NEMC yaionya migodi ya makaa ya mawe inayotiririsha maji yenye sumu

Songea. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewaonya wamiliki wa migodi ya makaa ya mawe mkoani Ruvuma wanaokiuka sheria na utaratibu wa uhifadhi wa mazingira.

Limesema endapo wataendelea kutiririsha maji yenye sumu kwenye vyanzo vya maji na mashamba ya wananchi, hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kutozwa faini ya Sh10 bilioni.

Utiririshaji maji hayo umekuwa ukisababisha athari kubwa za kiafya kwa jamii na uchafuzi wa mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Desemba 10, 2024 katika ukumbi wa mipango wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria wa NEMC, Jamal Baruti amesema ukaguzi umefanyika katika migodi 16 kati ya 18 iliyoko mkoani humo.

Ukaguzi huo umebaini changamoto kadhaa, ikiwemo ya utiririshaji wa maji yenye tindikali kwenye vyanzo vya maji.

Baruti amesisitiza kuwa NEMC haitakubali uzembe na itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 kwa ufanisi.

“Hatutamuonea mtu wala kuwa na muhali. Sheria itafuatwa kwa ukamilifu,” amesema.

Kwa mujibu wa Baruti, ukaguzi huo uliofanyika kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 8, 2024, katika wilaya za Madaba, Songea, Nyasa na Mbinga, ulibaini baadhi ya mashimo ya migodi yalijaa maji ya tindikali yanayotokana na mchanganyiko wa maji, hewa na madini ya salfa kutoka kwenye makaa ya mawe.

Amesema maji hayo yana athari mbaya kwa ubora wa ardhi, vyanzo vya maji, afya ya binadamu, wanyama na mifugo.

Akizungumzia migodi minane na vituo vitatu vya kuhifadhi na kuuza makaa ya mawe, Baruti amesema inaendesha pia shughuli bila vyeti vya Tathmini ya Athari za Mazingira (TAM).

“Hii ni kinyume cha sheria, vyeti hivyo ni lazima wawe navyo kabla ya kuanza shughuli zozote za uchimbaji au uhifadhi wa makaa ya mawe,” amesema Baruti.

Amesema mmiliki kama hana cheti hicho ni wazi kuwa mgodi wake haujakaguliwa na anatakiwa achukuliwe hatua kwa kuwa anafanya kazi bila kufuata utaratibu.

Naye Meneja wa NEMC Kanda ya Kusini, Mhandisi Boniphace Guni amesema ukaguzi huo ulibaini pia migodi mitano iliyotelekezwa bila kurekebisha mazingira yake baada ya uchimbaji. “Maeneo yaliyotelekezwa yana mashimo yaliyofurika maji yenye tindikali, hali hii ni hatarisha kwa mazingira na maisha ya viumbe hai,” amesema Guni.

Hata hivyo, Guni amesema tayari Baraza limeshatoa maelekezo kwa wamiliki wa migodi na vituo kufanya marekebisho maeneo yote yanayochimbwa makaa ya mawe.

Amefafanua jambo hilo haliwezi kufumbiwa macho, bali hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale watakaoshindwa kufuata maagizo hayo.

Related Posts