kuhusu nafasi yake hiyo, akisema wanachama na viongozi wa chama hicho ndiyo watakaoamua agombee au asigombee tena. Akibainisha kuwa muda ndiyo utakaoamua.

Mbowe ameeleza hayo leo Jumanne Desemba 10, 2024 wakati akisoma maazimio 10 ya Kamati Kuu ya chama hicho kuhusu mwenendo wa chaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Novemba 27, 2024.

Kauli hiyo ya Mbowe imekuja siku chache baada ya kuwepo kwa vuguvugu linalomuhusisha Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Tanzania Bara), Tundu Lissu anayetajwa kutaka kutangaza nia ya kuwania uenyekiti wa Chadema.

Hatua hiyo ya Lissu inadaiwa kuwagawanya wanachama wa chama hicho ambapo kuna wanaomuunga mkono yeye na wanaomuunga Mbowe.

Mbowe amebainisha hayo baada ya kuulizwa swali kwamba haoni sababu ya kumpumzika baada ya kuhudumu kwa miaka 20 kwenye nafasi ya  uenyekiti wa chama hicho?.

“Chama hiki hakijawahi kumnyima mtu yeyote nafasi ya kuwania nafasi anayotaka kugombea, na anayesema Mbowe nagombea mwenyewe ananionea, sijawahi kugombea mwenyewe wala kumzuia mtu.”

“Jambo la pili, chama hiki hakijawahi kutoa fomu moja ya uchaguzi ya uenyekiti kama chama cha siasa…yeyote anayejisikia kugombea agombee, hayo mambo mengine ni kukubaliana,” amesema Mbowe.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akifurahia jambo na Tundu Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Desemba 10, 2024. Picha na Michael Matemanga

Kuhusu Lissu kupigwa vita mitandoni, Mbowe amesema inawezekana Lissu anapigwa vita mitandaoni lakini sio peke yake, hata yeye na viongozi wengine wakuu wakiwemo wa sekretarieti ya chama hicho wanasemwa.

“Wengi wanaotupiga vita sio wanaChadema, nyie mnategemea CCM wafanye kazi watupatanishe mimi na Tundu Lissu?” amehoji.

Akizungumzia kutangaza kuwania tena uenyekiti: “Mimi sijasema kama nagombea, si msubiri muda useme? Shida iko wapi, ingekuwa kutosema kwangu nimemzuia mtu asisemee hilo ni jambo jingine. Vitu vingine vinapikwa ndani subirini viive.”

“Oooh wengine wanasema Mbowe umekaa sana, miaka 20, hii miaka 20 ni ya kukomaa, mwingine analinganisha kwamba Nyerere (Julius) aling’atuka, Nyerere alikuwa mtumishi wa umma, analipwa mshahara, hafungwi wala kushtakiwa, sisi unaona hapa wote tunajitolea,” amesema.

Kuhusu hoja ya kuondoka madarakani, Mbowe amesema wenye uamuzi huo wa yeye kuondoka au la, ni wanachama na viongozi wa chama hicho.

“Watakaoniambia Mbowe gombea ni wanachama hawa na viongozi wenzangu, tutaelewana ni mambo yetu ya ndani, nyie yanawahusu nini? Pilipili usizokula zinakuwashia nini? Tuacheni na Chadema yetu, tutaipanga kwa kadri tunavyopenda,” amesema Mbowe.

Mbowe amesisitiza kuwa Katiba ya Chadema haijamzuia mtu kugombea, lakini kuna watu wanavyomuona ameketi na Lissu wanahoji kwa nini hawagombani huku akisema wenye fikra hizo watasubiri sana.

Awali, wakati maswali hayo yanaulizwa hasa kipengele cha kuhusu Mbowe kukaa muda mrefu, kulizua mjadala kwa wanachama waliokuwapo katika mkutano huo waliosikika wakihoji: “Nyie waandishi vipi, mnatupangia mwenyekiti?

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje ya Chadema, John Mrema aliingilia kati akiwataka wanachama hao kutulia na kuwaeleza kuwa maswali yote yaliyoulizwa yana majibu kutoka kwa viongozi.

Related Posts