PROF. MKENDA AENDELEA KUPAMBANIA WANANCHI ROMBO.

NA WILLIUM PAUL, ROMBO.

MBUNGE wa Jimbo la Rombo mkoani Kilimanjaro, Prof. Adolf Mkenda ameendelea kuhakikisha tatizo la upatikanaji wa maji safi kwa wananchi wa Jimbo hilo linageuka kuwa historia ambapo amekabidhi rola tano za bomba kwa kuboresha miundombinu ya maji kata ya Motamburu kitendeni.

Akikabidhi mabomba hayo, Prof. Mkenda ambaye pia ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia alisema kuwa, serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikipambana kuhakikisha inamtua mama ndoo kichwani ambapo imetoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maji katika jimbo hilo.

Alisema kuwa, wananchi wa kata hiyo walikuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji ambapo walimuomba kwa barua kuwasaidia rola tano za bomba ili kutatua tatizo hilo ambapo amewasilisha kwao.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Rombo, Raymond Mangwala ameitaka mamlaka ya maji Rombo (Rombowsa) kuhakikisha bomba hizo zinafungwa haraka ili lengo lililokusudiwa la wananchi kupata maji linafanyika kwa vitendo.

Mangwala alisema kuwa, kwa sasa tatizo la upatikanaji wa maji safi katika wilaya hiyo limezidi kupungua na hii ni kutokana na serikali kutoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi mbalimbali. 


Related Posts