Profesa Sedoyeka: Madarasa mtandao yatatupeleka kimataifa

Arusha. Chuo cha Uhasibu Arusha (IIA), kimepanga kuanza kutumia madarasa mtandao, ili kuwezesha kutoa elimu kwa kundi kubwa la wanafunzi ndani na nje ya nchi na kukifanya kwenda na mabadiliko ya teknolojia kwenye ufundishaji.

Madarasa hayo ya yanayotumia vifaa vya kisasa vya Tehama yatamwezesha mwalimu atakayekuwa darasani kwenye kampasi zake za Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Babati  Manyara na Songea kufundisha wanafunzi wengi kwa wakati mmoja na kwa maeneo tofauti.

Hayo yamesemwa leo Jumanne, Desemba 10, 2024 na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Eliamini Sedoyeka, wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari, juu ya maendeleo ya chuo hicho kilipotoka, kilipo na kinapokwenda.

Amesema kampasi za Babati na Dodoma zimekamilika kwa sehemu kubwa, zikibaki kufanya udahili, huku akisisitiza fedha za mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) wa Dola za Marekani milioni 21, zimewezesha maboresho na mabadiliko hayo.

Amefafanua kuwa mabadiliko hayo  yatakifanya kuwa chuo kikubwa nchini kwa kuwa na miundombinu bora, wahadhiri na  wanafunzi wengi.

Aidha, chuo hicho pia kimepanga kufungua kampasi katika nchi za Comoro na Sudan Kusini.

“Tunaendelea kujenga madarasa smart, yaani mwalimu akiwa mfano hapa Arusha, anakuwa na uwezo wa kufundisha wanafunzi kwenye kampasi zetu zote na wanafunzi wanakuwa na uwezo wa kushiriki kikamilifu ikiwemo kuuliza maswali na kuchangia,” amesema Profesa Sedoyeka.

Ameongeza kuwa teknolojia hiyo haitotumika katika ufundishaji, bali hata ufuatiliaji wa maendeleo ya taaluma kwa wanafunzi.

“Kuna wanafunzi wanakuja hapa mwaka wa kwanza wako vizuri, lakini anapoingia mwaka wa pili na wa tatu anashuka, kwa kutumia teknolojia hii mwalimu anaweza kujua na kumfuatilia maendeleo yake,” amesema Profesa Sedoyeka.

Amesema maboresho na mabadiliko yote wanayoyafanya yanazingatia watu wenye ulemavu akisisitiza: “Ulemavu usiwe sababu ya mtu kukosa elimu. Tunahakikisha tunaweka mazingira rafiki kwa wao kupata elimu. “

Mkuu huyo wa chuo amesema ili kukifanya chuo kufikia hadhi ya kimataifa wamewapeleka wahadhiri wake kusoma vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi ikijumlisha  masomo ya uzamivu (PhD).

Ataja mwarobaini wa kilio cha ajira nchini

Katika hatua nyingine, Profesa  Sedoyeka  amesema kilio cha ukosefu wa ajira kwa wanaomaliza vyuo nchini, kinaweza kupungua iwapo watazalishwa wahitimu wanaozalisha ajira badala ya wanaotafuta ajira.

Akitolea mfano wa kinachofanywa na taasisi yake,  amesema chuo hicho mbali ya kuwapa wanafunzi ujuzi na weledi, kina programu za uanagenzi na pia kinawawezesha wanafunzi kuanzisha na kusajili kampuni changa.

“Tunaamini hili linaweza kuongeza idadi ya ajira. Nchi ni kubwa na ina opportunities ( fursa) nyingi, muhimu muhitimu achague anataka kufanya nini, ” amesema.

Kwa upande wake, mwanzilishi wa kampuni ya  Career na Mimi, Rahman Mbahe ambaye pia ni mwanafunzi wa stashahada chuoni hapo, amesema yeye na wenzake, walianzisha taasisi hiyo ikijihusisha na uvumbuzi, elimu, usawa wa kijinsia na afya njema.

“Tangu tumeianzisha tukiwa hapa hapa chuoni, tumewasaidia wenzetu. Lakini hata tukiwa likizo sasa tunaweza kuwa na kitu cha kufanya na nimeweza kukutana na watu tofautitofauti na haya ni matunda ya chuo kukubali na kuendeleza vipaji vyetu,” amesema Mbahe na kuiomba Serikali kutoa kipaumbele kwa vijana.

Related Posts